Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akizungumza na Mjumbe Maalum, Balozi Harro Adt aliyewasilisha Ujumbe Maalum kutoka kwa Kansela wa Ujerumani, Mhe. Angela Merkel kwenda kwa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Pamoja na mambo mengine walizungumzia pia namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Mazungumzo yakiendelea.
Waziri Mahiga akiagana na Balozi Adt mara baada ya kumaliza mazungumzo.
Waziri Mahiga (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mjumbe Maalum, Balozi Adt (wa nne kushoto) pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizarani pamoja na Ubalozi wa Ujerumani nchini.
---
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa Tanzania na Ujerumani zitaendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo yale yanayohusu kudumisha amani na usalama duniani pamoja na kuheshimu misingi ya haki za binadamu kupitia Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.

Mhe. Waziri Mahiga ameyesema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Balozi Harro Adt, Mjumbe Maalum wa Kansela wa Ujerumani, Mhe. Angela Merkel kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli alipofika Wizarani kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe huo.

Katika mazungumzo yao, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa, Ujerumani na Tanzania zina mahusiano ya kihistoria tangu enzi za ukoloni hadi sasa. Katika masuala ambayo Tanzania inanufaika na ushirikiano huo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu, maboresho katika sekta ya elimu na mchango katika uhifadhi wa wanayamapori.

“Uhusiano wa Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria tangu ukoloni. Hata hivyo Ujerumani wamejaribu kutafsiri ushirikiano wetu katika misingi bora sasa kuliko ile ya kikoloni. Ujerumani imekuwa ikiisaidia Tanzania moja kwa moja katika sekta mbalimbali kama elimu, wanyamapori na miundombinu na misaada mingine imekuwa ikipitia Umoja wa Ulaya” alisema Waziri Mahiga.

Akizungumzia ziara ya Balozi Adt nchini, Mhe. Waziri Mahiga alisema Mjumbe huyo Maalum wa Kansela wa Ujerumani ameleta ombi kwa Mhe. Rais na kwa Watanzania la kuiunga mkono Ujerumani kwenye nafasi ya Mjumbe asiye wa Kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa uchaguzi utakaofanyika mwaka 2018. Aliongeza kusema kuwa, Ujerumani imedhamiria kugombea nafasi hiyo ikiwa na dhamira ya kuunga mkono mageuzi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo kuziunga mkono nchi za Afrika kwenye harakati za kupatiwa nafasi mbili za kudumu kwenye Baraza hilo.

Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alifafanua kwamba, katika kufikia malengo hayo Ujerumani imejiwekea misingi mikuu minne ambayo ni:- Kusaidia jitihada za amani na usalama duniani; Kusimamia Haki ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; Kuhamasisha mageuzi ya Teknolojia na Kuhimiza ushirikiano na Ubia wa Kimataifa.

Mhe. Mahiga alieleza kuwa kwa kuzingatia misingi hiyo, amemueleza Balozi Adt azma ya Tanzania kuiomba Ujerumani iisadie Afrika kujenga Jengo la Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambapo Tanzania ndio Makao yake Makuu huko Mjini Arusha.

Mhe. Mahiga pia alimhakikishia Balozi Adt kuwa ameupokea ujumbe wa Kansela wa Ujerumani na atauwasilisha kwa Mhe. Rais.

Kwa upande wake Balozi Adt, Mjumbe Maalum kutoka Ujerumani alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata baada ya kuwasili nchini. Pia ana imani kuwa Tanzania ambao ni rafiki wa kihistoria wa Ujerumani itawaunga mkono kwenye nafasi hiyo ili kuwawezesha kutekeleza malengo waliyojiwekea ikiwemo kuhakikisha Afrika inapata nafasi mbili za kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 12 Machi, 2017
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: