Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe Jumanne Septemba 5 anatarajiwa kuongoza waombolezaji katika mazishi ya Mwandishi wa habari mkongwe nchini, Muhingo Rweyemamu.

Taarifa iliyotolewa jana na kamati ya mazishi, imeeleza kuwa ibada ya mazishi ya Muhingo ambaye alifariki dunia Jumapili kwenye Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, itafanyika kwenye Viwanja vya Mnazi mmoja, Dar es Salaam.

Mbali ya Dk. Mwakyembe, wengine wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi ya Muhingo ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa wilaya za Handeni, Makete na Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wabunge na viongozi wa vyama siasa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kabla ya kufikishwa Mnazi Mmoja, mwili wa marehemu Muhingo utaagwa mapema katika kanisa la KKKT Mbezi, kisha utapelekwa kwenye viwanja hivyo, ambako pia risala mbalimbali zitatolewa kuanzia saa 5 asubuhi.

Mara baada ya kuagwa uwanjani hapo, waombolezaji wataelekea kwenye makaburi ya Kinondoni kwa ajili ya mazishi.

Katika uhai wake, marehemu Muhingo aliwahi kuwa mwalimu kabla ya kusomea na kuanza kazi ya uandishi wa habari ambako alitumikia vyombo kadhaa vikiwamo magazeti ya Mtanzania na Mwananchi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: