Taa za furaha ziliwaka mioyoni mwetu, nyuso zetu zilitengenezwa na tabasamu ambalo lilitosha kuelezea furaha ya ushindi wa timu ya taifa ya vijana iliyochini ya umri wa miaka 17 yani serengeti boys.

Tafasiri halisi na nzuri kuhusu furaha ambayo Watanzania walikuwa nayo baada ya kupata ushindi dhidi ya timu ya taifa ya vijana ya chini ya umri wa miaka 17 ni kwamba Watanzania walikuwa wana uhaba wa furaha katika mpira wa miguu na wanahitaji tiba ya huu ugonjwa.

Daktari sahihi wa huu ugonjwa ameshaonekana na juhudi anazofanya kwenye matibabu ya ugonjwa wetu zinatia moyo sana na wengi tunaomba na kuamini kuwa tunaelekea kupata furaha ya kudumu.

Ni ngumu kutokuamini kuwa ndani ya kikosi cha Serengeti boys hakuna furaha ya kudumu , goli zuri la Yohana Mkomola linatosha kutuaminisha kuwa mguu wake uliletwa kwa ajili ya kufunga magoli kwa ajili ya furaha yetu.

Ni matamanio ya wengi wetu kwa Yohana Mkomola kufuata nyayo za kina Mbwana Samatta pamoja na Farid Musa hii ni kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kufunga unaochangiwa na yeye kuwa mtulivu na kujua sehemu sahihi ya kujipanga akiwa katika lango la adui.

Unaona nini ukimwangalia Kababange? Uwezo wake wa kukaba na kupandisha mashambulizi ya timu na kurudi haraka kuzuia mashambulizi pindi inaposhambuliwa hivi vyote vinatosha kukuonesha kuwa ndani ya Kakabange kuna beki wa kushoto mkubwa sana ambaye ana uwezo wa kucheza vizuri hata katika mazingira ya soka la kisasa, kwani pamoja na uwezo wa kucheza beki wa kushoto pia anauwezo wa kucheza kama Wingback katika mfumo wa kutumia mabeki watatu.

Haikuwa bahati, au hawakukosea kumpa mchezaji bora wa mechi Dickson Job. Uwezo wake mkubwa uwanjani ulikuwa na ushawishi mkubwa wa kuvikwa taji la mfalme wa mechi dhidi ya Angola.

Hii yote inaonesha timu yetu imejaza vipaji ambavyo vina uwezo mkubwa na vinatoa nafasi kubwa ya timu yetu kufika sehemu kubwa.

Muunganiko wa timu katika maeneo makuu matatu ya uwanja, yani eneo la ulinzi, kiungo na ushambuliaji linaonesha wazi kuwa timu hii imeundwa kwa mtindo wa kila mchezaji kutimiza majukumu yake kwa kiwango kikubwa.

Vipaji binafsi ni vingi na vinaonekana, lakini jambo kubwa lililofanywa na benchi la ufundi ni kuunganisha vipaji hivi vilivyopo kwenye timu na kuifanya timu icheze kitimu zaidi bila kumzunguka mchezaji mmoja kwa kiwango kikubwa na hii ndiyo sifa kubwa ya timu ya ushindi.

Timu imejengwa kiushindani na hii imejidhihirisha kwenye mechi mbili za kundi B, ya kwanza dhidi ya bingwa mtetezi Mali na hii ya Angola.

Matokeo waliyoyapata ni mazuri sana ila yasiwafanye wasahau lipi jukumu walilonalo kwa Watanzania. Hatima ya furaha ya Watanzania kwa sasa iko katika mikono yao.

Viganja vyao ndivyo vimebeba hatima ya kutengeneza tabasamu la Watanzania. Furaha ya muda mrefu itakuwa katika mikono yao ambayo tumeiamini ni salama kwetu.

Ni wakati kwao kufuta kumbukumbu ya matokeo ya mechi zilizopita katika akili zao na kuweka picha ya kwamba wanadeni kubwa la kuwapa ushindi Watanzania.

Ni muda sahihi kwao kutamani medali za kombe la Afcon kwa vijana wa umri chini ya miaka 17 kwa sababu medali hizi zitasaidia kunogesha utamu wa soga na wajukuu zao pindi watakapozeeka.

Matamanio chanya ya kufika India kushiriki kombe la dunia la vijana waliochini ya umri wa miaka 17 yawajae.

Roho ya upiganaji, upambanaji na ufiaji wa nchi iwe ndani yao. Matokeo mazuri waliyoyapata yasiwe chanzo kwao kushusha morali kwa sababu ya kubweteka na matokeo haya.

Vita bado mbichi hatujajihakikishia ushindi mbele ya wapiganaji wenzetu.

Silaha zetu zihusike kwa kiasi kikubwa katika vita hii.

Ni wakati sahihi kwa wachezaji kukumbuka jukwaani kuna mawakala na mascouts wengi.

Ukiachana na kuipigania nchi yetu, wachezaji wanatakiwa wajue wanapigania maisha yao. Macho ya mawakala na mascouts mbalimbali waliomiminika katika viwanja vya Gabon yatashawishika kwa ubora utakaooneshwa na wachezaji wetu, ndiyo maana nawakumbusha mwisho wa vita haujafika kwani vita ndiyo inaanza wanatakiwa wajidhatiti zaidi.

Kila la heri jeshi la furaha la Tanzania, jasho lenu ni damu tosha ya kutengeneza furaha yetu.

Martin Kiyumbi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: