Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Rais wa Baraza la Taifa (High State Council) wa Libya Mhe. Abdulrahman Asswehly jijini Tripoli, Libya.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Libya Mhe. Fayaz Serraj jijini Tripoli, Libya.

Rais Mstaafu na Mjumbe Maalum wa AU katika Usuluhishi wa Mgogoro wa Libya jana tarehe 10 Mei amefanya ziara jijini Tripoli, Libya kuzungumza na wadau muhimu wa siasa wa Libya. Safari hiyo ni ya kwanza kuifanya nchini Libya tokea kuteuliwa kwake kuwa Msuluhishi wa mgogoro huo.

Akiwa jijini Tripoli, Rais Mstaafu na ujumbe wake kutoka Kamisheni ya Umoja wa Afrika amekutana na Waziri Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Libya Mhe. Fayez Serraj na Rais wa Baraza Kuu la Libya (High State Council) Mhe Abdulrahman Asswehly.

Katika mazungumzo yake na viongozi hao, Rais Mstaafu amewapongeza kwa hatua madhubuti walizochukua katika kuimarisha hali ya usalama jijini Tripoli ambapo theluthi moja ya wakazi wa Libya huishi humo. Amejionea na kufurahishwa kwa kurejea na hali ya usalama na shughuli za kijamii na kiuchumi.

Ameelezea dhamira ya Umoja wa Afrika kuendelea kusaidia pande zinazotofautiana ndani ya Libya kufikia makubaliano. Amesisitiza kuwa suluhisho la mgogoro wa Libya liko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe. Ameunga mkono dhamira njema ya pande zinazotofautiana kupitia upya baadhi ya vipengele vya Mkataba wa Makubaliano wa Siasa (Libya Political Agreement) kwa lengo la kuuimarisha.

Kwa upande wao, viongozi hao kwa nyakati tofauti wamemshukuru Rais Mstaafu kwa kufanya ziara Libya na wamepongeza kwa uamuzi wake huo. Wameichukulia ziara hiyo kuwa ni imani kubwa juu ya kuimarika kwa hali ya usalama nchini mwao. Wameelezea dhamira yao ya kuendeleza Mkataba wa Makubaliano uliopo na kutumia njia ya mazungumzo kumaliza tofauti zilizopo. Wameomba Umoja wa Afrika kuendelea kusaidia jitihada za amani na kuchangia uzoefu katika kusuluhisha mgogoro wao.

Rais Mstaafu anaendelea na ziara yake nchini Libya kwa kukutana na viongozi wa upande wa Mashariki mwa Libya.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: