Mkuu wa Wilaya ya Njombe (wa kwanza kushoto) Ruth Msafiri akipata maelezo ya shughuli za ujasiriamali zinazofanywa na wanawake wa kikundi cha Upendo katika maadhimisho ya siku ya wanawake Njombe
Afisa Ustawi wa jamii Halmashauri ya Mji Njombe Veronika akitoa elimu juu ya ukatili wa kijinsi na ulinzi na usalama wa mtoto kwa wanawake waliohudhuria kwenye maadhimisho hayo
Miongoni mwa washiriki wa maonesho akijipatia mahitaji kwa mojawapo ya kikundi cha ujasiriamali cha wanawake
Mkuu wa Wilaya ya Njombe akikabidhi mahitaji mbalimbali kwa mzee asiyejiweza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake.
Watoto wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi na wageni waalikwa mara baada ya kupokea zawadi zao kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake Njombe.

Hyasinta Kissima - Njombe.

Ni katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniania ambapo katika Mkoa wa Njombe maadhimisho hayo yamefanyika Kiwilaya katika Kijiji cha Nundu halmashauri ya Mji Njombe na kuhudhuriwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya amesema kuwa lengo la Serikali kupitia Halmashauri kutenga asilimia kumi za mapato ya halmashauri kuwezesha wanawake na vijana limekuwa ni jambo jema kwani kupitia mikopo hiyo wanawake wamekua wakiendelea kufanya shughuli zao za ujasiriamali na zimekuwa zinamsaada mkubwa kwa familia na uchumi wa taifa.

“Wanawake walioaminiwa wakapewa mikopo na mitaji wamefanya vizuri na familia zao ziko vizuri na hivyo hatuna budi kuendelea kuwaunga mkono.” Alisema Mkuu wa Wilaya.

Akikabidhi zawadi za kadi za CHF, madaftari, kalamu, sabuni, dawa za meno na miswaki kwa watoto yatima 30, na zawadi za mafuta, sukari sabuni, chumvi kwa wazee 15 wanaoishi katika mazingira magumu Afisa Maendeleo wa Halmashauri Yohana Kalinga amesema kuwa vifaa hivyo vinaonyesha ni upendo na huruma ya pekee wanawake waliojaliwa kwa kuwasaidia watu wenye uhitaji na wanaoishi katika mazingira magumu.

“Maadhimisho haya tungeweza kufanya sherehe kwa kula na kunywa lakini tumeona si jambo jema watoto wetu ambao wazazi wao wameshatangulia mbele za haki wakakosa vifaa vya shule, huduma za afya na kwa wazee ambao ndio baba zetu na mama zetu wakashindwa kujikimu kutokana na hali ngumu na wakati huo sisi tunasherehekea si jambo la Baraka. Kwa kutambua huruma tuliyonayo tumeona ni vyema katika maadhimisho hayo tukawasaidia wenzetu wenye uhitaji zaidi.” Alisema Afisa Maendeleo huyo.

Rehema Nswila ni miongoni mwa wanawake wajasiriamali walioshiriki katika maadhimisho hayo ambayo yeye amesema kuwa uchumi wa viwanda kwa upande wa wanawake hautafanikiwa iwapo wanawake hawatajishughulisha mahali pale walipo na shughuli za uzalishaji kwani wanawake wengi ndio wazalishaji wakubwa wa bidhaa hususani kwa upande wa shughuli za kilimo.

“Fursa tunaanzia mahali pale mwanamke ulipo fursa zipo nyingi sana inategemea fikra ulizonazo, ni kitu gani unachokifahamu na unamalengo gani ya kufikia yale malengo ambayo unataka kufikia.Kupitia maadhimisho hayo tunajifunza vitu tofauti tofauti kupitia wajasiriamali wa aina tofauti tofauti na shughuli wanazofanya.Unaweza ukajishughulisha mwenyewe kwa kile ambacho unaweza kuanza nacho.”

Awali maadhimisho hayo yalitanguliwa na zoezi la upandaji miti katika eneo la shule ya msingi Nundu na kufuatiwa na zoezi la kutembelea mabanda na kukagua shughuli mbalimbali za ujasiriamali zinazofanywa na wanawake wa Mkoa wa Njombe.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: