Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akizungumza na Mtendaji wa Kijiji cha Butu, Kata ya Jipe Wilayani Mwanga Bw. Nassor Abdul wakati Waziri Makamba alipotembelea Ziwa Jipe ambalo limeathiriwa kwa kiasi kikubwa na magugu maji ambayo yanasababisha kupungua kwa shughuli za uvuvi ambazo ndio chanzo kikubwa cha mapato kwa wakazi wa eneo hilo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Aron Mbogho.
Mifano kwa vitendo: Pichani Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. January Makamba akiwa amembeba mtoto Meshack Ombeni katika Kijiji cha Butu pembezoni mwa Ziwa Jipe. Waziri Makamba amewaasa wananchi hao kulinda Ziwa hilo ili liweze kunifaisha vizazi vijavyo na kuwatahadharisha kuwa uharibifu wa mazingira utahatarisha uhai wa ziwa hilo. .
Upungufu mkubwa maji katika bwawa la nyumba ya Mungu. Inasemekana kupungua kwa kina cha maji kunatokana na ukame wa muda mrefu na uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na shughuli za binadamu katika vyanzo vya maji vinavyopeleka maji katika bwawa hilo ukiwemo Mto Kikuletwa.

Na Lulu Mussa, Mwanga - Kilimanjaro

Imebainika kuwa Ziwa Jipe liko hatarini kutoweka endapo hatua za haraka hazitachukuliwa katika kulinusuru. Hayo yamesemwa leo na Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa Mazingira Mh. January Makamba alipofanya ziara ya kukagua ziwa hilo ambalo sehemu kubwa imezungukwa na magugu maji.

Waziri Makamba amesema kuwa ziwa hilo ni rasilimali muhimu na hivyo ni lazima kuwe na mpango wa muda mfupi na ule wa muda mrefu. Kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamiza wa Mazingira (NEMC) ameazimia kutangaza kupita Tangazo la Serikali kuwa eneo hilo ni eneo nyeti kimazingira."Tutatanga eneo hili kuwa eneo nyeti kimazingira na tutaweka masharti ya matumizi katika eneo hili" Alisisitiza Makamba

Azimio hilo la kutangaza kuwa eneo mahsusi ama nyeti kimazingira itasaidi katika kuandika maandiko mbalimbali ya miradi na kupata fedha kutoka kwa wadau na washirika wa maendeleo. Pia litawekwa chini ya uangalizi maalumu na kuweka masharti ya matumizi bora ya eneo hilo. " Tutaweka masharti makali na magumu zaidi ili watakao kiuka wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria" Aliongezea Waziri Makamba.

Aidha, Waziri Makamba amesisitiza kuwa ni vema kunusuru ziwa hilo sasa maana ndani ya miongo 2-3 huenda ziwa hilo likatoweka. "Bila hifadhi ya mazingira hakuna maisha, na ukiyaharibu mazingira hakuna msamaha yatakuadhibu tu" Akiongea katika Mkutano wa hadhara kijijini Butu, Waziri Makamba amesema kuwa shughuli zozote za maendeleo iwe uvuvi, kilimo, utalii, mifugo kwa namna moja ama nyingine zinategema hifadhi endelevu ya mazingira.

Katika hatua za muda mrefu Waziri Makamba amewataka wasimamizi wa Bonde la Pangani, Wizaya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kukutana mara moja kuandaa mpango na mtazamo wa pamoja wa kunusuru Ziwa Jipe.

Akiwa njiani kuelekea Nyumba ya Mungu Waziri Makamba alipitia katika Kiwanda cha Kifaru Quarries Co. Ltd na kukuta kikiendelea na uzalishaji wa kokoto bila kuwa na cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeutaka uongozi wa Kiwanda hicho kusitisha uzalishaji mara moja na kutakiwa kulipa faini kwa kukiuka Sheria ya Mazingira kifungu namba 81 na 196.

Waziri Makamba pia amefanya ziara katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na kufanya mkutano wa hadhara na wakazi wa kijiji cha Kakongo ambao kwa pamoja wamelalamikia zuio la kufanya shughuli za uvuvi katika bwawa hilo kutokana na kupungua kwa kina cha maji na samaki katika bwawa hilo.

Bw. Charles John Waziri Mkazi wa Kijiji cha Kagongo amesema kuwa kuna hujuma katika matumizi ya rasilimali maji ambapo imebainika kuwa wakulima wanaotumia kilimo cha umwagiliaji wamekua wakitumia maji kwa kiasi kikubwa na kusababisha upungufu katika bwawa.

Akijibu kero na malalamiko ya wananchi hao Waziri Makamba ameagizia kufanyika kwa doria na kuainisha pampu zote zinazovuta maji kutoka bwawani hapo "Naaagiza Mamlaka ya Wilaya ya Mwanga, Serikali ya Mtaa na Mamlaka ya Bonde Pangani kufanya doria na kuhakiki pampu zote kujua uhalali wake kama zimesajiliwa na kama zinavibali, zitakazobainika kutokuwa na vibali zote zitaifishwe" Alisisitiza Waziri Makamba.

Waziri Makamba yuko katika ziara maalumu ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira, changamoto na kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu wa kukabiliana nazo. Mpaka sasa Waziri Makamba ameshatembelea Mkoa wa Pwani, Tanga na Kilimanjaro.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: