*Mkurugenzi aelezea namna wanavyotoa elimu ya  kuokoa maisha ya mama mjamzito

*Wapania kumfanya mwanamke mjamzito kuwa malkia, mwanamke shujaa na mwenye thamani 

*Aprili 6 mwaka huu Rais Mstaafu , Dk. Jakaya Kikwete  mgeni rasmi sherehe ya miaka mitano  ya uwepo wa CSI.

 Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

NGUVU ya mwanamke na iheshimiwe, itukuzwe maana imeshafanya mapinduzi mengi duniani na yoyote mwenye kumdharau au kumuumiza mwanamke hafai kutambulika kama binadamu mwenye kujitambua.

Ukweli ni kwamba mwanamke ni malkia na maisha yake ya sasa na baadae yanahitaji heshima kubwa. Pamoja na hayo mheshimu mwanamke maana wewe umetoka ndani yake, na unamwita mama.

Mwanaume ili aitwe baba anahitaji mwanamke. Mwanaume mwenye akili  timamu huhitaji mapenzi ya kweli na hayo hayapatikani kwingine zaidi ya kwa mwanamke. Mwanamke ni maisha.

Unaweza kujiuliza kwanini nimeanza kwa kueleza yote hayo. Kabla sijajibu sababu ya kuelezea hayo kwa kina niongeze tu mwanamke ni kiumbe mwenye thamani  mbele ya viumbe vilivyopo chini ya jua .

Kwanini? Jibu ni kwamba pamoja na sababu nyingine nyingi lakini Mungu amempa kazi moja ambayo ni muhimu katika maisha ya mwanadamu. Mwanamke ndio mwenye uwezo wa kuleta  mtu mpya duniani.

Kwa kutambua thamani ya mwanamke na namna ambavyo anahitaji kulindwa na kuthaminiwa Shirika la Kimataifa la Childbirth Survival International (CSI) ambalo Makao Makuu Ukonga wilayani  Ilala jijini Dar es Salaam.


Ni shirika ambalo pamoja na majukumu mengine kwa sehemu kubwa limejikita katika kuhakikisha maisha ya mama mjamzito yanakuwa salama. Wanahitaji kuona maisha ya mama mjamzito yanakuwa yenye uhakika wa kuishi kabla na baada ya kujifungua.

Shirika la Kimataifa la Childbirth Survival International (CSI) ni shirika ambalo limesheheni watalaamu wa afya ya uzazi na ndio maana wamejikita katika kuokoa maisha ya mama mjamzito pamoja na mtoto wake. Wamechukua jukumu hilo kwa kutambua kuna changamoto ambazo zimekuwa chanzo cha vifo vya wanawake  wajawaziti na watoto wachanga wanaozaliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la CSI , Stella Mpanda ambaye ndio mwanzilishi wa shirika hilo amefafanua kwa kina malengo na mikakati  ya kuokoa maisha ya mama mjamzito.

Akizungumzia majukumu wanayofanya CSI, akiwa kwenye Makao Makuu ya Ofisi hiyo iliyopo Ukonga jijini Dar es Salaam,  Mpanda anasema pamoja na majukumu mengi wanayofanya wamejikita zaidi kuokoa maisha ya mama mjamzito na mtoto kwa kutoa elimu kwa wajawazito umuhimu wa kwenda kliniki.


Pia kutoa elimu ya dalili za hatari kwa mama mjamzito, kutoa mafunzo kwa wakunga, kusaidia vifaa vya kujifungulia pamoja na kujikita katika kutoa elimu kwa jamii ya rika mbalimbali kuhusu elimu ya kujitambua na hasa kwa mtoto wa kike. Kazi ambayo wamekuwa wakiifanya kwa bidii na kila aina ya maarifa yao yote.

Mama Mpanda anasema taaluma yake ndio iliyomsukuma kuamua kuanzisha shirika hilo akiamini atatumia uwezo wake katika eneo hilo kusaidia jamii ya watanzania na hasa wanawake kwa ujumla.

Mkurugenzi huyo ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya afya ya uzazi na kutokana na uwezo alionao kwenye taaluma hiyo amebahatika kufanya kazi ndani na nje ya Tanzania. Mama Mpanda ni Muuguzi Mkunga, Mwalimu wa wauguzi, mwalimu wa wakunga na amefanya kazi hiyo kwa muda mrefu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Pia amefanya kazi Shirika la Afya Duniani ambako akiwa huko amehudumu katika nchi tofauti tofauti kabla ya kurudi Tanzania na kisha kuamua kuanzisha CSI mwaka 2013.

SABABU ZA KUANZISHA CSI  
Akizunguzia sababu za kuanzisha CSI, Mama Mpanda anasema moja ya sababu ni kwamba alifuatilia na kuona wajawazito wanapoteza maisha wakati wa kujifungua kwa kukosa elimu ya kawaida tu ambayo ingemsaidia kuwa salama kabla na wakati wa kujifungua.

"Nimesomea ukunga katika kiwango cha Uzamili (Mastars). Hivyo kuna sababu ambazo nikiziona au kusikia ndio zimesababisha mama mjamzito kupoteza maisha huwa naumia sana. Nikaona ipo haja ya kuanzisha shirika ambalo litajikita kutoa elimu ya afya ya uzazi.

"Hivyo wazo hilo likawa na nguvu kwenye akili yangu kwamba lazima niwe na shirika ambalo litatoa elimu kwa jamii ambayo tunaamini itakuwa msaada mkubwa kuokoa maisha ya mama mjamzito na mtoto.Wazo hili likapata nguvu zaidi baada ya kukutana na Tausi Kagasheki ambaye yeye yupo nchini Marekani.

"Hivyo tukaamua kuwa na shirika hilo hata hivyo hatuji kwanini tuliamua liwe shirika la kimataifa wakati dhamira yetu ni kusaidia watanzania wenzetu. Uwepo wetu katika jamii umetoa fursa ya kuelimisha wananchi wengi kuhusu namna bora ya kumlinda mama mjamzito,"anasema.

Anafafanua kilichomsukuma zaidi aliamini CSI itasaidia kupunguza vifo kwa wajawazito kwani vifo vingi vinazuilika."Mama anapata uchungu wakati mwingine anakuwa mbali na hospitali na ili kuokoa maisha yake akipata maji mara kwa mara maana yake anaweza kufika hospitali na akawa salama.

Anasema ili kufahamu maji yanasaidia kuokoa maisha ya mjamzito inahitaji elimu tu ambayo ni ya kawaida, hivyo wakaona wanayo nafasi ya kuelimisha jamii kuhusu namna ambayo itaisaidia kuokoa maisha ya mama mjamzito.

"Nakumbuka mwaka 1970 nilienda kituo cha Afya Lugoba-Chalinze, tukiwa hapo usiku akaja mama ambaye alikuwa mjamzito na hali yake haikuwa nzuri kwani alikuwa ameanza kuumwa uchungu siku mbili nyuma na alama zote za kupasuka chupa ya uzazi zilikuwa tayari.

"Uzuri pale kulikuwa na gari ingawa changamoto kubwa ilikuwa ni mawasiliano.Hivyo huduma kubwa ambayo tulimpa ni maji ya mara kwa mara hadi tukafika Hospitali ya Taifa Muhimbili.Tukamkabidhi kwa daktari na bahati nzuri tuliokoa maisha yake.

"Hivyo nikawa nikaweka kitu moyoni lazima mbele ya safari niwe na kitu cha kusaidia wanawake wenye ujauzito na kweli baada ya kustaafu Shirika la Afya Duniani mwaka 2013 nikaanzisha CSI ambayo inatoa elimu ya uzazi,"amesema Mama Mpanda. 

Anaongeza wakati wanaanza walitamani kujikita katika mikoa ya Kagera na  Mara katika Wilaya ya Musoma ambako ni moja ya maeneo ambayo kuna vifo vingi vya mama wajawazito.

"Tuliamini kwa kutumia taaluma yetu tutafanikiwa kupunguza vifo vya mama mjamzito. Hata hivyo tukafanikiwa kupata Wilaya ya Biharamuro ili kutoa huduma zetu lakini ikatokea changamoto ya rasilimali fedha,"amesema.

Anasema kwa kuwa walikuwa na dhamira ya kusadia wananchi wakaanza kutafuta fedha kwa kuandika maandiko ya kuomba msaada wa fedha lakini pia ikashindikana.Hata hivyo hawakukata tamaa kwani waliona uwezo wa kutoa elimu ya afya ya uzazi wanayo.

WATOA ELIMU SHULENI
Mama Mpanda anasema kuwa CSI katika kuhakikisha wanatoa mchango wao kwenye jamii wakaanza kutao elimu mashuleni kwa kutoa elimu ya afya ya uzazi kulingana na darasa ambalo mwanafunzi anasoma.

"Tulikuwa tunafundisha namna ya kujikinga na HIV, makuaji na namna ambavyo mtoto anakuwa na kufahamu kila hatua anayopitia kwenye ukuaji, elimu ya kujitambua na pamoja na kutoa athari za kupata mimba mapema kwa wasichana,"amesema.

Anasema elimu hiyo wamekuwa wakiitoa katika maeneo mbalimbali na  katika na Mkoa wa  Dar es Salaam mbali ya kuifanya mashuleni na maeneo ya wazi pia wamejikita zaidi katika Wilaya ya Ilala hasa Ukonga ambako wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na viongozi wa Serikali za mtaa.

 "Tumekuwa na programu maalumu kwa ajili ya kufundisha wanafunzi na jamii kwa ujumla.Tumefanikiwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ambapo pia tumekuwa tukitoa elimu ya afya ya uzazi kwa wakunga na wauguzi wanaotoa huduma kwa mama mjamzito,"amesema Mama Mpanda.

Anafafanua kijana anapofikia umri wa kuingia utu uzima anakuwa na mihemko ya kila aina na jukumu letu ni kumsaidia namna ya kuhimili hiyo mehemko ya ujana asiingie kwenye mambo ambayo si wakati wake kuyafanya.Kwa wanafunzi wa
kike tunawakumbusha umuhimu wa kutimiza ndoto zao na watafanikiwa kwa kujitojiingiza kwenye mambo ya ngono,"amesema.

Pia anasema kwa wanafunzi walioko mashuleni wanatoa elimu ya namna ya kujiepusha na mitandao ambayo imekuwa ikihamasisha jami kujiingiza kwenye mambo ya ngono. 

"Kuna mitandao unaingia na kisha ukipakua tu mtandao wao utaona maelekezo , kwa mfano unaambiwa vua nguo...unakuta unavua na ukishakubali tu unakuwa mtumwa wa ngono.Hivyo ni jukumu letu kutoa elimu ya kujikinga na mitandao ya aina hiyo,"amesema.

Pia anasema wamejikita kutoa elimu kwa akina mama wajawazito dalili hatari kwa mjamzito.Pia namna ya kuhakikisha mimba inakuwa katika ukuaji ambao hautakuwa na athari kwa aliyeibeba.

MAFANIKIO YA CSI 
Kuhusu wamefanikiwa kwa kiwango gani tangu waanze kutoa huduma ya elimu kwa jamii, anasema wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa ingawa katika utoaji wa elimu ya uzazi.

"Hatujafanya thamini kwa njia ya madodoso lakini tunachoweza kutoa elimu kwa sehemu kubwa na tunaamini imesaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto.Kwetu sisi ni fahari elimu tunayotoa kuokoa maisha ya mama na mtoto hata kama watakuwa sita au saba.Kuokoa uhai wa mtu si jambo dogo,"amefafanua.

Pia kwa wakunga ambao wamewafundisha kuhusu ukunga wamebaini wote ambao wamepata mafunzo kutoa CSI wamekuwa wakitoa huduma nzuri na bora kwa wajawazito wanaofika kupata huduma.

"Wanatoa huduma zao kwa kiwango cha hali ya juu na huduma ya ukunga yenye heshima ambayo tunaweza kusema ni ya kutukuka.Kazi ambayo anafanya huyu mama ya kuleta binadamu mpya ni jambo la kutukuka na hata anapokuja leba lazima apewe huduma ambazo zinastahili. Tunaeleza athari za kutoa lugha chafu kwa mjamzito anapokuwa leba,"amesema.


MALENGO YA SASA NA BAADAE
Mkurugenzi huyo ambaye amekuwa akishirikiana kwa karibu na Tausi Kagasheki wa Marekani , anasema mikakati yao ni kuendelea kutoa huduma hizo kadri wanavyoweza ili kusaidia jamii ya Watanzania.

"Bado tunataka kuendelea kutoa huduma na hasa katika kujikita zaidi kwenye jamii .Tunataka kuzungumza na Serikali za mtaa na tuweze kumpa thamani mama mjazmito na hatimaye kuonekana kuwa malkia,"amesema Mama Mpanda.

Pia anasema watajikita kuendelea kutoa elimu kwa jamii kwa lengo la kuwajengea ujasiri na hasa mtoto wa kike asiwe mwoga mbele ya uso wa mwanaume."Kwa mfano tunawaambia wasichana wasiogope kumtaza mwanaume usoni.Unapomtaza mwanamke ndivyo ambavyo unatakiwa kumtaza mwanaume,"amesema.


UHUSIANO WAO NA SARIKALI
Anasema wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na Serikali na kila ambacho wanakifanya kama kutoa elimu lazima wapate kibali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto.

"Tunashirikiana vizuri na Serikali kwani ni muhimu katika kutuwezesha kufikia malengo yetu ya kuihudumia jamii ya Watanzania.Mbali ya Serikali tunashirikiana na mashirika mengine kadhaa ambayo nayo yanajihusisha na huduma kama ambazo tunazitoa.Tunafanya majukumu yetu kulingana namna ambavyo Serikali inataka,"amesema Mama Mpanda.

CSI YAAMINI KATIKA KUFANIKIWA
Pamoja na mambo mengine anasema kuwa nia yao ni kufanikiwa hata kama kuna changamoto ambazo zinajitokeza katika kutekeleza majukumu yao na kufafanua elimu ambayo wanaitoa kuhusu afya ya uzazi bado wanaifanya kwa kukutana na makundi mbalimbali na wataendelea kuifanya.

"Ni ngumu kufanikiwa kwa mara moja lakini nia ikiwepo tunaimani tutafanikiwa kwani tunaendelea kufundisha jamii na wakunga.Tunataka baa afahamu wajibu wake, mama naye afahamu na mkunga naye ajue wajibu wake,"amefafanua.

Pia anasema katika mikoa mikoa ambayo wamekwenda wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakitoa changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika maeneo ya utoaji huduma kwa mama mjamzito.

CHANGAMOTO INAYOWAKABILI
Anasema changamoto kubwa ni kukosa fedha kwa ajili ya kufanikisha majukumu yao na kwamba fedha za mfukoni ndio zinatumika zaidi kwani kokote ambako wanakwenda lazima watumie fedha zao wenyewe.

"Manispaa nyingi zinatuomba twende kwenye shule zilizopo kwenye maeneo yao lakini wakati mwingine tunashindwa kwasababu ya kukosa fedha.Kwa kuwa tunajulikana na Shirika la kimataifa basi hata unapoomba msaada hakuna anayekupa fedha wakiamini sisi ndio tunatakiwa kusaidia na si kusaidiwa.Hii ni changamoto kwetu lakini tunadhani huko mbele ya safari tutaangalia njia nzuri ya kuliita shirika letu,"amesema Mama Mpanda.

Hivyo ili kukabiliana na changamoto ya fedha, wamedhamiria kuanzisha miradi na hasa ambayo itahusika na uanzishaj wa maduka ya dawa na vifaa tiba na kwa sehemu kubwa watajikita katika vifaa vya tiba kwa mama mjamzito na mtoto.

"Tunafikiria kuanzisha maduka ya dawa na tutauza vifaa mbalimbali vya kujifungulia,"amesema Mpanda.


KIKWETE MGENI RASMI SIKU YA CSI
Pamoja na yote hayo, Mpanda anasema Aprili 6 mwaka huu wakuwa na sherehe itakayofanyika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam.Sherehe hiyo ni kwa ajili ya kutimiza miaka 5 tangu kuanza kwa shirika hilo.

Mpanda anasema mgeni rasmi katika siku hiyo muhimu ndani ya CSI atakuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

"Tunaisubiri kwa hamu siku hiyo ambayo kwetu tutakuwa na mengi ya kuelezea mafanikio na changamoto.Tutaitumia siku hiyo maalumu kutoa maombi yetu kwa Serikali hasa yale wanayodhani yatafungua milango ya kufanikisha yale tunayoyafanya.Itakuwa ni siku ya kipekee kwetu na watanzania kwa ujumla hasa wale wanaotambua kazi tunazofanya katika jamii,"anasema Mpanda.

WHO umefanya miwili Uswiz na kisha akaenda Nigeria miaka mine, Pakistan miaka minne.Jumla miaka 11 Pale amekaa kuanzia mwaka 1996 hadi mwaka 2007

Baada ya kurudi akafanya kazi ITECH ambalo ni shirika la kimataifa la Traing Education Centre for Health ambayo ipo Seattre State of Muhimbili aliingia mwaka 1967 ndio aliingia hapo akasoma kwa miaka minne na kumaliza mwaka 1972.

Baada ya hapo akaanza kufanya kazi Muhimbili Hospitali kwa muda wa mwaka mmoja na baada ya hapo akarudi tena Muhimbili kufundisha uuguzi levo ya cheti.

Akiwa chuoni ndipo ikaanza kozi ya ualimu kwani baada ya wazungu kutoka kukawa na tatizo la walimu.Hivyo ilianzisha shule yake ya ualimu. Walimu wauguzi pale Muhimbili na ndipo yeye akaenda kujifunza ualimu.

Yeye alianza kwa kusoma ile ya mwaka mmoja lakini akatoka hapo akiwa mwalimu haswa.

Akaenda Tanga na kuendelea kufundisha kwa mwaka mmoja na aliporudi tena akaenda Muhimbili. Mkuu wa Chuo cha Muhimbili ambacho kinatoa uuguzi na baada ya hapo akaenda kusoma digrii ya uuguzi Irend na baada ya kurudi akaenda chuo cha walimu kwa ajili ya kufundisha wauguzi.

1986 ambako alipata digrii ya Uuguzi unesi iliyokuwa na mchepuo wa ufundishaji kwa hiyo akarudi na kuwa mkuu wa chuo  pale shule ya uuguzi.

1992-1994 akaenda Uingereza kwa ajili ya kuchukua digrii ya pili ya ukunga ,

Aliporudi sasa yeye na wenzake wakaenda kuanzisha digrii ya uuguzi nchini ambapo akafundisha na kisha akaazimwa kwenda kwenda Muhimbili kuwa Matron 1995.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: