Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala akizungumza wakati wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo watendaji na viongozi wa Majimbo 9 ya CCM na jumuiya zake Mkoa wa Mjini Unguja.
Washiriki wa mafunzo hayo wakisikiliza kwa makini Nasaha za Mgeni rasmi Dkt. Abdalla Juma Saadala huko katika ukumbi wa Mkoa huo Aman Unguja.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Saadala "Mabodi" amezitaka jumuiya za Chama hicho kutumia vizuri fursa ya uchaguzi kuwapitisha viongozi wenye sifa na uwezo wa kukiletea ushindi chama katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo viongozi wa majimbo Tisa (9) ya Chama na Jumuiya za Mkoa wa Mjini juu ya mabadiliko ya Katiba ya CCM ya 1977 yaliyofanyika hivi karibuni yaliyofanyika Katika ukumbi wa mkoa huo Aman Unguja.

Alisema uchaguzi unaofanyika hivi sasa katika kwa ngazi mbali mbali za Chama hicho ndio uwanja wa kuandaa jeshi kamili la kisiasa lililokamilika kila idara na lenye ujuzi na mafunzo yote ya vita ya kisiasa litakaloweza kupambana kwa ujasiri na kufanikisha ushindi katika uchaguzi mbali mbali za Dola ili CCM iendelee kushinda na kutawala kupitia utaratibu wa Kidemokrasia.

Aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo kutumia vyema mafunzo hayo ya siku moja ili waweze kuwa na uelewa mpana wa Mabadiliko kadhaa yaliyofanyika ndani ya katiba ya CCM ili watekeleze kwa ufanisi majukumu yao na kuwaelimisha wanachama wengine juu ya taaluma hiyo.

Dkt.Mabodi alieleza kwamba matarajio ya taasisi hiyo ya kisiasa ni kuona kasi ya mabadiliko ya kiutendaji kwa haraka hasa kwa viongozi na watumishi wa Chama na jumuiya zake.

Pia aliongeza kwamba mbali na matarajio hayo mafunzo hayo yatamaliza mizozo na malalamiko yaliyokuwa yalisababisha kutokuwepo kwa ufanisi mzuri wa kiutendaji kwa baadhi ya maeneo ndani ya Mkoa huo.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema hatovumilia tabia za kupangwa safu za viongozi kwani kufanya hivyo ni kukiuka Kanuni za maadili na miongozo ya uchaguzi huo.

" Tumekuwa tukisema siku zote kuwa CCM ndio mwalimu wa Demokrasia yaani hivyo vyama vya upinzani demokrasia na ustaarabu wa kisiasa tumewafunza sisi hivyo dhana hizo lazima tuzisimamie na kuzitekeleza kwa vitendo kupitia uchaguzi unaoendelea ndani ya taasisi yetu.", alisema Dkt.Mabodi na kuzitaka kamati za uchaguzi na maadili kufuatilia kwa kina mwenendo wa uchaguzi na watakapobaini kasoro watoe taarifa kwa ngazi husika ili zitafutiwe ufumbuzi wa haraka.

Alifafanua kwamba kupitia uchaguzi huo panatakiwa kupatikana viongozi na watendaji watakaoendeleza siasa za upendo, maendeleo, umoja pamoja na mshikamano unaojali misingi ya kidemokrasia ndani na nje ya taasisi hiyo.

Hata hivyo alieleza dhamira ya chama hicho kupitia mabadiliko yaliyofanyika katika Katiba ya Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kila mwanachama kujipanga kisaikolojia kusaidia kuimarisha uchumi wa CCM kupitia rasilimali zilizopo sambamba na kubuni miradi mingine ya kimaendeleo.

Sambamba na hayo kupitia Mafunzo hayo Dkt.Mabodi aliwakumbusha washiriki hao kwamba ili wafanikiwe katika utendaji wao ni lazima watumie vizuri rasilimali watu ya wazee wa CCM pamoja na wastaafu katika sekta za umma na binafsi kwani wana uwezo na uzoefu mkubwa wa kushauri na kutoa maelekezo mazuri juu ya masuala mbali mbali ya kiutendaji ndani ya Chama hicho.

Mapema akizungumza katika mafunzo hayo Mwenyekiti wa Mkoa huo, Nd. Bora afya Juma Silima alisema Mkoa huo umejipanga kufanikisha kwa ufanisi uchaguzi huo ili kulinda historia ya chama hicho katika kufanikisha uchaguzi unaoheshimu misingi ya utawala bora na demokrasia kwa wananchi wote.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: