Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, akizungumza na wahandisi (hawapo pichani), wakati wa kufunga Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), Mhandisi, Profesa Ninatubu Lema, akisisitiza jambo wakati wa kufunga Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.
Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), Mhandisi Patrick Barozi, akisoma maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika mjini Dodoma.
Baadhi ya wahandisi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga (hayupo pichani), wakati wa kufunga Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.
Katibu Mkuu wa wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, akimkabidhi cheti mmoja wa watoa huduma aliyefanya vizuri katika utoaji wahuduma bora kwenye Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma. Wa tatu kulia ni Mkurugenzi wa Barabara kutoka Sekta hiyo Mhandisi Ven Ndyamukama, akishuhudia tukio hilo. Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, amezungumzia umuhimu wa Wizara, Taasisi na Idara za Serikali kutumia vifungu vilivyopo kwenye sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2011 na kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013 na marekebisho yake ya mwaka 2016.

Sheria hiyo inawapa fursa makandarasi wazalendo, watalamu washauri, wa zabuni na watoa huduma mbalimbali kupata fursa nyingi katika miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini.

Akifunga maadhimisho ya 15 ya Wahandisi mjini Dodoma, Mhandisi Nyamhanga, amesema chini ya sheria ya sasa miradi isiyozidi bilioni 10 imewekewa utaratibu mzuri wa kutekelezwa na makandarasi wazalendo na hivyo kuwawezesha kukuza uwezo wa kitaaluma na kiuchumi.

"Hakikisheni mnapopata miradi hii mnafanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia muda na thamani ya fedha ili kuongeza tija katika miradi yenyewe na kutoa fursa kwa miradi mikubwa kupewa makandarasi wazalendo", amesema Mhandisi Nyamhanga.

Amewataka wahandisi kutumia maadhimisho ya 15 kama somo la kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa ili kufikia malengo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati yenye viwanda na rasilimali watu wenye weledi wa kisasa.

Aidha, ametoa wito kwa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), kutoa kipaumbele kwa wanafunzi waliohitimu katika kozi ya kihandisi kwa kugharamia mafunzo kwa vitendo kwa kutumia fedha zinazotolewa na Serikali na zile za wafadhili ili kuweza kuendeleza taaluma kwa Wahandisi.

"Wizara itaendelea na mkakati wake wa kufadhili mafunzo kwa vitendo na kuhakikisha wahitimu wa vyuo mbalimbali vya wahandisi nchini wanakidhi mahitaji soko la ajira ndani na nje ya nchi", amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Mhandisi Profesa Ninatubu Lema, amewapongeza watoa mada wote walioshiriki katika maadhimisho ya 15 na kuahidi bodi hiyo itayafanyia kazi mafunzo hayo na kuhakikisha kila mhandisi ananufaika na mafunzo hayo.

katika maadhimisho hayo wahandisi wamepata fursa ya kujifunza maswala ya utafiti na maendeleo, ubunifu, masoko na ujasiriamali, maendeleo ya viwanda na utunzaji wa mazingira, na uharakishaji wa Teknolojia, habari na mawasiliano kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.

Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya ERB, Mhandisi Patrick Barozi, amesema bodi hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha wahandisi wanapata mazingira mazuri ya kufanya kazi ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na ubora unaopimika.

Maadhimisho ya 15 ya Wahandisi yaliyofunguliwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Balozi John Kijazi na kufungwa leo na Katibu Mkuu (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga yamelenga kuwakutanisha wahandisi kujadili kwa pamoja "Jukumu la Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati katika Kukuza Viwanda kwa Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi",

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: