Thursday, June 1, 2017

MKUU WA MKOA NJOMBE ATEMBELEA MIRADI YA ELIMU NA AFYA HALMASHAURI YA MJI NJOMBE

 Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Christopher Ole Sendeka akiweka jiwe la msingi kwenye  nyumba za waalimu shule ya sekondari ya wasichana Anne Makinda. Nyumba zenye uwezo wa kuishi waalimu 6 katika nyumba moja "6 in 1"
 Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akikagua uimara wa milango kwenye moja ya madarasa katika shule ya sekondari ya wasichana Anne Makinda.Nyuma yake ni Mh. Mkuu wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe  akikata utepe kuashiria uzinduzi wa shule ya Msingi Mpeto
 Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akisisitiza jambo kwa Wananchi (hawapo pichani)  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Luponde mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la OPD  kituo cha afya Luponde wa kwanza kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga.
 Wananchi wa Kijiji cha Luponde wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa katika mkutano wa hadhara.
 Mkuu wa Mkoa wa Njombe akiwa katika Picha ya pamoja na uongozi wa wanafunzi shule ya sekondari ya wasichana Anne Makinda, Shule hiyo ya Kata ilifanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana na kushika nafasi ya Tano Kimkoa na Nafasi ya Kwanza Kiwilaya.

Na Hyasinta Kissima-Njombe

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe Christopher Ole Sendeka leo amehitimisha ziara yake ya siku mbili katika Halmashauri ya Mji Njombe ambapo alipata nafasi ya kutembelea miradi ya elimu na afya.

Miradi ya elimu iliyotembelewa ni katika Shule ya Sekondari Anne Makinda ambapo Sendeka alikagua Ujenzi wa Vyumba vitatu vya madarasa, Matundu nane ya vyoo na kuweka jiwe la msingi katika nyumba za waalimu zenye uwezo wa kuishi waalimu sita kwa wakati mmoja “6 in 1” ambapo ujenzi wa miundombinu hiyo umegharimu kiasi cha shilingi Milioni Mia Mbili na arobaini na Moja (241,000,000)/ kupitia mpango wa pili wa maendeleo elimu ya Sekondari (MMES II).

Aidha katika Sekta ya Elimu Mkuu huyo wa Mkoa alifanya uzinduzi wa shule ya Msingi Mpeto, shule iliyojengwa kutokana na shida iliyokuwepo ya watoto kutembea umbali wa KM 05 kwenda shule ya Msingi Kibena, shule iliyojengwa na Wananchi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji Njombe, na wadau wa maendeleo kikiwepo kiwanda cha Chai cha Kibena na TANWAT mradi iliogharimu kiasi cha shilingi milioni mia moja kumi na saba na laki nne (117,400,000) na kujengwa na mafundi waliojitolea kufanya kazi bila malipo na kuokoa kiasi cha shilingi milioni sabini na saba.

Kwa upande wa Sekta ya Afya Mkuu wa Mkoa wa Njombe aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa jengo la OPD katika kituo cha afya Luponde ambapo Halmashauri iliweza kuchangia bati 210 huku wananchi na wadau wa maendeleo wakichangia milioni thelasini (30,000,000/=)

Katika ziara yake Ole Sendeka, alipata nafasi ya kuzungumza na Wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Luponde na kusisitiza maswala ya ulinzi na usalama, uchangiaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha wazazi wanawapeleka watoto wao shuleni hususani watoto wa kike na kuhakikisha michango ya chakula inawasilishwa shuleni ili watoto waweze kupata chakula cha mchana shuleni na kuendelea na masomo vizuri.

Kwa wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa yeye na kamati yake ya ulinzi na usalama itahakikisha kuwa inadhibiti mauaji ya binadamu yanayotokea kwa kusababishwa na imani za kishirikina, wivu wa kimapenzi na wale wote wanaofanya matendo ya ubakaji kwa watoto wadogo amewasisitiza kuacha tabia hizo mara moja kabla ya kuingia mikononi mwake na kwenye vyombo vya sheria.

“Wale wote wanaofanya matendo maovu kama ya ubakaji, mauaji naomba kamati ya ulinzi na usalama ipate taarifa zao mara moja. Ikiwezekana nileteeni mimi Ofisinimajina ya hao watu yeyote yule atayehusika tutamkamata na kumburuza mahakamani asubuhi na mapema hatuwezi kuwa na watu wanaofanya mambo ya kiovu katika Mkoa wetu. Pale mnapoona mtu msiyemfahamu kijijini toeni taarifa msikae kimya na kuficha waovu.”Alisema

Akihitimisha ziara yake ya siku mbili katika Halmashauri ya Mji Njombe, Ole Sendeka ameipongeza Halmashuri kwa kuwa na miradi mizuri ambayo thamani ya fedha inaonekana na amewasisitiza wananchi kushirikiana na serikali iliyopo madarakani kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuwaonya wananchi kuacha kubeza viongozi wanaohamasisha uchangiaji wa shughuli za maendeleo katika Mkoa wa Njombe na amewataka viongozi wa vijiji na mitaa kuhakikisha wanasoma taarifa za mapato na matumizi na zinawekwa wazi ikiwa ni pamoja na kubandikwa kwenye mbao za matangazo ili wananchi wanaoshiriki katika kuchangia maendeleo wapate kujua ni kwa jinsi gani fedha zao zinavyotumika katika kufanikisha maendeleo kwenye eneo husika.

No comments :

Truck Driving Schools
Idadi ya Watu