Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville (kushoto).
Askofu Blaston Gaville wakati akiwekwa wakfu kuongoza Dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

KUKAMILIKA kwa mchakato wa uaandaaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutasaidia kuweka misingi imara na kuondoa changamoto zilizopo katika Katiba ya sasa, hivyo kukomesha ufisadi na kuinua uchumi wa Tanzania.

Aidha, kukamilika huko kwa Katiba Mpya kutaakisi jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville, ambaye alimtaka Rais Magufuli kuumalizia mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya, kwani alisema mbali ya kuakisi kasi yake anayoifanya ya kukuza uchumi pia kutasaidia kuhimiza uwajibikaji.


“Wakristo na Watanzania kwa ujumla tuna imani kubwa na Serikali ya Awamu ya Tano na ni matarajio yetu kwamba mchakato wa kuandika Katiba utamalizwa kama lengo lilivyokuwa,” alisema.

Askofu Gaville amesimikwa ili kuchukua nafasi ya Askofu Dkt. Owdenburg Mdegella ambaye amestaafu.

Alisema wanatiwa moyo na jitihada zinazoendelea kufanywa na Dkt. Magufuli katika kufufua uchumi na kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya Watanzania wote.

Alisema Tanzania ina wanyonge wengi kuliko wenye nguvu, hivyo wanatiwa moyo na jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli na serikali yake hasa anapowatetea wanyonge.

Aidha, pamoja na kupongeza jitihada hizo, Askofu Gaville, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa kodi akisema
hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo bila mapato hayo.

“Tunaiomba serikali iangalie upya suala la kodi kwa mashirika ya dini kwani baadhi ya kodi tunazolipa, ikiwemo ya kuendeleza vyuo vya ufundi na ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, zimekuwa mzigo mkubwa kwaetu.

“Kazi ya Kanisa ni kutoa huduma, siyo kutengeneza faida, kodi hizo zimeleta changamoto kubwa kwa uendeshaji wa taasisi, tunaomba serikali iziangalie upya,” alisema.

Kuhusu elimu, Askofu Gaville alisema Kanisa linasaidia watoto maskini ili wapate haki yao ya elimu na akaiomba serikali isiwaingize katika kundi la watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo kwa sababu wanasoma shule binafsi.

“Wanapojiunga na vyuo vikuu, tunaomba Bodi ya Mikopo isiwanyime mikopo stahiki kwa kisingizio cha shule wanazotoka, ufanyike upembuzi ili kutoa msaada kwa walengwa wote,” alisema.

Aidha, alisema Dayosisi ya Iringa inatoa mwaliko kwa vyama vyote vya kisiasa na jamii nzima ya Watanzania kuendeleza na kukuza tunu ya ushirikiano na moyo wa kizalendo ili kuwa na maendeleo yenye tija, badala ya kujenga uhasama kwa sababu za kiitikadi.

Katika salamu zake kwa waumini wa dayosisi hiyo, Askofu Mkuu wa KKKT Tanzania, Dkt. Fredrick Shoo, alizipongeza kamati mbili za madini zilizoundwa na Rais Magufuli akisema zimewaumbua baadhi ya Watanzania waliodhani ni sifa kusaini mikataba ya madini inayonyonya haki ya Watanzania.

“Kama hao watu waliosaini hiyo mikataba walidhani wanaisadia nchi huku wakijua mikataba hiyo inalenga kuiibia nchi, wajue hayo ni mambo ya aibu na ni upumbavu mkubwa kufanya mambo kama hayo kwa ajili ya matumbo yao binafsi,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William, akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, alisema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zote za dini ili kufikia malengo yake ya maendeleo.

William alizungumzia fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo mkoani Iringa na akawaomba Watanzania na wawekezaji kuzitumia ipasavyo kuunga
mkono jitihada za Rais za kuifanya nchi kuwa ya viwanda.

Katika hatua nyingine, Askofu Mstaafu wa Dayosisi hiyo, Dkt. Owdenburg Mdegela, aliipongeza serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa hatua
mbalimbali inazochukua kujirekebisha.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: