Mmoja wa Wananchi akiweka saini ya kielektroniki katika zoezi la usajili wa Vitambulisho vya Taifa linaloendela katika Banda la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa – NIDA ndani ya Viwanja Maonyesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA)
Afisa usajili Mamalaka ya Vitambulisho vya Taifa - NIDA Ndg. Daniel Katondo akitoa maelekezo ya namna ya kujaza fomu kwa mmoja wa Wananchi waliojitokeza katika zoezi la usajili ndani ya Banda la NIDA katika Maonyesho ya 41 ya kibiashara maarufu kama sabasaba.
Wananchi wakipatiwa huduma mbalimbali Ndani ya Banda la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa – NIDA ikiwemo Elimu kuhusu umuhimu wa kitambulisho cha Taifa. Pichani Afisa Uhamiaji Bw. Jamal Kaoneka akimhakiki mmoja wa Wananchi wakati wa kukamilisha Tararibu za Usajili.
Huduma za Usajili zikiendelea kutolewa kwenye Banda la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi waishio Mkoa wa Dar-es-Salaam, pamoja na kupatiwa taarifa za hatua za Maombi ya Vitambulisho yalipofikia kwa wale waliokwisha kujisajili.
Mmoja wa Wananchi waliojitokeza katika Banda la Mamlaka ya Vitambulihso akipatiwa maelezo mbalimbali hukusu Usajili wa Vitambulisho vya Taifa pamoja na Elimu juu ya umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa pamoja na Matumizi yake.
---
Wananchi kutoka viunga mbalimbali vya Mkoa wa Dar-es-salaam wameendelea kumiminika katika Banda la Maonyesho la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) lililopo kwenye hema la Jakaya Mrisho Kikwete kuchangamkia Ofa ya Kusajiliwa na kupata Vitambulisho vya Taifa, ndani ya siku za Maonyesho hayo yanayoendelea katika Viwanja ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mbali na kusajiliwa; baadhi wamejitokeza kupata taarifa za Usajili waliofanya siku za nyuma na kujifunza zaidi kuhusu matumizi na faida za Vitambulisho vya Taifa ambavyo vimeanza kutumika katika huduma mbalimbali nchini zinazotolewa na baadhi ya Taasisi na Mashirika ya Serikali yakiwemo makampuni ya Simu.

Akizungumza kupitia vyombo mbalimbali vya Habari leo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (NIDA), Bi. Rose J. Mdami amewataka wananchi kutumia vizuri fursa hii hususani wananchi na wakazi wa mkoa wa Dar-es-salaam ambao hawajasajiliwa Vitambulisho vya Taifa; kwani kwa kipindi hiki cha Sabasaba wametoa kipaumbele kwa wananchi hao ili kupanua wigo wa matumizi mapana ya Vitambulisho hivyo kielektroniki.

“Nasisitiza wananchi wa Dar-es-salaam ambao hawajasajiliwa; wajitokeze wakiwa na viambatisho muhimu vya kuwatambulisha mathalani Cheti cha Kuzaliwa, Vyeti vya Shule, Pasi ya Kusafiria(Passport), Kadi ya Kupigia Kura, TIN namba, Kadi ya Bima ya Afya, Kitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Leseni ya Udereva na Kadi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii. Kuwa na Viambatisho vingi zaidi ni kutambulika kwa haraka zaidi” Alisitiza

Kwa mujibu wa Bi. Rose Kitambulisho hicho ni bure; na huduma hii ya kupata Kitambulisho ndani ya siku za maonyesho ni kwa siku saba tu za mwanzo yaani hadi tarehe 07/07/2017, baada ya hapo utaratibu wa kawaida wa kuwasajili wananchi utaendelea. Wananchi pia wameshauriwa kuanza taratibu za kujaza fomu za maombo ya Usajili kwenye Serikali za Mitaa wanakoishi na kugonga mhuri kabla ya kufika kwenye Banda la NIDA ili kurahisisha zoezi.

NIDA inashiriki kwa mara ya pili maonyesho ya Kimataifa ya Sabasaba ikiwa imekusudia kuwaelimisha wananchi namna gani Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu ni ngazi katika kufikia malengo mapana ya Serikali ya Ukuzaji Biashara na Maendeleo ya Viwanda kama Kauli mbiu ya Maonyesho hayo inavyosema “Ukuzaji wa Biashara kwa Maendeleo ya Viwanda” .
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: