Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini Mhe, Hussein Bashe (kushoto) akibadilishana mkataba wa thamani ya shilingi milioni 20 na Meneja wa huduma kwa jamii wa Airtel Bi Hawa Bayumi (kulia) mara baada ya kusaini mkataba huo Nzega na kushudiwa na mkuu wa wilaya wa Nzega Mh, Godfrey Ngupula. mkataba huo unaunganisha Airtel FURSA na asasi iliyoundwa kimikakati na Mbunge huyo ya Nzega Urban Trust Fund kwa lengo la kumaliza tatizo la umasikini wa kipato katika jimbo la Nzega Mjini, Programu hii itawawezesha vijana wajasiriamali waishio katika ya kata 10 zilizoko ndani ya Jimbo la Nzega Mjini mkoani Tabora kupata mikopo yenye riba nafuu itakayosaidia kutatua changamoto za ajira kwa vijana.
---
Kampuni ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Nzega Urban Trust Fund imeanza kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo katika mji wa Nzega mara baada ya kuzindua mfuko maalumu utakaowawezesha wajasiriamali kupata mikopo iliyo na riba ndogo na nafuu sana kwa lengo la kuendeleza miradi yao ya kibiashara!

Mradi huo ujulikanao kama “WanaNzengo Airtel Fursa” ulibuniwa kwa jitihada za Mbunge wa Nzega mjini Mheshimiwa na Hussein Mohammed Bashe na kuzinduliwa mwanzoni mwa mwezi Novemba chini ya udhamini wa Airtel na kuwekwa chini ya uratibu wa taasisi ya Nzega Urban Trust Fund. Programu hii ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo imeonyesha mafanikio katika hatua za awali kwa kuwezesha makundi 20 yenye wafanyabiashara zaidi ya 100 kupata mikopo.

Akiongea kuhusu mikopo hiyo Meneja Programu wa Nzega Urban Trust Fund, Bw. Felician Andrew alisema “Tangu kuzinduliwa kwa mpango huu tumepokea maombi mengi sana toka kwa wajasiriamali ndani ya mji huu wa Nzega na leo tunayofuraha kuwapatia mikopo watu wapatao 100 ndani ya vikundi 20 vya awali baada ya kutimiza taratibu zote na kukidhi vigezo vya kupewa mikopo hii. Tunaamini hii sasa itakuwa fursa pekee kwa wafanyabiashara na wakazi wa Nzega kukuza biashara zao”

Aliongeza kwa kusema “Mikopo hii tunayotoa imelenga kukuza mitaji ya wafanyabiashara wadogo wadogo na ndio maana riba yake ni ndogo sana kwani tunatoza asilimia 1 kama riba. Tumeweza kufanya hivi kwa vile Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel ilituwezesha kwa kutupatia fungu la fedha kiasi cha shilingi million 20 ili kutekeleza program hii ambayo ni endelevu na Airtel wamefungua mlango wa fursa!”.

Ili kupata mkopo ikiwa wewe ni mjasiliamali na mkazi wa Nzega unatakiwa kujaza fomu ya maombi ya mkopo, ukiwa katika kikundi kisichozidi wala kupungua idadi ya watu 5 ambao wote mnapaswa kuwa watumiaji wa Mtandao wa Airtel, kwa kuwa fedha hizi hutolewa kwa mfumo wa Airtel Money.

Ni matumaini yetu wajasiriamali watatumia fursa hii vyema katika kuinua mitaji yao lakini vilevile sisi tumejipanga ili kuhakikisha tunawafikia wafanyabiashara wengi zaidi. Mpango wetu ni kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka huu tuweze kuwawezesha takribani wafanyabiashara 200 kupitia programu hii.

Kwa upande wake meneja huduma kwa jamii wa Airtel , Hawa Bayumi alisema”Airtel tunaendelea kutimiza dhamira yetu kwa vitendo kupitia mradi wetu wa Airtel FURSA na kuwawezesha wajasiriamali wadogo wadogo hususani vijana kuinua uchumi wao. “WanaNzengo Airtel Fursa” ni sehemu ya mikakati yetu katika kuhakikisha tunafikia malengo yetu na kuinua shughuli za jamii inayotuzunguka.

Vikundi vilivyonufaika ni pamoja na C. C.M Vijana, Vumilia, Purity, Huruma, Upendo Group, Upendo Na Amani B.B.C, Unyanyembe, Luquman, Isamilo Soko Kuu, Maua, Mama Lishe Parking, Tofali Choma, Umoja Wa Wakata Tairi, Amka Na Badilika, Seba Akujiwe, Umoja Lingini, Nzega Tanzania Deaf Society, Upendo Magharibi, Sister Group Na Hamarzon.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: