Afisa Maendeleo ya jamii kata ya Kwembe, Lucy Njela akielezea mikakati ya kuimarisha na kuboresha ushirikiano wa kutatua changamoto za vijana na kuboresha ustawi na Maendeleo ya vijana katika Kata yake. Alimalizia kwa vijana ni sehemu kubwa ya maendeleo katika jamii yoyote ile, tuwape nafasi ya kufanya maamuzi na kuheshimu maamuzi yao.
Baadhi ya wadau wa maendeleo ya Vijana wakichangia mada kwenye mkutano uliowakutanisha ili kuangalia namna ya kufanya kazi kwa ukaribu na vijana ili kuweza kufikia malengo yao waliyojiwekea.
Mwezeshaji wa mkutano huo, Saddam Khalfan akihamasisha washiriki hasa vijana kupitia Sera ya Taifa Maendeleo ya Vijana kama mwongozo wa kuratibu na kusimamia kazi na shughuli za maendeleo ya vijana hapa nchini.
Baadhi ya Vijana, wadau na viongozi wa kata ya Mbezi wakijadili mikakati ya kutatua changamoto za Vijana na kuboresha ustawi wa vijana katika kata yao.
Wadau wa Maendeleo ya Vijana katika Manispaa ya Ubungo wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumalizika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa La Paz Resort, Luguruni jijini Dar.

Shirika lisilo la kiserikali la Mpakani Tunaweza kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society wameandaa mkutano wa siku moja uliowakutanisha wadau wa maendeleo ya Vijana mahususi kujadili namna yakutatua changamoto za Vijana katika Manispaa ya Ubungo.

Mkutano huo umetoa fursa kwa wawakilishi wa majukwaa ya Vijana ya kata ya Mbezi, Msigani, Kwembe na Mabibo kuzungumzia changamoto za Vijana, fursa zilizopo, vipaumbele vyao na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha ustawi wa vijana katika Manispaa ya Ubungo.

Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Mpakani Tunaweza, Bi. Assia Khalifa alishukuru wadau wa maendeleo ya vijana kwa kutengeneza mkakati wa kila kata kusimamia na kutathmini masuala ya Maendeleo ya Vijana pamoja na Viongozi wa Kata kukubali jukumu la kuyalea majukwaa hayo ya Vijana.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Madiwani wa kata ya Kwembe na Msigani, watendaji na Viongozi wa Manispaa ya Ubungo pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia za Manispaa ya Ubungo.

Mikakati iliyotengenezwa kwenye mkutano huo imelenga namna ya kuwajengea uwezo Vijana kuchangamkia fursa zilizopo, kuwashirikisha Vijana katika shughuli za Maendeleo, kuwapatia mafunzo na ushauri wa masuala ya Uongozi na kufanya kazi kwa kushirikiana kati ya wadau wa maendeleo ya vijana, viongozi wa serikali na majukwaa ya Vijana.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: