WAKATI wafanyabiashara wengi huandamwa na hofu juu ya wevi kwenye pesa zao, hali ni tofauti kwa Mzee Mtalikidonga. Takribani kilometa 78, mashariki ya mji wa Njombe, zinapoanzia safu za milima ya Lukumburu, umbali mfupi tu kabla ya kukifikia kijiji cha Igawisenga, ndipo nyumbani kwa mzee huyu.

Biashara ya asali, viazi mviringo, tangawizi, maparachichi, ndizi na bidhaa nyinginezo za kilimo, zinajiendesha zenyewe.

Zinajiuza zenyewe. Ndiyo maneno yanavyoweza kusema.

Kwa kutumia mkaa, juu ya mabanzi yaliyogeuzwa hivyo kufanya mbao za kibanda, bei za kila bidhaa huandikwa.

Katikati, kuna birika dogo la rangi ya fedha. Ndiyo sefu ya fedha kutoka kwa wateja.

Tofauti na biashara tulizozizowea ambapo, muuzaji humhudumia mnunuzi huku wakipeana pesa taslimu, ama hundi; ama pengine, biashara mtandaoni zenye utaratibu maalumu wa kusimamia miamala, yote hayo hayafanyiki kwa Mzee Mtalikidonga.

Mteja, akishafahamu bidhaa anayoihitaji, na kuisoma bei kama ilivyoandikwa, hufunua mfuniko wa birika hilo dogo. Kisha, huweka pesa hiyo. Ataichukua bidhaa yake na kuondoka zake. Hapati nafasi ya kukutana na Mzee Mtalikidonga.

Kama fedha aliyoiweka inahitaji chenji, mteja mwenyewe hujihesabia chenji anayoistahili. Kisha kwenda zake.

"Nini hutokea kama mtu akifanya uhuni hapa; akaondoka na asichokistahili?" Siachi kumwuliza swali hili mwanamke mmoja wa makamo, mtumishi wa Mzee Mtalikidonga, anayetekwa na udadisi wangu.

"Asifiha wutali, alapiluha ye mwene!" (Hawezi fika mbali, atarudi mwenyewe). Ndivyo ninavyojibiwa.

Ninaamua kununua asali kutoka kwenye chupa ndogo. Bei yake ni shilingi 3,000/=. Mfukoni ninatoa noti ya shilingi 5,000/=.

Nafunua birika lile. Nakuta pesa nyingi za noti. Zaidi ya laki moja kwa hesabu ya macho madakuzi. Naiona noti ya shilingi 2,000/=. Naichukua. Nalifunika birika. Halafu, nachukua chupa ile na kuondoka zangu.

Ama kweli, tembea uone!

Fadhy Mtanga, 
Njombe, Tanzania. 
Jumatano, Disemba 13, 2017.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: