Meya mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni Yusufu Mwenda amewataka viongozi wa Chama na Serikali waliopo madarakani kumuunga mkono Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika harakati zake za kimaendeleo anazozifanya.

Akizungumza mara baada ya futari aliyoiandaa kwa waumini wa dini ya Kiislam nyumbani kwake Jijini Dar es salaam jana, Mwenda alisema viongozi hawana budi kuendana na dhamira aliyonayo Rais hususani kipindi hiki anapofanya mambo mbalimbali
 Alisema uongozi uliopita kabla ya magufuli ambao wao walikuwa madarakani ulikuwa na vipaumbele vyake ilivyokuwa ikivitekeleza na vivyo hivyo kwa Serikali ya sasa,jambo alilosisitiza kuwa ni vyema wananchi pia wakaunga mkono.

"Huu ni muda Magufuli, ana kipindi cha uongozi wa miaka mitano aliyopo sasa, na akimaliza hapo ataendelea na kipindi cha miaka mitano mingine...hatuna budi kumuunga mkono ili atimizie yale yote mazuri aliyokusudia kulifanyia Taifa hili" alisema Mwenda.

Aidha alisema viongozi waliopo madarakani kwa pamoja wanapaswa kushirikiana kwa namna mbalimbali ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana na kusisitiza kuwa pasipo ushirikiano huo hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.
 Awali Meya wa sasa waManispaa hiyo Benjamini Sitta, mbali na kusifu juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli, alimpongeza Meya Mwenda kutokana na namna alivyoiongoza Kinondoni enzi za utawala wake.

Alisema mfano wa uongozi uliyoonyeshwa na kiongozi huyo katika Manispaa hiyo wakati wa uongozi wake, ulimvutia kila mtu huku akiahidi kufuata nyendo zake ilikuiletea manispaa hiyo maendeleo.

" Ukiacha sifa zingine nyingi ulizoziacha pale ofisini, pia niliambiwa kipindi kama hiki cha mwezi mtukufu wa ramadhani ulikuwa na utaratibu wa kuwakutanisha watu mbalimbali na kuwafuturisha...nami naahidi kufuata utaratibu huo kwa kuwa ni jambo jema" alisema Sitta.
Aidha alisema wakati uliopo sasa unampasa kila kijana kufanya kazi kwa lengo la kujiletea maendeleo yeye binafsi pamoja na Taifa lake kwa ujumla.

Mbali na viongozi hao, dhifa hiyo pia iliudhuriwa na wananchi mbalimbali wa mtaa anaoishi meya huyo pamoja na viongozi wa dini ya Kiislam kutoka Makao Makuu ya Baraza la Kiislam Tanzania (BAKWATA) wakimuwakilisha Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakary Zuberi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: