Shehena ya Rwanda kupitia bandari ya Dar es Salaam katika kipindi cha miaka mitano imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 9.9 kwa mwaka kutoka tani 630,000 mwaka 2012/2013 mpaka tani 950,000 mwaka 2016/2017. 

Haya yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko alipokutana na balozi wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Eugene Kayihura aliyetembelea TPA leo.

Kakoko amesema kwamba kwa sasa shehena yote ya mizigo inayokwenda na kutoka Rwanda na nchi zingine za jirani inahudumiwa ndani ya bandari ili kurahisisha uondoshaji na usalama wa mizigo hiyo.

Mkurugenzi Mkuu amesema katika mkakati wake wa kuimarisha uhusiano zaidi na wateja, Serikali kupitia TPA imetenga eneo kwa ajili ya kuhifadhia mzigo wa Rwanda katika bandari Kavu ya Kwala, Ruvu na kuwataka wafanyabiashara wa nchini Rwanda kuitumia bandari Kavu ya Isaka kwa ajili ya mizigo yao ili kuwapunguzia safari ya kusafiri hadi Dar es Salaam.

TPA tayari imeshakamilisha ujenzi wa ofisi yake nchini Rwanda kwa ajili ya kuhudumia wateja wake toka nchini humo. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu, ofisi hiyo ya TPA nchini Rwanda imekamilika na kinachosubiriwa ni ufunguzi baada ya kukamilisha taratibu zote ili ianze kazi rasmi.

“Ufunguzi wa ofisi hiyo utasaidia sana kuimarisha huduma kwa wateja wetu wa Rwanda ambao wanatumia Bandari ya Dar es Salaam,” amesema Kakoko. 

Naye Balozi wa Rwanda nchini, Mhe. Eugene Kayihura ameishukuru TPA na Serikali ya Tanzania kwa kuwapatia eneo la kuhifadhia mizigo iendayo Rwanda.

Balozi Kayihura amesema kwamba biashara kati ya Tanzania na Rwanda imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika siku za hivi karibuni mara baada ya TPA kuimarisha huduma zake.

“Kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikihudumia asimilia 90 ya mizigo yote inayoingia na kutoka Rwanda hivyo kuweka rekodi ya ukuaji wa haraka sana wa mizigo ya Rwanda inayohudumiwa nchini,” amesema Mhe. Balozi Kayihura.

Amesema kwamba ziara yake aliyoifanya bandarini ni sehemu ya juhudi za Rwanda kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Tanzania haswa kwa kupitia huduma bora zitolewazo na Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.

Katika mkakati wake wa kuhakikisha inakuwa karibu na wateja wake, TPA hivi karibuni ilishiriki katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa nchini Rwanda ambapo pamoja na mambo mengine ilikutana na wafanyabiashara wa nchi hiyo ambao walionesha kuridhishwa na huduma za bandari ya Dar es Salaam.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: