Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeifukuzia mbali kesi ya madai iliyofunguliwa na Dk.William Morris raia wa Marekani dhidi ya mke wake Dk. Phills Nyimbi na Mchungaji Josephat Mwingira kwa garama.

Dk.William Morris aliwasilisha maombi mahakamani hapo, akiomba, mkewe, Mwingira na mtoto wake (9) wafanyiwe kipimo cha DNA.

Katika Maombi hayo Dk. Morris ambae ni mume wa (mdaiwa wa Pili, Philis Nyimbi) anaiomba Mahakama itoe amri ya mkewe Mwingira na mtoto wakafanyiwe kipimo hicho cha DNA.

Lengo ni kujua wazazi halisi wa mtoto aliyezaa na mkewe.
Katika madai yake, Dkt. Morris anadai mchungaji Mwingira alizini na mkewe na hatimaye kuzaa naye mtoto wa kiume( 9).

Mapema mahakamani hapo,

akisoma hukumu hiyo leo February 26 mwaka huu, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema Dk.Morris katika kesi hiyo ameshindwa kuonesha mahusiano ya kimapenzi  kati ya Dk.Phills na Mchungaji Mwingira.

Pia ameshindwa kuthibitisha kuwa mtoto aliyezaliwa na mke wa Dk. Morris ni matokeo ya  mahusiano ya kimapenzi kati ya Dk.Phills na Mchungaji Mwingira.

Hivyo mahakama imeifukuzia mbali kesi hiyo ya madai na kueleza mdai ameshindwa kuthibitisha madai yake katika kiwango kinachotakiwa katika mashauri ya madai na alipe gharama.

"Si tu ameshindwa moja kwa moja lakini ameshindwa kiasi ambacho Mahakama hii inalazimika kutoa amri kuwa alipe garama walizotumia wadaiwa kwenye shauri hili" amesoma Hakimu Simba.

Baada ya kutolewa kwa hukumu huyo Wakili wa mdai, Respicius Ishengoma amesema hawajaridhika na uamuzi huo na watakata rufaa.

Hukumu hiyo iliyoandaliwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini imesomwa leo nyakati za saa 8 mchana.

Awali kwenye utetezi wa Dk.Phills Nyimbi aliieleza Mahakama hiyo hajawahi kuwa na uhusiano na Mchungaji Josephat Mwingira.

Akiongozwa na Wakili Peter Swai kutoa  ushahidi katika kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa mumewe ambaye ni raia wa Marekani, Dk. William Morris, Dk.Nyimbi aliomba mwanaume huyo asilipwe kiasi cha fedha cha Sh.bilioni 7.5 anazodai kwa sababu yeye hakuwa na mahusiano na Mchungaji Mwingira.

Dk. Nyimbi kupitia Wakili wake Swai aliomba Dk.Morris asilipwe kiasi hicho cha fedha kwa sababu yeye hajawahi kuwa na mahusiano na Mchungaji Mwingira  na kwamba  hicho anachokidai si madai halali.

Wakili Swai alimuuliza Dk. Nyimbi anasemaje kuhusu madai ya mumewe Dk.Morris, kuwa wewe na yeye mkapimwe HIV.

Dk Nyimbi alidai yeye mwenyewe huwa ana utaratibu wa kupima na kwa bahati nzuri  sheria za Tanzania zinaruhusu.

Swai alimueleza Dk.Phillips kuwa mumewe Dk.Morris anataka mtoto wake akapime vinasaba (DNA).

Dk Phillips alidai mtoto huyo ni wa kwake yeye, Dk.Phillis na hajasema ni wa Dk.Morris  wala wa Mchungaji Mwingira.

Pia ameiomba Mahakama iamiru gharama za kesi zilipwe na Dk Morris.

Dk Nyimbi  alisisitiza kukana  kuzaa na Mchungaji Mwingira na kwamba Mchungaji huyo wala hajawahi kuujua mwili wake.

Dk.Nyimbi alitoa utetezi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mhini.

Alidai kuwa  alifunga ndoa na Dk.Morris mwaka 2001 katika Kanisa la Mtakatifu Albano.

Alieleza baada ya ndoa walikaa mapumziko kwa siku tatu katika Hoteli ya Starlight kisha wakahamia Muhimbili ambako alikuwa anaishi katika chumba kimoja akiwa katika mafunzo ya vitendo.

Alidai kuwa baada ya miezi mitatu Dk.Morris  alikwenda Marekani na mawasiliano kati yao yalikuwa ya shida shida.

Alidai kutokana na hali hiyo alichanganyikiwa kwa kuwa madaktari wenzake walikuwa wakimuuliza  anaondoka lini na kwamba alikuwa  akilia tu.

Alidai alijaribu kwenda katika  Ubalozi wa Marekani mara mbili kutafuta hati ya kusafiria lakini ilishindikana, hivyo akaamua kuendelea kusoma ili asije akakosa  vyote.

Alidai Dk.Morris baada ya miaka minane  alikuja Tanzania Aprili 25, mwaka 2009  baada ya kupata taarifa anakuja alikwenda  kumpokea katika uwanja wa ndege wa KIA.

Alidai baada ya kumpokea walilala katika  hoteli iliyopo Moshi ambapo usiku huo alimuelezea historia ya maisha yake, kwa muda mrefu, aliomuacha.

Alimueleza kuwa anamaisha yake na amezaa mtoto ambaye ana umri wa mwaka mmoja. Alimueleza alimuoa akiwa na miaka 30 hivyo amezaa akiwa na miaka 38.

Alidai alimueleza alimsukuma kitandani. Alieleza Dk Nyimbi.

Dk. Nyimbi alidai waliporudi nyumbani kwao Kibaha mkoani Pwani alimwambia kwamba mtoto huyo wa kiume kazaa na mfanyabiashara ambaye yuko nje ya nchi anaitwa Baraka.

Alidai Dk.Morris alisema ana kuna ili mtoto huyo atakuwa wake kwa sababu anampenda mkewe lakini siku zilivyokuwa zikienda mumewe alimwambia kwamba mtoto huyo kazaa na Nabii Mwingira.

"Aliniambia naitwa Polisi Kibaha nikatoe maelezo kuhusiana na mtoto, nilikataa, nikapigiwa simu na Polisi Kibaha ndipo nilipoamua kwenda, niliambiwa kwamba mu

mewe wangu kalalamika kuwa  nimebakwa na Nabii Mwingira na nimezaa naye mtoto." Alieleza Dk. Nyimbi.
Alidai alipoulizwa na Polisi alikataa hakuna jambo kama hilo na hajawahi kubakwa wala kuzaa na Mchungaji Mwingira.

Kwa upande wa Mchungaji Mwingira naye alikana kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Dk.Phills.

Katika kesi hiyo, Dk.Morris ambaye ni raia wa Marekani pamoja na mambo mengine anaiomba Mahakama hiyo imuamuru Mwingira kulipa Sh 7.5 bilioni  kama fidia  ya kuzini na kuwa na mahusiano na mke wake huyo.

Pia anaomba itoe amari ya kwenda kupima Ukimwi  kwa yeye, Mchungaji Mwingira na mkewe Phillis na ifanyike kipimo cha DNA  kati ya mtoto  na walalamikiwa hao.

Inadaiwa Mwingira na Phillis waliingia katika mahusiano muda usiojulikana bila ya kujali kuwa Phills alikuwa ni mke wa Morris na kwamba mara baada ya Morris kufanya uchunguzi  juu ya mahusiano hayo mke wake alidai kwamba yeye alibakwa na Mchungaji Mwingira.

Iliendelea kudaiwa kuwa kubakwa huko  kulipelekea  siyo tu mke wake  kuwa na ujauzito pia kulisababisha  kuwa na matatizo ya afya.

Desemba 28,mwaka 2011 Morris na Phills  walifunga  ndoa  ya Kanisani  na wakati wa mahusiano yao, Phillis na Mchungaji Mwingira wanadaiwa  kuingia katika mahusiano ya kimapenzi.

Na kubahatika kupata  mtoto wa kiume ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 9.

Mlalamikaji huyo anadai alitoa taarifa katika kituo cha polisi  Kibamba  ambapo walimueleza  suala hilo  ni la uzinzi  ama udhalilishaji  na haliwezi kuwa la kijinai na kushauriwa kufungua  kesi ya madai.

Kitendo cha mke wake kuwa na mahusiano na Mwingira  ni kwenda kinyume  na ndoa yao halali  na kwamba kitendo hicho  kimeharibu mipango yake ya mbele  kiasi cha kumfanya  apoteze hata matumaini ya kuendelea kuishi.

Pia kimemuaibisha na kushusha hadi yake siyo tu Tanzania  na Duniani hivyo  kumsababisha ateseke kiakili na kiuchumi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: