By Bakari Kiango, Mwananchi bkiango@mwananchi.co.tz

Wahenga walisema mdomo uliponza kichwa na hilo ndilo linaloonekana kumfika rais wa Marekani, Donald Trump baada ya viongozi, wanadiplomasia na wasomi barani Afrika kumshutumu kutokana na yake kuwa bara la Afrika lina “nchi chafu”.

Wote wanasema Trump, ambaye amekuwa akitoa matamko tata, anapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote.

Hivi karibuni, vyombo vya habari vya Marekani yakiwamo mashirika makubwa kama CNN na Washington Post yalinukuu vyanzo vya uhakika vikisema kwamba Trump aliyaita mataifa ya Haiti, El Salvador na baadhi ya nchi za Afrika kuwa “mataifa machafu”.

Alikaririwa akisema hayo katika kikao chake na wabunge wa vyama vyote Alhamisi iliyopita kujadili pendekezo la mpango wa wahamiaji usiopendelea upande wowote.

Rais huyo anadaiwa kuhoji: “Kwa nini tunawaruhusu watu hawa kutoka ‘nchi chafu’ kuingia nchini?”

Baada ya kutoa kauli hiyo ambayo baadaye alijaribu kuipoozesha kupitia akaunti yake ya Twitter akidai kwamba hakutumia maneno hayo, japo aliyoyasema alitumia “lugha kali”, mataifa, taasisi, vyama na watu binafsi walijitokeza kulaani.

Botswana ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kumshtumu na kusema kauli ya Rais huyo ni kukosa kuwajibika.

“Linakera na ni uthibitisho wa ubaguzi wa rangi,” imesema Botswana katika taarifa yake.

Botswana imemuita balozi wa Marekani aliyeko Gaborone ili afafanue iwapo taifa hilo kubwa kiuchumi linachukulia nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika kama “taifa chafu na taifa la mabwege”.

Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Adolf Mkenda alisema Tanzania imewakilishwa katika tamko la mabalozi wa nchi 54 za Afrika katika Umoja wa Mataifa (UN), waliotoa msimamo dhidi ya Trump.

“Pia Tanzania ni sehemu ya (Umoja wa Afrika) AU ambayo nayo imetoa tamko,” alisema Profesa Mkenda.

Katika tamko lao la pamoja, mabalozi hao wamelaani maneno ya kibaguzi, chuki na yenye kukasirisha yaliyotolewa na Trump na wamemtaka ayafute na kuomba radhi.

Wakati Trump akisema hayo, mwaka 2015 Marekanihe ilifanya biashara na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyofikia dola 37 bilioni. Nchi hizo ni sehemu kubwa ya bara la Afrika.

Marekani iliuza nje bidhaa za thamani ya dola 18 bilioni na kuagiza bidhaa zenye thamani ya dola 19 bilioni, ikiwa ni nakisi ya dola 1 bilioni.

Trump amekuwa akilalamikia kutokuwepo na usawa kibiashara na China ambayo nakisi yake ilikuwa dola 300 bilioni mwaka 2016.

Biashara na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara inahusisha zaidi mafuta ghafi, huku Nigeria ikiuza bidhaa hiyo yenye thamani ya dola 11.7 bilioni. Lakini Trump aliwahi kusemna mwaka jana kuwa Wanigeria wanaoenda Marekani,hawawezi kurudi kwao kuishi kwenye vibanda.

Juzi Umoja wa Afrika ulitoa taarifa ukieleza kusikitishwa kwake na matamshi ya Trump na kumtaka ayafute na kuomba radhi Waafrika.

Ebba Kalondo, msemaji wa mwenyekiti wa umoja huo, alisema AU inaalani vikali matamshi hayo yasiyo na heshima na inamtaka ayafute na pia awaombe radhi si Waafrika tu, bali watu wote wenye asili ya Afrika duniani.

Nchini Tanzania baadhi ya wasomi na wanadiplomasia waliungana na AU na Botswana kukemea kauli hiyo ya Trump.

Profesa Gaudence Mpangala Chuo Kikuu cha Ruaha alisema sera za Marekani na mataifa madogo hasa ya Afrika ni kusaidiana na kuwa na uhusiano mzuri lakini kwa Trump hilo halipo.

“Nafikiri hata Wamarekani wenye nia njema hawana imani na Rais Trump. Ni rais mwenye misingi ya ubabe na anayefanya uamuzi wake binafsi,” alisema.

“Nchi za Ulaya ni washirika wake wakubwa, lakini kuna wakati wanapingana na Trump kutokana na maamuzi yake. Kwa kauli hii itaifanya Marekani kutokuwa na uhusiano mzuri na mataifa aliyoyataja rais wao.”

Kauli ya Trump pia ililaaniwa na Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) ambaye alisema Marekani ina uhusiano mzuri wa kidiplomasia na nchi za Afrika.

“Niliposikia kauli hii ya Trump haikunishangaza. Kwa sababu aliwahi kusema nchi za Afrika zinapaswa kutawaliwa tena,” alisema.

Profesa Baregu alisema ni wakati pia kwa nchi za Afrika kujiimarisha kidemokrasia na kuangalia namna zinavyojiendesha kiutawala kwa kuwa nchi za Ulaya na Amerika zinawaangalia.
 
Alisema muda mwingine baadhi ya nchi za Afrika zinajitakia kutokana na vitendo vyake kama vya kuomba misaada kwa mataifa hayo.

Aliyekuwa kuwa balozi wa Tanzania katika nchi za Japan, India, Malaysia na Sir Lanka, Dk Ahmed Kiwanuka alisema: “Marekani ni taifa kubwa, lakini kwa hili itashuka hadhi yake maana kiongozi wake hana utu wala hekima.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: