Kampuni ya simu za mikononi ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania (TFF) itaendesha kliniki ya soka kwa vijana waliong’ara wakati wa michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Airtel Rising Stars awamu ya sita ambayo ilifika tamati Septemba mwaka huu kwenye uwanja wa Karume Jijini Dar es Salaam. Timu ya vijana ya Morogoro ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuifunga Ilala 1-0 huku Temeke wasichana wakiwafunga wenzao wa Kinondoni kwa changamoto za mikwaju ya penati na kutwaa ubingwa kwa upande wa wasichana.

Kliniki hiyo ambayo lengo lake ni kuwapa vijana fursa nyingine ya kukuza vipaji vyao itafanyika Januari 2017, huku ikihudhuriwa na vijana 65 wavulana na wasichana ambao wamepatikana kwenye mikoa ya Arusha, Lindi, Kinondoni, Ilala, Temeke, Zanzibar, Mbeya, Mwanza na Morogoro ambayo ilishiriki kwenye Airtel Rising Stars 2016.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Soka la vijana nchini Ayoub Nyenzi alisema kliniki ya Airtel Rising Stars itatoa nafasi kwa vijana kuchanguliwa kijiunga na timu za Taifa ikiwemo Serengeti Boys. Kwa miaka mitano iliyopita, TFF imekuwa ikitumia michuano ya Airtel Rising Stars kuchagua wachezaji wa timu zetu za Taifa. Hii imekuwa na mafanikio makubwa kwani timu ya Serengeti Boys inawachezaji 11 waliochanguliwa kutoka michuano iliyopita ya Airtel Rising Stars. Nachukua nafasi hii kutoa pongezi kwa Airtel Tanzania kwa kudhamini michuano ya vijana kwani ndio msingi bora wa mchezo wa soka. Naamini kwa pamoja tutaendelea kupata matokeo ya kuridhisha, alisema Nyenzi.

‘Airtel imewezesha TFF kufika maeneo kadhaa ya nchi ambayo hapo awali ilikuwa ngumu kufika kutafuta vipaji vya soka. Kwa kuongezea, TFF imezindua Ligi ya Taifa ya Wanawake. Nachukua fursa hii kuwaomba viongozi wa timu hizi kujitokeza wakati wa kliniki hii hili wapate fursa ya kuchagua wachezaji wa kujiunga na timu zao, alisema Nyenzi.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde alisema Airtel inajivunia kuwekeza kwenye maendeleo ya soka la vijana kwa miaka mitano iliyopita na kusema kampuni yake itaendelea kudhamini michuano ya Airtel Rising Stars kwa lengo la kuendelea kukuza soka la Tanzania pamoja na kutoa ajira kwa vijana wetu.

Tunatoa pongezi kwa serikali kupitia Wizara ya Habari, Michezo na Sanaa na TFF kwa kuendelea kuunga mkono michuano hii. Bila ushirikiano wa serikali na wadau wa mpira wa minguu nchini, Airtel Rising Stars isingekuwa na mafanikio kama haya, alisema Matinde.

Kliniki ya Airtel Rising Stars itakuwa ya siku sita na itaendeshwa na makocha wa timu za Taifa za vijana akiwemo Mkurugenzi wa ufundi wa soka la vijana Kim Poulsen. Kliniki hiyo itakuwa ndio hitimisho la Airtel Rising Stars 2016 na itatoa fursa kwa maandalizi ya uzinduzi wa michuano ya Airtel Rising Stars msimu wa saba.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: