Na Mathias Canal, Singida

Mfuko wa Pensheni wa PSPF kupitia mpango wake wa uchangiaji wa Hiari (PSS) umeendelea kuyafikia makundi mbalimbali kujiunga na mpango huo ambapo pamoja na mambo mengine umeendelea kusaidia jamii ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali.

Mapema Leo asubuhi Novemba 25, 2017 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amekabidhiwa mabati 100 na Meneja Uendeshaji wa Mfuko wa Penseni (PSPF) Mkoani Singida Bi Hafsa Ally kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo.

Mabati hayo yametolewa na PSPF Kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Uongozi wa Wilaya ya Ikungi inayoongozwa na Mhe Mtaturu katika kuimarisha mfuko wa elimu kwa muktadha wa kuboresha elimu ikiwa ni pamoja na kuhimiza utatuzi wa Changamoto mbalimbali katika Wilaya ya Ikungi ikiwemo Upungufu wa nyumba za walimu, Vyumba vya madarasa, Ofisi za walimu, Maabara, Thamani mbalimbali, Matundu ya vyoo vya walimu na wanafunzi.

Akizungumza katika dhifa ya makabidhiano ya mabati hayo iliyofanyika katika eneo la shule ya sekondari Ikungi Mhe Mtaturu ambaye pia ni mlezi wa mfuko wa Elimu amewasihi wananchi na wadau kuchangia fedha au thamani zozote kadri wawezavyo ili kufanikisha kuboresha miundombinu ya elimu katika wilaya hiyo.

Sambamba na hayo pia ameushukuru Uongozi wa Mfuko wa Penseni PSPF kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli katika kuboresha elimu kwa manufaa ya watanzania wote.

Aidha, ameupongeza mfuko huo wa PSPF kwa mpango wao wa uchangiaji wa hiari ambapo mwanachama hutakiwa kuwa na umri wa kuanzia miaka 18 , ili kuwa huru kuchagua muda wa kuchangia kutegemea kipato chake ambapo kiwango cha chini kikianzia Shilingi 10,000 ambayo mwanachama anaweza kulipia kupitia benki.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa mfuko huo, Meneja Uendeshaji wa Mfuko wa Pensheni (PSPF) Mkoani Singida Bi Hafsa Ally Ameeleza kuwa PSPF ipo karibu na watumishi lakini pia ipo karibu na jamii hivyo wamempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi kuwashirikisha kwenye jambo hilo muhimu la kuboresha elimu katika wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla wake.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: