Meneja mkuu wa mgodi wa Bulyanhulu Graham Crew akikabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni 374 kwa mkuu wa mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga kwa ajili ya malipo ya ushuru wa huduma ya mgodi kwa halmashauri ya Nyang'hwale iliyopo mkoani Geita
Mkuu wa wilaya ya Nyang’wale Hamim Gwiyama akishikana mkono na Meneja mkuu wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu Graham Crew wakati wa makabidhiano ya hundi ya shilingi milioni 374
Meneja mkuu wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu Graham Crew (kushoto) akizungumza wakati wa kukabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni 760 kwa ajili ya malipo ya ushuru wa huduma ya mgodi kwa halmashauri ya Msalala iliyopo mkoani Shinyanga. Katikati ni katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela akifuatiwa na mbunge wa jimbo la Msalala Ezekiel.
Meneja mkuu wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu Graham Crew akishikana mkono na katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela wakati wa kukabidhi hundi ya shilingi milioni 760 kwa ajili ya halmashauri ya wilaya ya Msalala iliyopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog.
---
Mgodi wa dhahabu wa Acacia Bulyanhulu uliopo katika halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga umekabidhi hundi zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya malipo ya ushuru wa huduma kwa halmashauri ya Msalala iliyopo mkoani Shinyanga na halmashauri ya wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita.

Hafla fupi ya kukabidhi hundi hizo imefanyika Alhamis Machi 2,2017,katika ukumbi wa halmashauri ya Msalala wilayani Kahama na kuhudhuriwa na viongozi wa halmashauri na mikoa ya Shinyanga na Geita pamoja na viongozi mbalimbali kutoka mgodi wa Acacia Bulyanhulu.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo,Meneja mkuu wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu Graham Crew alisema fedha hizo ni malipo ya ushuru wa huduma kwa ajili ya kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2016.

Alisema fedha hizo ni asilimia 0.3 ya ukokotoaji wa ushuru wa huduma ya mgodi huo kwa kipindi cha miezi sita katika awamu ya pili kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2016.

“Mgodi umelipa shilingi za kitanzania 1,135,178,526/= na malipo hayo yamegawanyika katika halmashauri mbili kwa mujibu wa makubaliano na serikali ambapo halmashauri ya Msalala imelipwa shilingi milioni 760 sawa na asilimia 67 na Nyang’wale shilingi milioni 374 sawa na asilimia 33”,alisema Crew.

Aidha alisema mpaka sasa mgodi huo umelipa jumla ya shilingi bilioni 4.3 tangu mwaka 2014 kampuni ya Acacia ilipoanza kutoa malipo ya ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 ya mapato ghafi kwa halmashauri husika.

“Katika kipindi cha miaka hiyo minne halmashauri ya Msalala imelipwa zaidi ya shilingi bilioni 3.7 na Nyang’wale imelipwa shilingi bilioni 1.1”,aliongeza Crew.

Katika hatua nyingine Crew alisema mgodi huo unaendelea kushirikiana na serikali na wadau wa maendeleo ili kutekeleza miradi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma endelevu za kijamii na miundombinu katika jamii hususani katika elimu,barabara,umeme,maji na huduma za afya.

Wakipokea hundi hizo,mkuu wa mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga na Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela waliushukuru mgodi huo kwa kutimiza wajibu wa kulipa kodi na kuongeza kuwa fedha hizo zitatumika katika shughuli za maendeleo ya wananchi katika halmashauri za Msalala na Nyang'wale.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: