Wabunge wa Chadema, na makada wao pamoja na Wakili Wao Peter Kibatala wakifurahi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kiachiwa huru kwa kuonekana hawana kesi ya kujibu dhidi ya tuhuma iliyokuwa inawakabili ya kumjeruhi Katibu Tarafa Mkoa wa Dar es Salaam Theresia Mmbando.
Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru wabunge watatu wa Ukawa na Makada wao baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu. Wabunge hao na wenzao walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresa Mmbando.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kiridhika kwamba ushahidi ulioletwa mahakamani hapo haukuwa unatosha kuwakuta washtakiwa na kesi ya kujibu.

Amesema kuwa katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibisha kwani, hata mlalamikaji Mmbando hakumbuki ni nani alimjeruhi. Ameongeza kuwa, ushahidi wake ulielezea tu Jinsi washtakiwa walivyojishughulisha na nyaraka siku ya tukio na siyo kumjeruhi.

Kuhusu kushikwa matiti, Hakimu Shaidi alisema kitendo hicho kingeweza kupelekea mlalamikaji kufungua kesi nyingine lakini siyo kujeruhi.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka uliita mashahidi watatu kutoa ushahidi ambapo hakuna ushahidi ulioweza kuwatia hatiani watuhumiwa hao na kukutwa na kesi ya kujibu.

Wabunge walioachiwa huru ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara, Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema , mfanyabiashara na kada wa chama hicho, Rafii Juma na Diwani wa Kata ya Saranga Kimara, Ephreim Kinyafu.

Ilidaiwa kuwa Februari 27, 2016 katika Ukumbi wa Karimjee wilaya ya Ilala jiji la Dar es Salaam walifanya kosa la kumjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha.

Mmbando katika ushahidi wake alieleza jinsi alivyovamiwa, kujeruhiwa na kupokonywa faili lililokuwa na ajenda na muongozo wa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa jiji la Dar es Salaam uliopaswa kufanyika Februari 27, 2016.

Alidai kuwa siku hiyo ya Februari 27, 2016 alipewa jukumu la kuusimamia uchaguzi huo wa Meya na Naibu Meya ambao ulipaswa kufanyika nyakati za saa 4 asubuhi katika ukumbi wa Karimjee.

Kama Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa ni Mwenyekiti wa uchaguzi huo, wajumbe wote walifika, Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Salehe Yohana ambaye alikuwa Katibu alifungua uchaguzi huo kwa sababu koramu ya wajumbe ilikuwa inajitosheleza.

Baada ya kikao kufunguliwa na Katibu huyo Salehe alisema uchaguzi huo hautaweza kufanyika kwa sababu amepokea zuio la mahakama la kuzuia uchaguzi huo kuendelea na akawaalifu wajumbe.

Baada ya uchaguzi huo kuahirishwa, wajumbe wa CCM walitoka nje lakini wajumbe wa vyama vingine wakiwamo Ukawa walimvamia wakisema aendeshe uchaguzi huo.

“Walinifuata mezani nilipokuwa nimekaa wakitaka niendelee na uchaguzi huo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alilivuta faili lililokuwa na muongozo wa uchaguzi huo na katika tukio hilo niliweza kuwafahamu walionivamia kwa wengine kwa majina, wengine kwa sura.”Alisisitiza kusema Mmbando wakati akitoa ushahidi wake.

Aliongeza kuwa kuna mwanamke mmoja alimkoa konzi kichwani na wengine wakimgonga gonga huku na kule

Aliieleza mahakama watu wengine aliowatambua siku hiyo ya tukio kuwa ni Mbunge wa jimbo la Ubungo, Saed Kubenea akimwambia kuwa yeye ni Kibaraka wa CCM, hawawezi kuendesha serikali kama mali yao, akae aendeshe huo uchaguzi.

Mbunge wa jimbo la Ukonga, Mwita Waitara yeye alikuwa akimsisitiza kuwa hakuna kuondoka hapa kaa uendeshe kikao.

Akiendelea kutoa ushahidi mahakamani hapo, Mmbando alidai kuwa Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (56) yeye siku hiyo ya tukio alimuona akiwatuliza wenzake ‘muacheni tuweke utaratibu mzuri tutafanya tu kikao’.

Mheshimiwa Hakimu, walinikamata kwa nguvu nisitoke , wengine walinishika maziwa hadi sketi yangu iling’oka zipu na kwamba baada ya tukio hilo aliokolewa na askari wa jeshi la polisi na wafanyakazi wa jiji kupitia mlango wa nyuma na hakujua kilichoendelea nyuma yake.

“Katika tukio hili nilipata madhara, utu wangu nilidhalilika na mwili wangu ulivia damu”. Alimaliza kutoa ushahidi wake Mmbando.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: