Na Fredy Mgunda, Iringa.

MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahamud Mgimwa amemwokoa mtoto wa kike ambaye ni mlemavu wa viungo kwa kumpeleka shule baada ya wazazi wake kushindwa gharama za masomo.

Mtoto huyo Rosemary Lutego ambaye ana umri wa miaka 15 alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule yawasichana Iringa lakini alishindwa gharama za masomo na matumizi shuleni baada ya wazazi wake kukimbia jukumu la kumpeleka shule.


Mbunge Mgimwa baada ya kugundua changamoto inayomkabili binti huyo licha ya kufaulu na kushindwa kujiunga na wenzake kuanza masomo ya kidato cha kwanza ndipo alipoamua kumsomesha katika shule maalum ya Wasichana Iringa ambayo ni mchanganyiko.


Mwanafunzi huyo alijulikana kama yuko nyumbani baada ya ziara ya kikazi aliyofanya mbunge Mahamud Mgimwa katika kata mbalimbali na kubaini uwepo wa mwanafunzi ambaye alikosa vifaa mbalimbali vya shule na kuamua kuchukua jukumu la kumsomesha hadi anamaliza shule.

Mara baada ya kupata taarifa za mwanafunzi huyo,Mgimwa alizungumza na wazazi na walimu katika shule ya Msingi Ikweha na kuwataka uongozi wa kijiji cha Ikweha kuwatafuta wazazi hao na kuwapeleka katika vyombo vya sheria huku akichukua jukumu la kumnunulia vifaa vyote vinavyohitajika shuleni hapo.


Aidha aliwataka wazazi wote ambayo wana tabia ya kuwazuia watoto waliofaulu kujitokeza haraka kabla ya msako kuanza popote pale katika jimbo la Mufundi Kaskazini ambapo wawapeleke shule kutokana na sasa hakuna ada wala mchango katika shule za serikali.

Aidha aliwataka wazazi kuacha tabia ya kuwafundisha watoto wao tabia ya kujifelisha katika mitihani ili waweza kuolewa wakati uwezo wa kufaulu upo kwa mtoto husika.

Akizungumza mara baada ya kupata msaada huo mtoto Rosemary Lutego alisema kuwa ndoto yake ya kupata elimu na kuweza kuja kuwasaidia wazazi wakeimeanza kupata mwanga kwani alidhani ndoto zake zimeishia darasa la saba.

alimshukuru sana mbunge Mgimwa msaada huo mkubwa wa kufanikisha masomo yake kwani itakuwa mfano mkubwa wa wazazi wengine ambayo hawataki mtoto wa kike aende shule.

Aliongeza kuwa wazazi wake walimwambia kuwa wanaenda kutafuta fedha za kununulia vifaa lakini hadi sasa hawakuweza kufanikisha hali iliyomlazimu abaki nyumbani wakati wanafunzi wengine wakiendelea na masomo.

"Namshukuru sana mbunge kwa kusikia na kuamua kugharamia masomo yangu ya sekondari nitahakikisha nasoma kwa bidii licha ya ulemavu wangu ili kuweza kuikomboa familia yangu katika umaskini." alisema.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: