TAARIFA YA SPIKA KUHUSU TUKIO LA KUSHAMBULIWA KWA
MHESHIMIWA TUNDU ANTIPHAS LISSU, MBUNGE WA SINGIDA
MASHARIKI (CHADEMA)

  1. Tukio lilivyotokea

Jana tarehe 07 Septemba, 2017 majira ya saa 7: 00 Mchana mara baada ya Bunge kusitishwa Mheshimiwa Tundu Antiphas Lissu (Mb) alitoka Bungeni kwenda nyumbani kwake kwa ajili ya mapumziko.  Alipofika nyumbani kwake Area D (Site III) kabla hajashuka kwenye gari yake, watu wasiojulikana wakiwa kwenye gari jeupe aina ya Nissan ambalo namba zake hazikutambulika walianza kushambulia gari la Mheshimiwa Lissu kwa Risasi kadhaa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma SACP Giles Mloto risasi zilizotumika ni kati ya 28 mpaka 32.  Risasi kadhaa zilimpata kwenye mwili wake kama ifuatavyo:-

  1. Mkononi risasi moja;
  2. Miguuni risasi mbili; na
  3. Tumboni risasi mbili

Baada ya tukio hilo watu hao walikimbia.

  1. Matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma

Mara baada ya tukio hilo, Tundu Lissu alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu.  Mheshimiwa Tundu Lissu alipelekwa Hospitali kwa kutumia gari la familia ya Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kuwa wanaishi jirani.  Alipofika Hospitali aliingizwa moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji na kufanyiwa upasuaji kuzuia damu kuendelea kutoka katika majeraha aliyokuwa ameyapata.  Upasuaji huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt.  Usubisye Mpoki akisaidiwa na Madaktari Bingwa wa Mkoa wa Dodoma.  Baada ya upasuaji huo ilielezwa kuwa hali yake inatengemaa na anaweza kusafirishwa kwa matibabu zaidi.

Hivyo, Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) uliagiza ndege ambayo ilifika Dodoma saa 10.30 jioni kwa ajili ya kumchukua mgonjwa na kumpeleka Hospitali ya Rufaa Muhimbili kwa matibabu zaidi kama taratibu zetu za kawaida zilivyo.  Hata hivyo, baada ya mashauriano, familia na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni walishauri kuwa ni vema mgonjwa apelekwe Hospitali ya Agha Khan, Nairobi.  Hivyo, saa 4: 30 usiku ilifika ndege nyingine ya Kampuni ya Flying Doctors na kuondoka na mgonjwa saa 6.00 usiku kuelekea Nairobi nchini Kenya.

Katika safari hiyo Mheshimiwa Tundu Lissu ameambatana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mheshimiwa Mch. Peter Msigwa, Mke wa Mheshimiwa Tundu Lissu na Madaktari wawili toka Kampuni ya Flying Doctors.  Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya alishauri Surgeon kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambaye alimfanyia upasuaji Mheshimiwa Tundu Lissu hapa Dodoma naye aambatane na Mgonjwa na kumkabidhi kwa madaktari wa Agha Khan Nairobi, hivyo naye ameambatana na msafara huo.

  1. Juhudi za kuwatafuta wahalifu

Tukio hili liliripotiwa Polisi ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma waliahidi kwamba Jeshi la Polisi litafanya doria na msako wa kuwatafuta wahalifu hao kasha Serikali itatoa taarifa kamili ya tukio hilo kwa kuzingatia taratibu za Bunge.

  1. Wabunge wachangia
Leo kulikuwa na kikao cha pamoja cha Kamati ya Uongozi na Tume ya Utumishi wa Bunge ambapo pamoja na mambo mengine wamekubaliana wabunge wote kuchangia nusu ya posho ya kikao kimoja ambayo ni jumla ya Shilingi Milioni 43 ikiwa ni mchango wa Bunge kwa familia kwa ajili ya matibabu

Imetolewana:
Ofisi ya Spika,
P.O.Box 941
DODOMA.

08 Septemba, 2017.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: