Ndugu zangu,

Majuzi hapa ndugu yangu Ezekiel Kamwaga ameligusia. Nadhani hoja ya Kamwaga katika hili haijadadavuliwa inavyopaswa.

Nadhani tuna changamoto ya uelewa mpana na wa kina kwenye hili la wimbi la michezo ya kubahatisha lililoingia kwenye jamii yetu.

Michezo hii ya kubahatisha katika sura ya sasa, kwa baadhi ya vijana wetu na hata baadhi ya watu wazima, imekuwa ni ulevi kama ulevi wa madawa ya kulevya.

Walioingia kwenye ulevi huu wa kucheza michezo ya kubahatisha ambayo kimsingi ni kamari kuna waliogeulka mateja wa ' Ulevi wa kucheza kamari'.

Ndio, Casino sasa zimehamishiwa viganjani mwetu. Kwenye simu za Watanzania.
Unakutana na kijana leo anaomba elfu moja si kwa ajili ya chakula kama anavyodai, bali anataka kwenda kucheza kamari.

Kwenye kamari hizi wanaopoteza ni wengi na wenye kupata ni wachache sana. Kuhalalishia kamari hizi kwa kisingizio cha kuwawezesha kiuchumi Watanzania ni moja ya dhihaka kubwa kuwahi kufanyiwa Watanzania wanyonge walala hoi tangu kuondoka kwa Baba wa Taifa.

Kimsingi wanyonge wenye pato dogo wanashawishiwa kuwachangia na kuwatajirisha wachache. Faida hii ya wachache hairudi kwa wanyonge hawa.

Kuna wajanja wachache wenye kucheza na akili za wanyonge wengi wasio na maarifa. Wameshatambua, kuwa Watanzania wengi wanaishi katika ndoto. Wanapenda sana zawadi za ' Donge Nono!

Naam, ndoto kubwa ni kupata utajiri wa haraka, tena bila kuuvujia jasho. Hivyo, ukiwaletea chochote kile chenye kuamsha ndoto zao hizo, basi, wewe taja tu mia tano kwa milioni tano.

Wape namba za kutuma kwa meseji, kaa na gunia lako, utazivuna mia tano mia tano ukapata mamilioni. Kisha unawafanyia kiini macho kwa kuwachagua wawili watatu miongoni mwao na kuwapa zawadi ya 'Donge Nono' la milioni tano. Wataongezeka.

Babu wa Loliondo alikuja na akavuna mia tano mia tano za kikombe chake. Mamilioni walikwenda Samunge. Kama huduma ya Babu ingekuwa inalipiwa kwa meseji kwa kusikiliza neno lake la tiba alilorekodi, basi, Babu wa Loliondo leo angekuwa bilionea

Nimechokoza mjadala...

Maggid.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: