Wednesday, January 18, 2017

TIGO YAZINDUA TWENDE APP KUSAIDIA HUDUMA YA USAFIRI WA TEKSI NCHINI TANZANIA

Mkuu wa Zana za Kidijitali wa Kampuni ya Simu ya Tigo, Tawonga Mpore (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu kampuni hiyo kuzindua Twende APP kwa ajili ya kusaidia huduma ya usafiri wa teksi nchini. Kulia ni Mkuu wa Utawala na Fedha wa DTBi ambao ni wawezeshaji wa mradi huo, Mramba Makange na Mkurugenzi wa Idara ya Ubunifu wa Costech, Dk. Digushilu Mafunda.
Ofisa Mtendaji na Muasisi wa Twende App, Justin Kashaigili, akielezea jinsi ya kutumia mfumo huo kupitia simu ya mkononi.
Mkurugenzi wa Idara ya Ubunifu wa Costech, Dk.Digushilu Mafunda (katikati), akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Hassan Mshinda.
Wadau mbalimbali na waandishi wa habari wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Wapiga picha wakichukua tukio hilo.
Uzinduzi ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale

KAMPUNI inayoongoza kwa maisha ya kidijitali Tigo Tanzania leo imezindua huduma mpya ya kidijitali inayoitwa Twende App ambayo ni suluhisho la kuita teksi na hivyo kuwapatia wateja wake huduma sahihi na wanayoimudu ya usafiri wa teksi nchini Tanzania.

Kwa kuunganishwa moja kwa moja na madereva wa teksi, huduma hiyo inawawezesha watumiaji kufurahia kiwango cha chini kuliko ambavyo wangetumia njia nyingine mbadala za mitaani. Twende App itakuwa na mawasiliano ya madereva teksi, bajaj na boda boda ambao wamehalalishwa na vyama husika vya madereva.

Akitangaza huduma hiyo mpya katika mkutano wa wanahabari jijini Dar es Salaam leo asubuhi , Mkuu wa Zana za Kidijitali wa Tigo Tawonga Mpore alisema, “Huduma hii ni kielelezo cha Tigo kujikita katika mageuzi ya mtindo wa maisha ya kidijitali kwa kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wateja wake. Tunaamini kwamba Twende App itatoa huduma nzuri kwa abiria kwa kuwaunganisha na madereva ambapo watapata huduma bora zilizo na gharama nafuu na zenye ufanisi wa hali ya juu.”

Mpore aliongeza: “Tunaamini kwa kutoa njia mbadala kwa usafiri uliopo wa teksi, tunaweza kusaidia kuboresha usafiri kwa ujumla nchini Tanzania. Tunafahamu msongamano wa vyombo vya usafiri uliopo jijini kwa sasa; hivyo tunalenga kuwa sehemu ya suluhisho katika kutatua adha hiyo.

Kimsingi tunaamini kupunguza usumbufu katika barabara za jijini na kupunguza athari za kimazingira zinazotokana na msongamano wa magari ikiwa ni sehemu ya kukua kwa uchumi.”

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Hassan Mshinda ambaye alisema: “Napenda kumshukuru mbia wetu Tigo ambaye kila mara amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wajasiriamali wetu vijana katika teknolojia ya kisasa wanapata msaada muhimu katika kufikia malengo yao na kwa huduma hii naamini itawapatia fursa mpya zenye manufaa kwa madereva kote jijini.”

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Ofisa Mtendaji na muasisi wa Twende App, Justin Kashaigili alisema: “Nimesukumwa na kasi ya maendeleo ya miundo mbinu na nguvu ya ujasiriamali hapa nchini. Ninategemea kuwapatia wakaazi wa jiji la Dar es Salaam chaguo wanalolimudu, rahisi na linalofaa kwa ajili ya usafiri salama.”

Akielezea jinsi ya kujiunga na huduma hiyo, Kashaigili alisema, “abiria analotakiwa kufanya ni kupakua Twende App katika simu yake ambayo itamuunganisha na dereva moja kwa moja badala ya kuhangaika kwenda mwenyewe kufuata sehemu ilipo teksi. Huduma hii pia inatumia muda sahihi wa taarifa za dereva, mfumo hai wa satelaiti unaowezesha ramani ya kufahamu sehemu alipo abiria na kumuunganisha abiria mwenyewe na dereva aliyepo karibu na wakati huo huo kumwezesha dereva kutoa majibu.”

Twende App hivi sasa inatoa mbadala sahihi wa malipo kupitia Tigo Pesa kwa namba binafsi za Tigo Pesa kwa madereva na inapatikana katika mfumo wa Android na hivi karibuni itapatikana kwa watumiaji wa simu zilizo na mfumo wa iOs.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu