Anaandika Bernard Mukasa

Jana mitandao ya kijamii nchini ilienea habari za kanisa kutokumzika tajiri mmoja kwa sababu alikufa katika hali ya "kinyumba" bila ndoa takatifu, na kwamba hakuwa mshiriki hai wa masuala ya kanisa.

Baada ya hapo kukatokea maneno mengi sana baadhi ya watu wakilishanbulia kanisa katoliki kwamba limekosea na linakosea kwa utaratibu huo, kwa maelezo mepesi kwamba suala la mtu kwenda mbinguni ni wajibu wa Mungu na siyo kazi ya kanisa kuhukumu (huenda wamesahau kwamba kanisa halijaihukumu roho ya marehemu bali limekataa kuuzika mwili wake tu ardhini).

Basi nimewiwa kufafanua kidogo niwezavyo kuhusu suala hili.

Karibu.......

Maziko ya kikanisa hayamfanyi mmoja aliyefariki aende mbinguni wala Jehanamu, bali yanamkumbusha mwombolezaji aliyebaki hai wajibu wake wa kuishi katika ushirika na kanisa ambalo ni mwili wa Kristo.

Kumzika au kutokumzika mtu kikanisa siyo jambo la kubeza ingawa ni kweli siyo linalompeleka marehemu mbinguni au motoni. Tukumbuke mwili wa marehemu unabaki ardhini. Kinachoenda mbinguni au motoni ni roho.

Lakini maziko ya kikanisa ni jambo lenye maana kubwa kutukumbusha tunaobaki duniani kwamba Kanisa ambalo ni mwili wa Kristo na ambalo Kristo mwenyewe ndiye kichwa chake (Waefeso 5:23) linataka waamini tuige mfano wa mwenzetu aliyeishi na kumaliza maisha yake akiwa na ushirika na kanisa, ndiyo maana linafanya maziko ya kikanisa kama sherehe ya kumpongeza, kumuaga na kutuonesha mfano wake ili tuufuate. Na kama ameishi na kumaliza maisha yake bila shirika kamili na Kristo kwa njia ya kanisa ambalo ni mwili wa huyo Kristo, kanisa linakataa kumzika ili kutuambia kwamba mfano wake siyo ufaao kuigwa.

Kwa nini ni muhimu Mkristo ashiriki maisha ya kanisa badala ya kuishi kivyakevyake tu?

Kwa sababu Kristo alitaka hivyo. Wakati anawaaga mitume wake na wanafunzi wake aliwataka WABAKI KATIKA UMOJA, NA WAKAE HIVYO HATA ROHO MTAKATIFU MZINDUZI RASMI WA KANISA AKIJA AWAKUTE WAKIWA PAMOJA NA WAMOJA.

Tutakumbuka hata sala ya Mwisho ya Bwana wetu Yesu Kristo kabla hajatiwa mikononi mwa wauaji aliwaombea wanafunzi wake WABAKI WAMOJA kama yeye na Baba walivyo MMOJA (Yohane 17:11).

Hivyo maisha ya ukristo ya kivyakovyako kwa kujitenga na kanisa Siyo mpango wa Kristo bali mpango wako binafsi. Siyo mfano tunaopaswa kuuiga wala kuuendekeza.

Kungia mbinguni kuurithi uzima wa milele kunamdai mtu atimize masharti makuu mawili (Luka 10:25-28):

1. Mapendo kwa Mungu
2. Mapendo kwa jirani.

Lakini huwezi kumpenda Mungu nusunusu. Yaani ukampenda kichwa na ukamchukia mwili. Kama kanisa ni mwili wa Kristo, wawezaje kusema unampenda Yesu (Mungu nafsi ya pili) na bado huna muda na mwili wake yaani kanisa lake? Mnafiki wewe.....!

Na kama hukumpenda Mungu (kichwa na mwili) na hukumpenda jirani, utawezaje kuurithi uzima wa milele? Ni vigumu.

Ni vema kujitahidi kuiepuka njia hiyo, ndiyo maana kanisa linautumia msiba kutukumbusha njia njema na kutuonya juu ya njia isiyo njema.

Kumbuka Yesu alisema atakayemkiri yeye Yesu (ambaye kanisa ni mwili wake) mbele za watu, Yesu pia atamkiri mbele ya baba, na atakayemkana Yesu mbele za watu Yesu pia atamkana yeye mbele ya Baba yake wa Mbinguni atakapofika mbele ya kiti cha utukufu wa Mungu (Mathayo 10:32-33).


Mfano wa taratibu za ki-kanisa ambazo ukijitenga nazo siyo rahisi kuupata uzima wa milele ni huu:

Ukiuishi ukristo wako peke yako nyumbani mwako huna nafasi ya kushiriki EKARISTI TAKATIFU au kwa maneno mengine KOMUNYO au wengine wanaita CHAKULA CHA BWANA au wengine wanaita MKATE WA BWANA.

Lakini Yesu mwenyewe alisema:

"Kweli nawaambieni, Msipokula huu mwili wangu na kuinywa damu yangu, hamtakuwa na uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho"

Yohane 6:53-54

Zingatia vizuri hayo maneno ya mwanzo niliyoya-bold. Yesu anaanza kwa kusisitiza akisema "Kweli nawaambieni,..

Kwa nini Yesu alisisitiza?

Kwa sababu alijua kuna wengi watapuuzia suala la kukomunika (kushiriki chakula cha Bwana) wakidhani watakuwa na uzima wa milele kwa kuishi tu majumbani kwao bila kuja kanisani ambako ndiko chakula hicho hutolewa, wakijidanganya kwamba maadam waliishabatizwa (na wengine walibatizwa kwa maji mengi ya mto wote au bahari nzima) basi hiyo inatosha kwa wao kuurithi uzima wa milele.

Pia alijua wapo ambao wanaweza kuwa wanasali na kutoa sadaka kubwakubwa lakini wanaishi maisha yanayowafanya wasistahili kushiriki chakula cha Bwana, wakidhani ni rahisi kuupata uzima wa milele bila chakula hicho.

By the way..., hatuokolewi kwa matendo yetu. Tunaokolewa kwa neema (Waefeso 5:2).

Neema ya Mungu (yaani uwepo wa Yesu Kristo katika maisha na mazingira ya mwanadamu) haipatikani katika kujitenga wewe binafsi, bali inapatikana kwa kuungana na wenzako kwa jina la Yesu.

Yeye mwenyewe alisema:

"Wakutanikapo wawili watatu kwa jina langu, mimi nipo hapo kati yao"

Mathayo. 18:20.

Na kama Yesu yupo katikati ya walio na umoja/ushirika katika yeye, basi neema ya Mungu inapatikana katika ushirika huo na siyo katika ubinafsi na kujitenga. Na kwa kuwa tunaokolewa kwa neema, ni rahisi zaidi kuokolewa tukiwa ndani ya kanisa kuliko kuokolewa tukiwa tumejitenga na mambo ya kanisa.

Kwa hiyo ndugu yangu..., ni muhimu sana kushiriki mambo ya kanisa. Na ni muhimu sana kwa kanisa kuonesha shukrani nanpongezi (appreciation) kwa yule anayekufa katika ushirika na kanisa, na kuonesha kuhuzunishwa na yule anayekufa akiwa hana shirika na kanisa.

Neno la Mungu linasema "Heri watu ambao wanakufa wakiwa wameungana na Bwana. Naam, watapumzika kutoka katika taabu zao, maana matunda ya jasho lao yatawafuata" (Ufunuo 14:13).

Mstari huo wa mwisho kunukuu ni muhimu sana kwako ndugu yangu. Kwamba ukifa umetengana na Bwana kwa matendo yoyote ikiwemo kutengana na mwili wa Bwana Yesu (Kanisa lake) una ole. Na ukifa ukiwa umeungana naye kwa matendo yoyote ikiwemo kuungana na mwili wa Bwama Yesu (Kanisa lake) una heri. Na amemalizia kwa kusema "matendo yako yataambatana nawe" hata baada ya kufa. Ndiyo maana umekufa, lakini sifa za jitihada za jasho lako tunazihubiri hata wakati wa mazishi yako. Na kinyume chake, sifa mbaya ulizoacha tunazikana hata baada ya kufa kwako kwa kuyakana mazishi yako.

Tumsifu Yesu Kristo.

Ben Mukasa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: