Leo tuzungumzie sifa za mtu kuwa dereva. Kwa maana ya kwamba kwa kupata leseni ya kuendesha gari na/au kuwa kwenye usukani unatarajiwa kwamba unasifa au umekidhi sifa gani. Lakini kabla ya kwenda huko tuangalie kwanza sheria inasema dereva ni nani?

Kwa mujibu wa Kifungu cha 3 cha sheria ya Usalama Barabarani, dereva ameelezewa kama ifuatavyo:

(a) Kwa upande wa magari , dereva ni mtu yeyote ambaye anaendesha au kujaribu kuendesha au ni msimamizi wa gari wakati huo na pia mkufunzi wa udereva atakuwa dereva pia;

(b) Kwa upande wa wanyama, dereva ni mtu yeyote anayewaongoza wanyama, akiwa mmoja au kundi barabarani;

(c) Kwa upande wa gari linalovutwa, dereva ni mtu yeyote anayeliendesha gari linalovuta gari jingine.

Sifa za kuwa dereva wa gari (Motor Vehicle).

Ili mtu aruhusiwe kuendesha gari, mtu yeyote anatakiwa kukidhi sifa zifuatazo:

1. Awe na ujuzi wa kutosha kuendesha gari analoombea leseni (Kf 24)

2. Lazima awe na ufahamu wa sheria ya Usalama Barabarani, Kanuni za kuendesha barabarani (Highway Code), alama na michoro ya barabarani. (kf.24)

3. Asiwe chini ya umri wa miaka 18, na kwa kuendesha Mopeds asiwe chini ya umri wa miaka 16;(kf 25(4))

4. Awe na leseni halali kwa gari husika (Kif.19)

5. Awe na umri usiopungua miaka 21 ikiwa anataka kuendesha basi au gari la biashara na awe alishakuwa na leseni kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu;(kf25(4))

6. Kwa upande wa mabasi ya abiria umri ni kuanzia miaka 30 kwa mujibu wa sheria za SUMATRA.

Hivyo basi, *sifa namba 1,2&3 ndizo sifa kuu za msingi* ambazo zinahalalisha mtu kupewa leseni(sifa ya 4) na kuitwa dereva. Sifa nyingine zilizobaki ni sifa za ziada na endelevu.

Kwa mantiki hii basi mtu yeyote mwenye leseni akikutwa barabarani dhana (assumption) ni kwamba moja, amefuzu kuendesha gari husika, na pili, anazijua vema sheria za usalama barabarani, kanuni za kuendesha njia kuu, alama na michoro ya barabarani.Na ndio maana akapewa leseni. Kama hangekuwa na sifa hizo asingekuwa na hiyo leseni. Na hii ndio sababu dereva akitenda kosa barabarani anakamatwa na kuadhibiwa.

Makosa ya Barabarani.

Sheria ya usalama barabarani tofauti na sheria nyingine nchini au duniani ambazo huwa zinaangalia nia ya mkosaji kufanya kosa (intention/mens rea) ndipo aadhibiwe, sheria hii huwa inaangalia kitendo (actus reus) tu na kuadhibu. Hivyo ukikamatwa barabarani ukajitetea kuwa haikuwa nia yangu kufanya hivyo, utetezi huo utakuwa dhaifu sana kukubalika mahakamani. Na ndio sababu ukiisoma sheria hii haitumiii maneno yanayoonesha nia ya kutenda kosa (intention) kama vile “any person who unlawfully, au any person who with intent to commit an offence au any person who intentionally au deliberately” nk.

Kwa lugha nyingine watu husema makossa ya kitrafiki ni “strict liability”. Yaani hayaangalii nia ili kuhalalisha adhabu, tofauti na sheria nyingien za kijinai ambazo kwa kiasi kikubwa ili mtu aadhibiwe huangalia nia(mens rea) na kitendo (actus reus). Maana yake ni kwamba kama upande wa mashtaka utashindwa kuthibitisha kuwa mtuhumiwa alikuwa na nia ya kutenda kosa, basi mtuhumiwa ataachiwa huru. Wakati kwenye kesi za trafiki Jamhuri inachopaswa kuthibitisha ni tu kuwa ulitenda kitendo husika, bila kujali ulinuia au la.

Ni matumaini utakuwa umelielewa somo hili vizuri. Hivyo ni wajibu wako kufanya juhudi kuzijua sheria za usalama barabarani, hasa kama unajua umesahau au ulipuuzia darasani au leseni yako uliipata kiujanja ujanja.

RSA TANZANIA
USALAMA BARABARANI NI JUKUMU LETU SOTE.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: