Wednesday, March 22, 2017

WILAYA YA BAGAMOYO KUNUFAIKA NA VISIMA VIREFU 17

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba (kushoto) akiwa katika kikao cha majumuisho na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Maggid Mwanga mara baada ya kukamilisha ziara katika Wilaya hiyo.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba (Mb.) akiongea na Bi. Tatu Rajab mmoja wa wafanyakazi katika Kiwanda cha kutengeneza chumvi cha Sea Salt. Waziri Makamba alifanya ziara kiwandani hapo kuangalia changamoto za mazingira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi. Zainab Abdallah mara baada ya kutembelea kijiji cha Buyuni na kuongea na wananchi.
---
Na Lulu Mussa, Saadani - Pwani

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amesema katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake Ofisi yake imeandaa mradi utaonufaisha shule za msingi katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Akiwa Wilayani Bagamoyo Waziri Makamba amesema kuwa, moja ya changamoto kubwa ya Wilaya ya Bagamoyo ni ukame unaotokana na athari za mabadiliko ya Tabianchi, uliopelekea kupanda kwa kina cha bahari na kusababisha visima vilivyochimbwa pembeni mwa miji na fukwe za bahari kufukiwa na maji na chumvi.

"Ofisi ya Makamu ya Rais imeamua kuisadia Wilaya ya Bagamoyo kuchimba visima kumi na saba (17) virefu kwenye maeneo ambayo yameathirika na kupanda kwa kina cha maji na maeneo yenye ukame mkubwa" Makamba alisisitiza.

Takribani kila kisima kitagharimu kiasi cha Shilingi Milioni Hamsini na Ofisi ya Makamu wa Rais pia itaandaa mfumo wa kuvuna maji katika shule tano mradi utakao gharimu takribani Milioni mia moja sabini.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba alitembelea Kiwanda cha Sea Salt kilichopo Saadani, Wilaya ya Bagamoyo kuona namna kiwanda kinavyofanya kazi kwa kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.

Waziri Makamba ambaye amewasili Mkoani Tanga kujionea hali ya mazingira na changamoto za uhifadhi pia ametembelea Wilaya ya Pangani na kukagua mradi wa ujenzi wa Ukuta wa Pangani.

Waziri Makamba, amemtaka mkandarasi anayejenga ukuta wa mto Pangani kampuni ya ( DEZO CIVIL CONSTRUCTION L.TD ) kukamilisha ujenzi wa ukuta kwa kipindi cha muda wa miezi kumi, kama mkataba unavyoonyesha na kuzingatia ubora. Ujenzi huo wa sehemu ya ufukwe wa kaskazini ambao una urefu wa mita 950 ambazo kati yake mita 550 zipo katika ujenzi wa awali utagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 2.4

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi Zainab Abdalah amemuomba Waziri Makamba kutuma timu ya wataalamu kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kwa fukwe pekee iliyoko katika maeneo ya Tanga DECO ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa na athari zitokanazo na mabadiliko ya Tabia nchi na haipo katika bajeti kwa mwaka huu wa fedha.

Ziara ya kikazi wa Waziri Makamba leo imeingia siku ya pili na ametembelea Kijiji cha Buyuni ambapo pia alifanya mazungumzo na wakazi wa eneo hilo.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu