Thursday, February 9, 2017

EZEKIEL KAMWAGA: HESHIMA YANGU KWA SHAFFIH DAUDA

NIMEANZA kumfahamu Shaffih wakati angali mwanafunzi katika Chuo cha IFM. Nilikuwa na rafiki pale, Chunga Jaafar Misonge, na kila nikienda nilikuwa nikipewa habari zake. Kwamba jamaa ni shabiki wa kutupwa wa Man United na anaujua sana mpira wa Ulaya.

Mimi tayari nilikuwa mwandishi wa habari wakati huo. Kulikuwa na jambo lingine lisilo la kawaida kwa watu wa umri wangu, kama Shafi, kwamba alikuwa anaonyesha mechi za Ligi Kuu ya England palepale chuoni kwa wanafunzi kulipia.

Kwamba ingawa alikuwa mwanafunzi, Shaffih tayari alikuwa na mawazo ya kutengeneza fedha. Kama Dauda anatengeneza fedha hadi leo, ni kwa sababu ujasiliamali uko kwenye damu yake. Tukafahamiana kijuujuu tu wakati huo kupitia Chunga.

Baadaye aliajiriwa pale Twiga Bancorp ambayo kwa bahati nzuri nami nilikuwa mteja wa benki hiyo. Mara moja moja kama yuko dirishani nami nimeenda pale, tungeweza kuzungumzia mpira kidogo; mimi na Liverpool yangu naye na Man (SIX) yake.

Halafu akaacha kazi yake benki na kujiunga na Clouds Media. Hili la kuacha kazi pia si la kawaida. Unaacha kazi ya kitu ulichosomea na kujiunga na dunia mpya kabisa!!!

Shafi sasa ni mwandishi wa kipekee katika tasnia ya michezo hapa nchini. Ndiye mwandishi wa habari wa kizazi chake ambaye amesafiri zaidi kwenda nje ya nchi kuhudhuria matukio MAKUBWA ya kimichezo duniani.

Wakati akiingia kwenye tasnia, waandishi wengi wa Tanzania walikuwa wakisafiri kwenda ama kuhudhuria mechi za kimataifa za Taifa Stars, Simba au Yanga. Walikuwa wakisafiri, lakini si kwenye mashindano ambayo timu za Tanzania hazishiriki.

Ninapoandika makala hii, Shafi amehudhuria karibu mashindano yote makubwa ya kidunia. Kuanzia Kombe la Dunia, Kombe la Ulaya, Ligi Kuu ya England na karibuni zaidi Kombe la Mataifa ya Afrika.

Ingawa tangu zamani alikuwa akipenda mpira, Shafi wa leo si yule wa miaka 10 iliyopita. Leo anajua mpira na anazijua biashara za kwenye mpira. Na kwa sababu anakwenda mwenyewe viwanjani kuna faida nyingine ndogondogo anazipata.

Sijasahau usiku mmoja, miaka michache iliyopita, wakati Shafi aliponitamkia kwa mara ya kwanza jina la klabu ya Ujerumani. Mimi nilizoea kulitamka Schalke 04 (Shalke Zero Four). Shafi akaenda Ujerumani na akaleta tamshi jipya Schalke Nol Fiya (Kwa Kijerumani, 0 ni Null na Nne ni Vier).

Mimi ni Mtanzania na Mswahili, lakini Waingereza waliniharibu na kutamka jina la klabu ya Kijerumani kwa lugha yao, kitu ambacho si sahihi. Leo sisemi tena Zero Four kama ilivyokuwa zamani. Na hii ni shukrani kwa Shafi.

Shafi amekuja baada yangu lakini amenifundisha vitu vingi. Na bado naendelea kujifunza kutoka kwa wengine wanaochipukia hivi sasa.

Nimeamua kuandika hivi kwa sababu mara nyingi tumekuwa na tabia ya kuwasifia watu wakati hawapo duniani. Wakiwa wazima tunafanya kila jitihada kuwakatisha tamaa. Wakiondoka sifa tele.

Na labda naweza kutangulia mimi kabla ya Shaffih. Nisije nikaondoka pasipo rafiki yangu huyu kujua kwamba kwa kweli ninamheshimu sana.

Na hili halimaanishi kwamba Shafi hana mapungufu. Anayo ya kwake. Lakini namimi nina ya kwangu pia. Sote tu binadamu. Nimekataa kufungwa na kongwa la minyororo ya kutazama kasoro za watu na si mafanikio.

Nataka nifanye jambo moja kwenye maisha yangu ya uandishi wa habari. Kwamba sasa ifike mahali nami niwe nasafiri kuyafuata matukio makubwa ya kihabari yanayofanyika duniani. Mimi nafanya habari za siasa na nadhani matukio yangu yatakuwa ni ya siasa.

Lakini, kabla sijaianza hiyo safari, nilitaka Shaffih Dauda walau ajue kwamba yeye ndiye aliyekuwa Fuente de Inpiracion.

Shafi, Keep It Up !

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu