Katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na watoto,Shirika la Kivulini limefanya kikao cha wana mabadiliko kwa ajili ya kufanya tathmini na mrejesho wa shughuli za mradi wa usawa wa kijinsia kujenga uwezo kiuchumi kwa wanawake na vijana unaotekelezwa halmashauri wilaya mbili za Shinyanga na Kishapu mkoani Shinyanga.

Kikao hicho kilichokutanisha wana mabadiliko 65 kutoka vijiji vitano vya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Shinyanga Vijijini) ambavyo ni Nyida,Nsalala,Butini,Nduguti na Welezo kimefanyika leo Disemba 5,2017 katika Ukumbi wa mikutano wa Empire Hotel mjini Shinyanga.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa mwandamizi wa mradi huo, Bi. Eunice Mayengela alisema lengo la kikao hicho ni kujadili mafanikio na changamoto ambazo wana mabadiliko wanakutana nazo kwenye maeneo yao katika kutekeleza mradi.

Mayengela alisema suala ya ukatili dhidi ya wanawake ni la jamii nzima hivyo panahitajika ushirikiano wa pamoja ili kuhakikisha vitendo hivyo vinatoweka katika jamii.

“Lazima tushirikiane kwa pamoja kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,wana mabadiliko,serikali na wadau wengine tunapaswa kuungana ili tuwe na nguvu ya pamoja”,aliongeza Mayengela.

Mayengela alitumia fursa hiyo kuwataka wanawake kuacha uoga wanapofanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo kubakwa na badala yake watoe taarifa kwenye vyombo vya sheria ili kukomesha vitendo hivyo katika jamii.

Naye afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Deus Masili Mhoja aliwataka wanawake kupaza sauti wanapofanyiwa ukatili.

“Akina mama pazeni sauti,fuateni sheria,msiwahurumie sana hawa wanaume,nanyi wanaume acheni mila na desturi zilizopitwa na wakati,wapeni urithi wa mali ikiwemo ardhi wake zenu,hata kupigana katika ndoa nako kumeshapitwa na wakati”,alieleza Mhoja..
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: