Selemani Jaffo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) akisikiliza maelezo kutoka kwa mama Abia Magembe kuhusu bidhaa zinazotokana na zao la muhogo. Kushoto kabisa ni Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia Cebada na kulia ni Mratibu wa mradi huo nchini Tanzania, Secelela Balisidya.

NAIBU Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo, amesema halmashauri zinawajibu wa kuunga mkono jitihada za utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Kutokana na hali hiyo, ameonya mtu yeyote asikwamishe jitihada zinazofanywa na akinamama washiriki wa mradi wa Green Voices Tanzania huku akiahidi kuwa serikali iko nao bega kwa bega.

Alisema kwamba, endapo kuna mtu katika idara zilizo chini ya wizara yake atakwamisha jitihada zao, basi akinamama hao wawasiliane naye moja
kwa moja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa Green Voices nchini Tanzania uliofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Jaffo alisema kwamba, wizara yake ndiyo yenye jukumu kubwa la kuwawekea mazingira mazuri akinamama hao kutekeleza miradi yao chini ya halmashauri husika, hivyo akawaahidi kuwapatia ushirikiano wa kutosha kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na suala la mazingira linapewa kipaumbele.

Mradi wa Green Voices unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro, kukiwa na miradi 10 ikiwemo ya kilimo cha mihogo, kilimo cha matunda, uyoga, ufugaji wa nyuki, ukaushaji wa mbogamboga na utengenezaji wa majiko rafiki wa mazingira.
Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia Cedaba (kushoto) akiwa na Leocadia Vedasto kutoka Ukerewe anayeratibu kilimo cha viazi lishe pamoja na usindikaji wa bidhaa zake. Katikati ni mdau mwingine aliyehudhuria uzinduzi wa awamu ya pili ya Mradi wa Green Voices Tanzania.
Bidhaa za mbogamboga zilizokaushwa kutoka Morogoro.


Akinamama walioanzisha miradi hiyo – miradi na mikoa watokayo vikiwa kwenye mabano –ni Regina Kamuli (Mkuranga, Pwani – Majiko Banifu), Abiah Magembe (Kisarawe, Pwani – Usindikaji
wa Muhogo na Mtama), Magdalena Bukuku (Kinondoni, Dar es Salaam – Kilimo cha Uyoga), Mariam Bigambo (Dakawa, Morogoro – Ufugaji wa Nyuki), na Esther Muffui (Morogoro – Ukaushaji wa Mboga na Matunda).


Wengine ni Farida Makame (Kilimanjaro – Majiko ya Umeme-Jua), Leocadia Vedastus (Ukerewe, Mwanza – Kilimo na Usindikaji wa Viazi Lishe), Monica Kagya (Kisarawe, Pwani – Ufugaji wa Nyuki), Dkt. Sophia Mlote (Kinyerezi, Dar es Salaam – Kilimo Hai cha Nyanya na Mbogamboga), na Evelyn Kahembe (Uvinza, Kigoma – Kilimo cha Matunda).

Kupitia miradi hiyo, zaidi ya wanawake 300 wamepatiwa mafunzo mbalimbali huku program nyingine za mafunzo kwa vitendo zikiendelea katika makundi yao.

“Serikali ya Tanzania na hasa wizara hii, na wizara hii Mheshimiwa Rais mwenyewe ni wizara yake, naomba niwahakikishie kwamba tutashirikiana na Green Voices kwa nguvu zote na nitawapa pasiwedi ya kuwasiliana na ofisi yangu moja kwa moja ili kama mnakwama mambo yenu yaweze kwenda huko katika halmashauri mlipo,” alisema Jaffo, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jaffo, akizungumza katika uzinduzi huo.
Secelela Balisidya akipokea cheti.

Mmoja wa washiriki wa mradi wa Green Voices, Mariam Bigambo, mkulima wa Mvomero ambaye amejikita katika ufugaji wa nyuki akiwa na kikundi cha wanawake 15, alisema kwamba licha ya umuhimu wa mradi huo, lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinakwamisha maendeleo yao.

“Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni kushushwa kwa mizinga yetu na watu wasiojulikana kwa sababu tumeiweka porini,” alisema na kuongeza: “Kila mara tunakuta mizinga yetu imeshushwa, tumekwishatoa taarifa kwa serikali ya kijiji pamoja na kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na hata Polisi.”

Aidha, alisema kwamba, ufugaji wa nyuki unahitaji uvumilivu
na mpaka sasa baadhi ya wanakikundi wamevunjika moyo kwa sababu bado
hawajanufaika na matunda ya kazi yao.

Kutokana na hali hiyo, alisema, wameamua pia kugeukia kilimo cha uyoga ili kuongeza tija.

Mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya, alisema awamu ya kwanza ya mradi huo ililenga katika uanzishwaji na uzalishaji, lakini awamu ya pili inalenga kuwapatia stadi akinamama ili kuboresha bidhaa wanazozizalisha ili ziongezeke ubora la kuwaletea tija.

“Hivi sasa katika awamu ya pili akinamama watapatiwa mafunzo ya namna ya kutengeneza bidhaa zao kama vifungashio ili kuongeza ubora na thamani na tunataka bidhaa zao ziingie sokoni katika viwango ambavyo vinakubalika,” alisisitiza.

Akizungumza katika uzinduzi huo wa awamu ya pili, Mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka Hispania kutoka taasisi ya Women for Africa Foundation inayodhamini mradi huo, Alicia Cebada, alisema wamefarijika na mradi huo kwa kuwa umeonyesha mafanikio makubwa nchini Tanzania katika awamu ya kwanza na ndiyo maana wameamua kuwaongezea uwezo akinamama hao
katika awamu hii.

“Tumekuwa tukiwasiliana mara kwa mara na Secelela (Mratibu wa Green Voices Tanzania) kuhusu mafanikio na changamoto za mradi huu na kwa kweli tunafarijika kuona miradi yote inakwenda vizuri,” alisema Alicia.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: