Na Bashir Yakub.
+255784482959.

1 . SERIKALI ZA MITAA KUCHUKUA ASILIMIA KUMI WAKATI WA MANUNUZI YA KIWANJA/NYUMBA

Watu wanauziana kiwanja au nyumba, serikali za mitaa wanawaambia kuwa mnatakiwa kulipa asilimia kumi kama ada ya mauziano .

Asilimia kumi ni hela nyingi sana kwakuwa kama nyumba imeuzwa milioni 400 asilimia kumi ni sawa na milioni 40.

Zipo serikali za mitaa nyingine ambazo wakati mwingine hudai chini ya hizo lakini mara kwa mara asilimia 10 ndio huwa inaombwa. Kinachouma zaidi hawa jamaa wa serikali za mitaa huwa wanalazimisha kutolewa kwa fedha hizo.

Hufikia hadi hatua ya kutoa vitisho na ikitokea kuwa mtu ameuza bila kuwa taarifu ili wachukue hela basi wanamjengea uadui na hata yule aliyenunua naye anajengewa uadui.

2 .ASILIMIA KUMI YA SERIKALI ZA MITAA HAIPO KISHERIA.

Hakuna sheria yoyote katika nchi hii ambayo inatambua hiyo asilimia kumi. Hili ni jambo la kuzuka tu na limeanzishwa kwa matamanio(tamaa) ya watu.

Narudia tena hakuna katika sheria yoyote ya nchi hii inayosema kuwa watu wanapouziana kiwanja au nymba inatakiwa muuzaji au mnunuzi alipe asilimia kumi serikali za mitaa.Ni mradi wa watu tu ambao wameamua kujipatia kipato kwa njia hiyo.

Natoa changamoto( challenge) ukimuona kiongozi yoyote wa serikali za mitaa kwa nia njema tu muulize asilimia kumi wanayotoza au gharama yoyote ile wanayotoza wakati wa mauzo ya viwanja na nyumba inapatikana katika sheria ipi.

Niseme tu kuwa Sura ya 113, sheria namba 4 ya ardhi pamoja na sura ya 334 sheria ya usajili wa ardhi zinachosisitiza ni kuwa mkataba wa ununuzi wa ardhi ni lazima uwe katika maandishi.

Sambamba na sheria hizo, kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba kimesema mkataba unaokubalika kisheria ni ule uliofanywa kwa hiari huru,wahusika wenye sifa, malipo halali na mali halali.
Sheria hizi ndizo zinazosimamia mauzo ya ardhi.

Hakuna asilimia 10 humu pote. Pia humu pote hamna mahali kuwa usipolipa asilimia 10 ununuzi wako sio halali. Hakuna kabisa .

Kadhalika hakuna sheria nyingine yoyote nje ya nilizotaja hapa juu imeruhusu jambo hilo.

3 . JE IPI HADHI YA ASILIMIA KUMI ?.

Jibu ni rahisi kuwa asilimia kumi au malipo yoyote unayoyatoa serikali za mitaa wakati wa ununuzi wa nyumba/kiwanja ni kama rushwa na ulaghai.

Ifahamike wazi kuwa viongozi wa serikali za mitaa ni watumishi wa serikali. Fedha yoyote ambayo hulipwa serikalini ni lazima iwe imeainishwa katika sheria fulani.

Hakuna malipo yoyote kwa serikali ambayo hutolewa bila ya kuwa yameainishwa katika sheria.

Pili, fedha yoyote halali inayolipwa kihalali katika mamlaka yoyote ya serikali ni lazima itolewe risiti ya serikali. Inatolewa risiti ya serikali ikiwa na rmaana kuwa inatambuliwa na serikali , itakwenda serikalini,na matumizi yake yatakaguliwa na serikali.

Fedha yoyote inayotolewa kwa serikali bila aliyetoa kupewa risiti ni fedha ambayo ina ufisadi ndani yake.

Na katika maana hiyo ni kuwa unapolipa fedha serikali za mitaa bila risiti kwasababu ya kufanyika kwa mkataba wa manunuzi ya kiwanja/nyumba unakuwa umeshiriki katika ufisadi.

Wakati mwingine ukipata bahati kupewa risiti haitakuwa EFD bali zile za vitabu vyao vya kutengeza.Lakini si mnajua sasa hivi risiti ni EFD. Yaa, asikwandikie zile za makondakta za kuchana kwenye vidaftari. Kama atasema risiti ipo akupe EFD na itoke kwenye mashine unaona.

4 . UWEPO WA SERIKALI ZA MITAA UNAPONUNUA ARDHI.

Kisheria unaponunua kiwanja au nyumba pahala fulani suala la kuwashirikisha serikali za mitaa ni la hiari.

Katu kisheria mkataba wa ununuzi haubatiliki kwakuwa hakukuwa na serikali za mitaa.

Serikali za mitaa tunawahitaji kwa ajili ya kuainisha mipaka, kujua tu ikiwa eneo lina mgogoro, na pengine historia ya eneo, na hapo ni kama huijui au unapenda tu kujiridhisha.

Hata hivyo zingatia kuwa hizi dili za kuuziwa kiwanja mara mbili nk nao wamekuwa wakizicheza wakati mwingine.

Kwahiyo wewe utaamua uwashirikishe au usiwashirikishe.

Narudia tena mkataba wa ununuzi wa ardhi kisheria haubatiliki ati kwasababu serikali za mitaa hawakushirikishwa.

Basi yafaa tuyafahamu hayo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: