Balozi wa Japan Nchini Tanzania, Yoshida Masaharu (mwenye miwani) wakiweka jiwe la msingi la mradi wa Soko la Kimataifa la Samaki na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Joel Hari uliofadhiliwa na Serikali ya Japan kwa gharama ya Shilingi milioni 320 kijiji cha Kasenda Chato.
Balozi wa Japan Nchini Tanzania, Yoshida Masaharu akifurahi na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel wakifurahi pamoja mara baada ya makabidhiano ya Soko la Samaki la Kimataifa lililopo kijiji cha Kasenda Kata ya Mganza Wilaya ya Chato.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Chato Bw;Joel Hari na Balozi wa Japan Nchini Tanzania Mheshimiwa Yoshida Masaharu wakisaini mkataba wa ukarabati wa barabara ya Mganza hadi Kasenda Kilometa 1 huku wakishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya ya Chato.
Mradi wa ujenzi wa Soko la kimataifa la Samaki la Kijiji cha Kasenda Wilayani Chato.
Balozi wa Japani nchini Tanzania, Yoshida Masaharu (wa nne kutoka kushoto) akiwa na Viongozi wa Mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato mara baada ya makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa Soko la Samaki la Kimataifa la Kasenda Wilayani Chato wakiwa katika picha ya pamoja.

Na Magesa Jumapili, Geita RS

Serikali ya watu wa Japan imekabidhi mradi wa Soko la Samaki la kimataifa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chato wenye thamani ya shilingi milioni 320 na kusaini makubaliano ya ukarabati wa barabara ya Mganza - Kasenda.

Akizungumza baada ya kukabidhi mradi huo kwa Serikali Balozi wa Japani nchini Tanzania, Yoshida Masaharu amesema mradi huo umetolewa na Serikali ya Japan kwa watu wa Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa urafiki wa siku nyingi katika utekelezaji wa miradi ya kilimo na uvuvi.

 ''Mradi wa huu ulitolewa baada ya kuona soko la Kasenda liko katika hali mbaya na samaki kuharibika kwa kukosa miundombinu ya kuhifadhi ndipo Japan ikachukua hatua za haraka kwa kutoa fedha dola za kimarekani 148,146 kwa ajili ya kujenga soko na kukarabati soko la zamani''. Utekelezaji wa mradi ulianza mwaka 2017 na sasa wananchi wanaendelea kunufaika.

Awali akisoma taarifa ya mradi huo kabla ya makabidhiano mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato Joel Hari amesema mradi unahusisha ujenzi wa ghala kubwa la kuhifadhia samaki na ukarabati wa sokola zamani.

Ameeleza kuwa soko lipo chini ya Halmashauri ya Chato likiwa na wanachama 241 huku likikasimiwa kukusanya shilingi milioni 140 kwa mwaka huku likitoa huduma kwa nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Congo DRC.

Kwa upande mwingine Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amemshukuru balozi wa Japan nchini kwa miradi hiyo na kumwomba kuangalia na Wilaya zingine za Mkoa wa Geita ili nazo zinufaike na miradi ya namna hiyo. 

Aidha, ameutaka uongozi wa soko kwa kushirikiana na Halmashauri ya Chato kuhakikisha malengo yote yaliyokusudiwa kwa mradi huo yanatekelezeka na kuleta faida ili watu wote wanaofanya kazi katika soko hilo waongeze kipato kwa kuwa kazi ya Serikali ya awamu ya tano ni kujenga miundombinu bora na kuweka mazingira wezeshi ya kusaidia kuendesha biashara.

Mhandisi Robert Gabriel ameahidi kuangalia namna ya kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga vibanda vya pembeni mwa soko ili kuwe na mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: