Afisa Rasilimali Watu wa GAPCO Tanzania, Chrispin Kayombo akitoa msaada wa baiskeli kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Matumaini ya Jeshi la Wokovu, Masoud Omary Babu ili kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu. Katikati ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Luteni Thomas Sinana huku wanafunzi wakishuhudia.

Na Mwandishi wetu

GAPCO Tanzania ikishirikiana na Network 21 ya Afrika Kusini imetoa baiskeli kwa wanafunzi wenye ulemavu wa Shule ya Matumaini ya Jeshi la wokovu ikiwa ni sehemu ya mchango wa kampuni hiyo kwa jamii.

Akikabidhi msaada huo, Afisa Rasilimali Watu wa GAPCO, Chrispin Kayombo alisema waliguswa na mahitaji ya shule hiyo kwani wao pia ni sehemu ya jamii na wana jukumu la kusaidia hasa wale wenye mahitaji maalumu.

“Tumeshirikiana na Network 21 kuwasaidia hawa wanafunzi kufikia malengo yao kwani baiskeli hizi zitawasaidia kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo za kielimu. Ulemavu sio kushindwa na ndio maana tuko hapa leo kutoa msaada na kuwahimiza wasome kwa bidii,” alisema.

Alisema baiskeli nyingine zilikabidhiwa kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Pugu wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa shule hiyo, Luteni Thomas Sinana aliishukuru GAPCO na Network 21 kwa msaada huo na kuomba makampuni mengine pia yajitokeze.

“Tumefarajika mno kupokea msaada huu inatia moyo sana kuona jinsi mnavyowakumbuka watu wenye mahitaji mbalimbali katika jamii hususani wenye ulemavu. Kama mlivyoona, wanafunzi hawa wana mahitaji mengi kama chakula, madaftari, vitabu, kalamu, sare za shule na ndio maana natoa wito kwa makampuni mengine pia wajitokeze kutusaidia, alisema.

Alisema watu wenye ulemavu wakiwezeshwa wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika jamii kwani wana uwezo pia.

Kaka mkuu wa shule hiyo, Ernest Timothy, aliishukuru GAPCO kwa msaada huo na kusema baiskeli hizo zitawasaidia mno katika masomo yao.

“Tumefarajika na kuguswa mno kuwaona hapa leo na kitendo cha kutukumbuka na kutuletea msaada huu kina maana kubwa sana kwetu ndio maana mnaona sote tuko hapa kusema asante,” alisema na kuomba makampuni megine yaige mfano huo wa GAPCO.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: