Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro (pichani) amewataka maafisa watendaji wa mitaa,vitongoji,vijiji na kata kuwa chachu ya maendeleo kwa kushirikiana kikamilifu na madiwani wao ili kuwaletea maendeleo wananchi huku akiwataka kukataa miradi wasiyoielewa katika maeneo yao.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna.Kulia ni mwenyekiti wa mafunzo hayo Simon Mpaname.Wa kwanza kushoto ni Afisa Utumishi wa Manispaa ya Shinyanga Magadi Magezi akifuatiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini
Afisa Utumishi wa Manispaa ya Shinyanga Magadi Magezi akizungumza ukumbini
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi akisisitiza jambo ukumbini.

Matiro ameyazungumza hayo leo May 24,2017 wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya maafisa watendaji wa mitaa,vitongoji,vijiji,kata na maafisa tarafa katika manispaa ya Shinyanga yaliyolenga kuwajengea uwezo katika utendaji wao yaliyofanyika katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna katika manispaa hiyo.

Matiro aliwataka maafisa watendaji kuwa makini na miradi inayoanzishwa katika maeneo yao ili kuepuka kwenye lawama na migogoro inayoepukika na kukwamisha maendeleo katika jamii.

“Tunahitaji kuwa na ushirikianona kufanya kazi kwa umoja,nitasikitika sana kuona mradi unapelekwa kwenye kata yako lakini afisa mtendaji hauufahamu,ikitokea hivyo ukatae huo mradi kwani inapotokea mradi huo unaharibika atakayeulizwa ni wewe,kwa hiyo lazima ujue vyema mradi uliopo katika eneo lako ili kuepuka shida”,alieleza Matiro.

“Nilishawaambia hata wataalamu wa halmashauri zetu kuwa wanapokwenda kwenye kata au vijiji wawashirikishe maafisa watendaji kwa wao ndiyo wasimamizi wakuu wa miradi lakini mnaweza kusimamia miradi hiyo ikiwa mnaitambua na miradi ambayo hamuitambui ikataeni”,aliongeza Matiro.

Katika hatua nyingine alisema serikali haitasita kuchukua hatua kwa watendaji watakaoisababishia serikali hasara kupitia fedha mbalimbali zinazotolewa na serikali kwa ajili ya maendeleo.

Aidha Matiro aliwasisitiza maafisa watendaji hao kusimamia vyema suala la ukusanyaji wa mapato na kusimamia vyema suala la ulinzi na usalama katika maeneo yao.

Matiro alitumia fursa hiyo kuwakumbusha maafisa watendaji kutatua matatizo ya wananchi kwa kuhakikisha kuwa wanatenga siku maalum za kusikiliza kero za wananchi.

Naye Mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi aliwataka maafisa watendaji hao kusimamia vyema utaratibu wa kusoma mapato na matumizi kwa wakati.

Mwangulumbi pia aliwaagiza maafisa watendaji kutoa ushirikiano kwa maafisa ardhi wakati wa kupima ardhi,kutunza mali za ofisi na kukusanya mapato katika maeneo yote ya biashara.

Nao washiriki wa mafunzo hayo walisema yawasaidia kiutendaji kwani wamejifunza mambo mbalimbali ikiwemo wajibu wao,umuhimu wa kufuata taratibu za kazi,kusimamia miradi,uandishi sahihi wa vitabu na nyaraka za serikali, masuala ya ulinzi, rushwa na tahadhari ya majanga ya moto.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: