WAZIRI wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama akiwa anamsikiliza Balozi wa Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro Mrisho Mpoto mara baada ya kuwasili katika banda hilo hivi karibuni jijini Arusha katika maadhimisho ya sikukuu ya nane nane.
Ofisa Utalii wa Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro Peter Makutian aliwashukuru watanzania kuendelea kuhamasika kutembelea hifadhi hiyo tofauti na awali na kusema kuwa idadi ya wageni toka nje ya nchi wanaotembelea hifadhi hiyo kwasasa ipo sawa na watanzania.

Na Pamela Mollel, Arusha.

WAZIRI wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama  amezitaka hifadhi za taifa nchini kuendelea kuwatumia wasanii nchini  katika kutangaza vivutio mbalimbali vinavyopatikana huku akiipongeza  Mamlaka ya hifadhi za taifa Ngorongoro inavyotangaza vivutio vyake  kupitia msanii Mrisho Mpoto.

Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni jijini Arusha alipotembelea banda la Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro katika maonesho ya Nanenane.

Alisema kuwa wasanii wananafasi kubwa ya kuutangaza utalii wa ndani na  kuendelea kuitangaza Tanzania endapo watatumiwa kama mabalozi kupitia  umaarufu wao jambo ambalo litasaidia pia kuiingizia nchi kipato kupitia  watalii.

Naye Balozi wa Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro Mrisho Mpoto aliwapongeza  watanzania kuwa na mwitikio mkubwa wa kutembelea hifadhi hiyo ikiwa ni  pamoja na kuwapeleka watoto wao katika maonesho hayo ili kujifunza na  kuona shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo hivyo kuwaandaa watoto hao  kuwa wahifadhi kwa baadae.

"Mfano mzuri ni hili la punguzo la shilingi elfu 50 lililotolewa ili  watanzania waweze kutembelea hifadhi ya Ngorongoro tumeona watu  walivyochangamkia na kwenda kutembelea Ngorongoro hivyo ni jambo zuri  na la kupongezwa kwa watanzania na ninaomba waendelee kutembelea  hifadhi zetu"alisema Mpoto.

Kwa upande wake Ofisa Utalii wa Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro Peter  Makutian aliwashukuru watanzania kuendelea kuhamasika kutembelea hifadhi hiyo tofauti na awali na kusema kuwa idadi ya wageni toka nje ya nchi  wanaotembelea hifadhi hiyo kwasasa ipo sawa na watanzania.

Aidha aliwaomba watanzania wengine kuendelea kutembelea vivutio vya Tanzania  ikiwemo Ngorongoro kwakuwa gharama wanazotoza ni ndogo kwao
ukilinganisha na wageni toka nje ya nchi hivyo ni fursa nzuri kwao
kuitumia na kuwa mabalozi wa hifadhi kwa wengine.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: