Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Bwana Masanja Kaodogosa (wa pili kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) kazi ya kukarabati reli ikiendelea unaofanywa na wafanyakazi wa Shirika hilo baada ya kuharibika kwa mvua wakati wa ziara yake ya kukagua ukarabati huo katika kijiji cha Mkadage kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akishuka kwenye tingatinga inayojaza udongo kwenye eneo lililopo katika kijiji cha Munisagala kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro baada ya kukagua kazi inayoendelea ya kujenga na kurejesha miundombinu ya reli iliyoharibika na mvua wakati wa ziara yake kwenye eneo hilo. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bwana Masanja Kadogosa.
Kazi ya kujaza udongo kwenye eneo la ukubwa wa mita 170 lililopo katika kijiji cha Munisagala kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro ikiendelea kwa ajili ya kujenga na kurejesha miundombinu ya reli iliyoharibika na mvua.
Mhandisi Mkuu Ujenzi wa TRL Mhandisi Nelson Ntejo akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano (kulia) uharibifu wa miundombinu ya reli uliotokea kutokana na mvua wakati wa ziara yake ya kukagua uharibifu huo na ukarabati unaoendelea kati ya Kilosa, Morogoro na Gulwe, Dodoma. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bwana Masanja Kadogosa.

Serikali imetoa miezi sita kwa wananchi wanaolima ndani ya eneo la hifadhi ya reli inayopita Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kuhama eneo hilo baada ya kuvuna mazao yao ili kuhifadhi miundombinu ya reli na kupunguza uharibifu wa miundombinu hiyo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ua Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake alipotembelea kukagua ukarabati wa reli iliyopo eneo la Kilosa, Morogoro na Gulwe, Dodoma lenye umbali wa kilomita mia moja baada ya kuharibika kwa mvua na Serikali kusitisha usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa mbali mbali na nchi za jirani.

Nditiye amesema kuwa uharibifu wa eneo hilo ni wa kiwango kikubwa kwa kuwa katika kipande cha umbali wa kilomita mia moja zilizoharibika kwa mvua baadhi ya maeneo reli imebomoka, kuhama kwenye njia yake na ardhi husika kuliwa na maji ya mvua yaliyojaa kwenye mto Mkondoa ambao unapita pembezoni mwa reli hiyo.

Ameongeza kuwa uharibifu huo unasababishwa na shughuli za kibinadamu ambapo wananchi wanaishi na kulima ndani ya mita thelathini upande wa kulia na kushoto mwa reli ambapo ni hifadhi ya miundombinu ya reli na wananchi hawaruhusiwi kutumia eneo hilo kwa shughuli yeyote. “Nakuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bwana Masanja Kadogosa ushirikiane na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kuwahamisha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hii wakishavuna mazao yao kwa kuwa kilimo kinasababisha mmomonyoko wa udongo hivyo kuharibu miundombinu ya reli”, amesisitiza Mhandisi Nditiye.

Amesema kuwa Wizara yake itawasiliana na kushirikiana na Wizara ya Maji, Kilimo na Umwagiliaji ili waweze kukarabati mabwawa makubwa matatu ya Hombolo, Kidete na Manyara ili yaweze kuhifadhi maji na kuyadhibiti kama ilivyokuwa hapo awali ili yasipitilize kuingia kwenye mto huo bila kufunguliwa kwa utaratibu na kuharibu miundombinu ya reli.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Bwana Masanja Kadogosa amesema kuwa tayari Shirika lake limeleta vifaa na wafanyakazi katika eneo hilo ambapo wanafanyakazi kazi mchana na usiku ili kuhakikisha kuwa reli hiyo inaanza kutumika tena kwa shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo.

Ameongeza kuwa kwa siku Shirika lake linapoteza takribani shilingi milioni mia mbili ambazo ni chanzo cha mapato kwa Shirika hilo na Serikali kwa ujumla. Amesema kuwa Shirika lake limefanya tathmini na kubaini kuwa kiwango cha uharibifu wa reli hiyo ni kikubwa na tayari ameiomba Serikali impatie jumla ya shilingi million 994 za kukarabati eneo hilo.

Aidha, Bwana Kadogosa amewashukuru wakandarasi wanaojenga reli mpya ya kisasa ya SGR kwa kuwa wazalendo na kuwapatia vifaa ambavyo wanavitumia kukarabati eneo hilo. Mmoja wa wafanyakazi wa Shirika hilo akiwa katika moja ya eneo la tukio lililopo katika kijiji cha Mkadage wilayani Kilosa mkoani Morogoro, akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Bwana Jumanne Kinyasi ameiomba Serikali kumpatia Bwana Kadogosa fedha hizo na kuwaongeza vifaa ili waweze kukarabati reli hiyo ili waweze kurejesha huduma kwa wananchi.

Bwana Kadogosa amemweleza Mhandisi Nditiye kuwa ukarabati huo utakamalika mapema wiki ya pili ya mwezi Januari mwaka huu. Bwana Kadogosa alifafanua kuwa reli hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto ya kuharibika kila baada ya kipindi cha miaka kumi ambapo iliwahi kuharibika tena mwaka 1998, 2007 na sasa mwaka huu 2018 kutokana na mabadiliko ya majira ya mvua, tabia nchi na hali ya hewa.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: