Wednesday, May 31, 2017

BALOZI SEIF ALI IDD AKIONGOZA MAZISHI YA MAMA MZAZI WA VUAI ALI VUAI

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balosi Seif Ali Idd akipokelewa na viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali mara baada ya kuwasili katika mazishi ya Mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, huko kijijini kwao Bwejuu.
Viongozi mbali mbali wa Chama na serikali pamoja na wananchi wakiiombea Dua Maiti ya Bi. Mwanaisha Hassan Vuai ambaye ni Mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu Msitaafu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai katika msikiti wa kijiji cha Bwejuu.
Viongozi mbali mbali wa Chama na serikali pamoja na wananchi wakiiombea wakiwa msikitini kabla ya kuanza kuiswalia Maiti ya Bi. Mwanaisha Hassan.
Baadhi ya Viongozi na wananchi kwa upande wa wanawake wakiomba dua katika mazishi ya Marehemu Bi. Mwanaisha Hassan Vuai ambaye ni Mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu Msitaafu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai katika msikiti wa kijiji cha Bwejuu.
Matukio tofauti ya kubebwa kwa maiti inapotolewa msikiti hadi sehemu ya kaburi ilipofanyiwa mazishi.
viongozi mbali mbali wa Chama na serikali wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Nd. Abdulrahman Omar Kinana wakimfariji Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar katika mazishi ya Mama yake mzazi yaliyofanyika huko kijijini kwao Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja.( PICHA NA AFISI KUU CCM ZANZIBAR).

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MAMIA ya Wananchi wameudhuria mazishi ya Mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar.Vuai Ali Vuai, Marehemu Bi.Mwanaisha Hassan Vuai huko Kijijini kwao Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Mazishi hayo yameongozwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, aliyeambatana na viongozi mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na jamhuri ya muungano Tanzania.

Bi. Mwanaisha amefariki jana wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Tasakhtaa iliyopo Vuga Mjini Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya mazishi hayo, Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar, Nd. Vuai Ali Vuai alisema kifo cha Mama yake mzazi kimeacha pengo kubwa katika familia hiyo kwani marehemu huyo alikuwa akitegemewa na jamii kutokana na busara zake.

Aidha Vuai amewashukru wananchi mbali mbali waliojitokeza kumuunga mkono katika mazishi hayo na kuwasihi waendelee kuwa na umoja wa kushirikiana katika mambo mbali mbali ya kijamii.

“Mama yetu tulimpenda sana lakini ndio hivcyo amefariki sasa kilichobaki kwetu sisi tuliobaki ni kumuombea dua yeye pamoja na wazee wetu wengine waliofariki kabla yake.”, alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Mbali na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pia Mazishi hayo yameudhuriwa na Viongozi mbali mbali wakiwemo Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Omar Kinana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi”,Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Tanzania Shaka Hamdu Shaka, Mkuu wa Mkoa kusini Unguja Dk.Idrissa Muslim Hija, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu.

Viongozi wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Idrissa Kitwana Mustafa, Mnadhimu wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM, Ali Salum Haji pamoja na baadhi ya Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Makatibu wakuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Bi.Mwanaisha Hassan Vuai amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 85 ameacha watoto tisa (9) pamoja na wajukuu kadhaa.

Mungu ailaze roho ya marehemu pahali pema peponi-Amin.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu