Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (kulia) leo hii amemtembelea Mh. Paul Makonda (kushoto) ofisini kwake Jijini Dar es salaam kwa ajiri ya kutoa pongezi za Wizara ya Katiba na Sheria kwa serikali ya Mkoa wa Dar es salaam kwa kuendesha programu ya msaada wa kisheria kwa wananchi wa Mkoa Dar es salaam na wale wa mikoa jirani waliofika kupatiwa huduma hiyo kuanzia siku ya tarehe Januari 29, 2018 mpaka Februari 3, 2018.

Prof. Mchome amesifu namna ambavyo utaratibu huo ulioanzishwa umeweza kugundua mianya na changamoto mbalimbali ambazo wananchi wanakutana nazo katika utafutwaji wa Haki zao kupitia vyombo vya utoaji haki.

Akizungumzia hilo, alisema: "Kwa kuona idadi kubwa ya wananchi zaidi ya elfu kumi na sita na takribani wananchi 5600 kupata huduma ya msaada wa kisheria inaonyesha wazi kuwa kuna mahali kuna tatizo katika taasisi na mamlaka za utoaji haki. Hii inatupa alarm sisi watendaji tujitathmini na tuone namna gani inatubidi tubadilike."
 "Mimi kama katibu Mkuu wa wizara hii kazi yangu kubwa niliyoelekezwa na ambayo imelekezwa ndani ya ilani ya Chama tawala CCM ni kuhakikisha naboresha mifumo ya kiwizara ili kuleta tija katika kuwahudumia wananchi. Hivyo hata hili unalofanya Mh RC ni jambo ambalo linanisaidia sana katika kutengeneza mifumo itakayo endana na matakwa ya utatuzi wa changamoto za wananchi." aliongeza Prof. Mchome.

Katika mazungumzo hayo Mh Makonda alielezea kwa undani zaidi namna ambavyo Mabaraza ya Ardhi ya kata ndani ya Mkoa wake yalivyokuwa chanzo cha migogoro mingi ya ardhi na uvunjwaji wa amani sehemu mbalimbali.

" karibu 70% ya malalamiko yaliyofika hapa kwangu katika wiki ya msaada wa kisheria yanayagusa mabaraza ya ardhi. Mimi nikaaangalia na nikaona kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa huu siwezi kufumbia macho mambo ambayo yanaenda kinyime na shughuli yangu Kuu ya Kuhakikisha amani na utulivu vinatawala Dar es saalam. Mabaraza haya nimeyaamuru yasimamishe shughuli zao na makatibu tarafa wafanye kazi ya kukusanya mashauri ya mabaraza na wayapeleke katika ngazi za mahakama za wilaya ili yashugulikiwe kikamilifu huko."
Pia Prof. Mchome utakubalina na mimi kuwa hata sheria yenyewe ya mahakama (ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi) "The Courts Land Disputes Settlements" Act, 2002 inatambua kazi ya mabaraza ni kusuluhisha migogoro na kuhakikisha hali ya utulivu. Tofauti na wanachokifanya sasa hivi cha kuamua kesi hadi zilizo juu ya mamlaka yao." aliongeza Makonda.

Katika kuunga mkono uamuzi huo Prof. Mchome naye ameahidi kuwa wizara yake itaielekeza Tume ya Kurekebisha Sheria ishauri namna gani changamoto za Mabaraza ya Kata zinawezwa malizwa mara moja.

Kati ya changamoto ambazo wizara imeziona na inazifanyia kazi ni pamoja na:

i/ Mfumo mzima wa shughuli za mabaraza ya kata kuwa wa kizamani sana na kutoendana na matakwa ya muda wa sasa kwa kiasi kikubwa sana.

ii/ Sheria namba 206,kifungu cha 5(1) (d) kinakataza uwepo wa mtu mwenye sifa za uwanasheria katika baraza hili. Hii inaleta mkanganyiko wa kutafsiri sheria hiyo kwa wajumbe wa baraza hilo ambao wana uelewa mdogo wa sheria mbalimbali".

Prof. Mchome amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ya kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itatoa ushirikiano wa hali na mali katika muendelezo wa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria unaofanywa na Serikali ya Mkoa wa Dar es salaam.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: