Ili kupunguza uhalifu katika Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam imebainika kuwa ni vyema kuwatambua wananchi wote na mahali wanapoishi ikiwemo kubaini wageni wote wanaowasili katika Manispaa ya Ubungo ikiwa ni pamoja na mahali wanapofikia.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Kibamba Chama Jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi Kayombo amesema kuwa kumekuwa na uhalifu kwa kiasi kikubwa katika maeneo mbalimbali Katika Manispaa hiyo jambo ambalo limetafutiwa muarobaini kwa kuanzishwa daftari la wakazi litakalobainisha wakazi wote ili kukitokea uhalifu iwe rahisi kuwabaini wahalifu hao.

Kuanzishwa kwa Daftari la Rejesta ya Wakazi wa Mtaa ni agizo lililotolewa hivi karibuni na MKUU wa Wilaya ya Temeke Mhe Felix Lyaviva kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa za Kigamboni, Ilala, Temeke, Kinondoni na Ubungo wakati akihutubia kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda katika ufunguzi wa semina ya mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ili kuwaelimisha watumiaji wa Intaneti wapatao milioni 20 sambamba na watumiaji wa simu za mikononi wapatao milioni 40 kuwa na matumizi bora ya simu za mikononi na mitandao ya kijamii.

Mkurugenzi wa manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amesema kuwa pamoja na kuanzishwa kwa Daftari la Rejesta ya wakazi wa Mtaa pia kutakuwa na Fomu ya Rufaa ya Malalamiko katika kila Mtaa sambamba na kitabu cha kutunza kumbukumbu za kusikiliza malalamiko ya wananchi katika Ofisi za serikali.

Tayari vitabu hivyo vyote vimeanza kugawanywa katika kila Mtaa ili kuanza utekelezaji wa zoezi hilo haraka iwezekanavyo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: