Na Kajunason/MMG-Dar.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imelishutumu gazeti la Nipashe kwa kuandika habari ya ukatazwaji wa uvaaji wa nguo fupi (vimini) na unyoaji wa mtindo wa kiduku ambayo imeleta sitofahamu kwa jamii.

Akitoa ufafanuzi mapema leo katika baadhi ya vyombo vya habari hususani televisheni kwa nyakati tofauti, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Lazaro Mambosasa wakati akielezea operesheni mbalimbali ambazo jeshi hilo limekuwa likiziendesha ili kupambana na majambazi.

"Napenda kupingana na mwandishi aliyeandika habari katika gazeti la Nipashe la Januari 17, 2018 iliyokuwa na kichwa kilichoandikwa "Polisi yakamata wavaa vimini, kunyoa viduku", napenda kukanusha maneno ambayo binafsi sikuyasema," Kamanda Mambosasa.

"Katika hili lililoleta tafrani ni uzushi wa gazeti la Nipashe, juzi nilifanya mkutano na waandishi wa habari na alijitokeza mwandishi mmoja mwanadada wa gazeti la Nipashe aliuliza swali akihusisha matukio hayo kutokea Arusha lakini nilimjibu kuwa mimi ni msemaji wa Kanda maalum ya Dar es Salaam siwezi kuyasemea mambo ya Arusha, na Dar es Salaam hatuna msako huo na hatuna mpango huo," alisema Kamanda Mambosasa.

Kamanda Mambosasa alisema kuwa kuna matendo ambayo ukiyatenda yanakwenda kinyume cha sheria na sheria lazima iwepo na jeshi la polisi lazima likukamate, kwa nguvu iliyopo.

Alisema kuwa suala la Mavazi halijatungiwa sheria, hakuna vazi la taifa... ila kuna matendo yanafikia unakeuka sheria... na kuna matendo unakiuka maadili... Hauwezi kuvaa sketi fupi ukaenda kanisani au msikitini maana unaweza kuleta tafrani ila vimini hivyo kuna sehemu unaweza kuvaa wala watu wasishtuke mfano mfukweni... Yeyote anayekwenda kule lazima akutane navyo hawezi kushangaa.

Aliongeza kuwa suala la kunyoa viduku, au kuvaa vimini ni si biashara ya jeshi la polisi, sisi tupo kwa ajili ya kuwalinda raia na mali zao.

Mwisho alipenda kuwaasa waandishi wa habari kuandika kile ambacho anakitoa tu na si kujaza mambo mengine ambayo yanaleta sintofahamu kwa jamii.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: