Na Ally Kamwe

HAYATI Nelson Mandela. Apumzike pema peponi. Siku katika siku zake bora alizoishi duniani aliwahi kusema,? kuwapuuza watu kwenye haki zao ni kuupima Ubinadamu wao.?

Huyu ni Nelson Mandela, baba wa taifa la Afrika Kusini.

Hayati Julias Kambarage Nyerere. Apumzike pema peponi. Siku katika siku zake bora alizowahi kuishi duniani aliwahi kusema " Utii ukizidi unakuwa uoga na mara zote uoga huzaa unafiki na kujipendekeza.?

Huyu ni Julias Nyerere, baba wa taifa la Tanzania.

Lakini William Penn Adair Rogers, au Will Rogers kama alivyofahamika na wengi kule Marekani katika shughuli zake za maigizo, aliwahi kusema ?Kitu muhimu kwa shujaa ni kuchagua wakati gani anatakiwa afe.?

Apumzike pia pema peponi Will Rogers.

Zaidi ya miaka 80 imepita tangu mwili wake ulipolazwa katika viwanja vya Forest Lawn Park, kule California.

Kwanini nimekwambia juu ya watu hawa?

Jibu ni rahisi sana.

Msikie kwanza Warren Buffett, miongoni mwa mabilionea wanaojua kuitafuta na kuitumia hela, alisema ?Nionyesha shujaa wako, nikwambie mwisho wako utakavyokuwa.?

Mimi shujaa wangu ni Mh Nape Moses Nauye.

Aliyekuwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo. Sekta ambayo kalamu yangu ilikuwa inafanya kazi chini yake.

Kwanini Nape?

Hili ni swali la kwanza ninaloweza kuulizwa na jibu lake ni rahisi sana. Nape ?amekufa? wakati aliotakiwa kufa.

Wakati ambao tasnia ya habari ilimuhitaji zaidi kusimama na kusema, alisimama na kusema. Bila uoga, bila hofu, bila unafki, Nape alisimama na kuitetea tasnia ya Habari.

Ieleweke.

Wanahabari hatuna tatizo na Mh Harrison Mwakyembe, hatuna tatizo pia na maamuzi ya Mh Rais, sikitiko letu ni kuwa ?tumempoteza Nape wakati ambao tulimuhitaji zaidi.?

Sisi kwetu hatujapoteza Waziri tu. Tumepoteza rafiki, ndugu, kaka, kiongozi mwenye kujua na kuthamini jasho la mwingine. Tasnia ya Michezo imepoteza mtu huyu.

Ben Frankil, mwanasiasa wa zamani wa Marekani aliwahi kusema ?Asiyeweza kutii, hawezi kuongoza.? Nape alikuwa mtiifu kwetu.

Wote. Si waandishi pekee. Hata Waigizaji, Wanamuziki, Wachoraji, wachezaji na wote walio kwenye tasnia ya michezo na sanaa kwa ujumla, wamelia kwa ajili ya Nape.

Kwanini tunaamini Nape ni shujaa?

Mbali na uthubutu aliokuwa nao kwenye kutatua matatizo ya Wana habari, Nape ndiye aliyesimama peke yake na kumtetea Diamond Platinumz baada ya kumkabidhi bendera alipokwenda kutumbuiza kule Gabon.

Alisimama peke yake akiamini alichokiamini. Waliosema amekosea, alijibu kifupi tu, ?nimefanya kosa lenye faida?. Huu ndio ushujaa tunaozungumzia.

Kwa mwaka mmoja tu aliokaa Wizarani, Nape alikutana na Wahariri na kuzungumza nao, alikutana na waigizaji na kuzungumza nao, alimfata Diamond akazungumza nae, akajua kero za watu wake na kuanza kuzifanyia kazi.

Huyu ndiye shujaa tunayemlilia.

Mwandishi wa zamani wa Marekani, Joseph Campbell aliwahi kumuelezea shujaa kuwa ni mtu anayeamini kuna kitu kingine muhimu zaidi ya maisha yake.

Nape ni shujaa wetu kwa kuwa alitambua kuwa kero zetu ni muhimu kuliko kiyoyozi chake alichowekea ofisini.

Angeweza kukaa tu na kutatua ?kisayansi? kero zetu kama wanavyotatua viongozi wengine.

Katika kila uzinduzi wa Filamu nchini, iwe ndogo au kubwa, iwe usiku au mchana, ungemuona Nape katikati ya wasanii akiwapa moyo na kuwasapoti. Huyu ndiye shujaa tunayemtolea chozi!

Kiongozi ambaye aliweza kuzunguka na wasanii mchana wa Jua kali pale Kariakoo kujua kero za wasambazaji na namna wanavyoibiwa kazi zao.

Angetoka huko na bado usiku ungemuona kwenye uzinduzi wa bendi, akishiriki kwenye kupiga ngoma na magitaa.

Kama tukishindwa kumpenda Nape kwa hayo, tumpende kwa yapi tena mengine?

Tumesahau kuwa ni Nape ndiye aliyemsimamia na Mwanariadha Alphonce Felix Simbu, mpaka tukawa na majivuni tunayojivunia nayo leo hii kama Taifa?

?First lady? aliyekaa muda mrefu katika Ikulu ya Marekani, bibie Eleanor Roosevelt aliwahi kusema, ?Tumia kichwa chako kujiongoza, lakini tumia moyo wako kuongoza wengine.?

Kichwa cha Nape kilibaki nyumbani kwake, alipokuja kazini alikuja na moyo wake, aliipenda kazi yake na ndio maana kuna chozi linalomlilia leo hii.

Waandishi walimpenda Nape kwa sababu aliamua kwa kwa dhati kututumikia, si kweli kwamba ?Tulipendana?.

Hivyo hivyo kwa Wasanii na waigizaji, anayeondoka ni zaidi ya Waziri kwao.

Asingeweza kuandika na sisi, asingeweza kuigiza na kina JB, asingeweza pia kuimba na kina Ali Kiba, lakini alijisogea katikati yetu, tukaishi nae kama mwenzetu.

Nakumbuka mwigizaji wa Marekani, David Carredine aliwahi kuiasa dunia akisema ?Kama huwezi kuwa mshairi, kuwa shairi?.

Nape alikuwa shairi kwa kuwa alishindwa kuwa mshairi!
Kujali kwake kukazifanya nafsi za wote tuliokuwa chini yake kumpenda. Na siku zote kwenye upendo wa kweli, kuna Mungu pembeni.

Mungu akasimama kando yake na baraka zikaanza kushuka.

Kwa mara ya kwanza Watanzania wawili wakacheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa mara ya kwanza Samatta akabeba tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa Ligi za ndani.

Samatta akaenda Ulaya, akafunga sana na sasa tunasubiri kumuona kwenye robo fainali ya Kombe la Uropa akicheza dhidi ya Celta Vigo.

Unaweza kumsifu kwa juhudi zake binafsi, lakini ni ujinga tukiacha kuheshimu dua nyingi za Watanzania zinazosimama nyuma yake leo hii.

Sisi Watanzania ni wakarimu sana lakini si matajiri wa moyo wa kupenda mafanikio yaw engine, ukweli uko hivyo. Kwanini kwa Samatta tumeweza?

Moyo wa Nape uliingia kwenye Falme za Mbinguni na baraka zikashuka ndani yetu. Kwanini tusimlilie shujaa wetu?

Sipati picha baada ya miaka mitano au kumi, ndani ya Wizara, Nape angeleta mafanikio makubwa kiasi gani? Hamna anayejua zaidi ya kufungua milango na kumkaribisha Mh Mwakyembe.

Hatuna kinyongo nae hata kidogo, tunajua ni mtu safi na makini sana hivyo tuna sababu ya kunyamaza na kuanza kumsikiliza.

Tuna imani akifika ofisini, atasoma ramani ya tasnia ya michezo ilipo kwa sasa. Jukumu la kutuchagulia njia ya kupita liko kwenye himaya yake, tunamtakia kila la kheri!

Ally Kamwe ninachoweza kumwambia ni kitu kimoja tu, ?Kadri nyani anavyozidi kupanda juu zaidi, ndivyo anavyozidi kuyaanika makalio yake.?

Karibu Mh Mwakyembe.

Kalamu yangu ikomee hapa kwa leo na kama kuna niliowakosea kwa andiko hili ni vyema wakaziomba radhi nafsi zao kwa kulisoma, mimi nimesimamia kile alichowahi kukisema Lil Wayne.

?Ni dhambi kuomba radhi kwa kuwa mkweli?.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: