JANA, kulikuwa na mjadala humu mitandaoni baada ya Hussein Bashe kutoa taarifa kwamba amepanga kupeleka hoja binafsi bungeni kuhusu hali ya kisiasa na kiusalama hapa nchini.

Taarifa ile haikupokewa vema na viongozi wa upinzani. Baadhi yao walimkejeli, wengine walimbeza na wengine walipingana naye kwa hoja.

Nitachukua mfano wa Julius Mtatiro ambaye aliweka hoja badala ya kutoa mabezo tu. Julius S. Mtatiro alionyesha kwamba Bunge la sasa haliwezi kufanya lolote kubadilisha hali iliyopo.

Ninaelewa mazingira ya hoja ya Bashe na mapokeo kutoka katika kambi ya upinzani. Kabla sijahitimisha, ni vema kwanza nikaweka msingi wa hitimisho langu. Inabidi nirudi nyuma miaka 60 iliyopita.

Tanganyika ilikuwa chini ya Mwingireza na Gavana akiwa Edward Twining. Kwa wasiofahamu, Twining ndiye kizazi cha mwisho cha Waingereza waliokuwa wakiamini kwamba ukoloni ulikuwa ni wajibu mkubwa kwa Waingereza na msaada kwa watawaliwa.

Huyu ni mfuasi wa Rudyard Kipling ambaye shairi lake la "White Man's Burden" lilieleza kuhusu mzigo mkubwa ambao Uingereza inao wa kutawala makoloni yake. Twining alitawala kwa mabavu akiamini kwamba anatusaidia sisi tusiojiweza. Huo ndiyo "msalaba" ambao mtu mweupe alikuwa nao kwa makoloni yake kote duniani! Twining huyo.

Wakati huo, akina Nyerere walikuwa wanatafuta Uhuru na Twining akawa hawaelewi kabisa. Matokeo yake, Nyerere na Twining wakawa chui na paka.

Katikati ya uadui wao, wakakutanishwa na Chifu David Makwaia. Wakakaa chini, Twining akanywa Gin yake huku Mwalimu akipata bia. Wakazungumza. Wakayamaliza hata kama hawakuwahi kuwa marafiki.

Kwenye maelezo yake ya kwanini alikutana na Twining -na hii ndiyo hoja yangu kubwa leo, Nyerere alisema hivi " Mimi naheshimu watu, hata kama napingana na utawala wao". Hoja ya Mwalimu ilikuwa kwamba katika mapambano, kuna umuhimu wa kutenganisha kati ya mfumo na watu binafsi.

Nyerere aliweza kuwa na urafiki na JF Kennedy wa Marekani lakini wakati huohuo alikuwa anapinga ubeberu wa taifa hilo.

Kingine.

Nyerere alikuwa anatumia Land Rover kuzunguka nchi nzima kuhamasisha watu kudai Uhuru. Twining akamuwekea Land Rover iliyojaa askari ya kumfuata nyuma kila aendako wakati.

Mwalimu akatumia akili. Akajenga urafiki na askari wale wa mkoloni (sembuse hawa wa sasa wa Tanzania huru). Wakajenga makubaliano kwamba, kama gari ya TANU ikiharibika, Mwalimu atabanana na askari kwenye gari yao. Kama ya askari ikiharibika, watabanana kwenye gari ya TANU.

Badala ya kuwa maadui, wakawa marafiki.

Halafu kukawa na tukio la Mbeya. Miaka 60 imeshapita sasa. Mwalimu kafika mkoa huo akiwa hana kipaza sauti. Mbeya nzima wakakosa. Wakaenda seminarini kuomba, wakanyimwa.

Akaenda Polisi kuomba vile vipaza sauti vyao. Inspekta mmoja mzungu akakubali kumpa Mwalimu na mkutano ukafanyika. Kwenye mkutano ule, Nyerere akatamka, " Adui yetu si mtu mweupe, ni ukoloni". Maana kama adui angekuwa mzungu, yule inspekta asingewapa kipaza sauti.

Hoja yangu hapa ni kwamba, kama upinzani unataka kufanikiwa katika mapambano yake, unatakiwa kuweka tofauti kati ya watu binafsi na mfumo. Wahenga wana msemo, kuwa na marafiki zako karibu, lakini kuwa na adui zako karibu zaidi".

Vinara wa upinzani wanatakiwa kupunguza mapambano na watu binafsi na badala yake wapambane na mfumo. Haina haja ya leo kugombana na Bashe, kesho Kibajaji, keshokutwa Nkamia, mtondogoo Polepole etc. Hawa ni watu ambao inawezekana wakatumiwa na upinzani kuharakisha wanachokitaka.

Kama TANU ingekataa kushirikiana na waasia na wazungu kwenye uchaguzi wa kura tatu miaka 60 iliyopita, Tanganyika ingepata Uhuru wake pengine mwaka 70 au 75. Lakini kwa kukubali kushirikiana na wengine, Uhuru ukaja mapema zaidi.

Kama hoja ya Bashe ina mashiko, hata kama inaonekana mfumo hautaikubali, anatakiwa aungwe mkono na si kupendwa. Na hii ni kwa sababu iko siku wapinzani watahitaji kuungwa mkono na Bashe kwenye jambo lao.

Namna ya kuubomoa mfumo ni kupata ushindi mdogo mdogo hapa na pale, kutengeneza uhusiano na kuaminiana. Kuchora mstari kati ya "sisi na wao" hakujawahi kusaidia kuleta mabadiliko.

Pambana na mfumo, achana na watu binafsi. Tengeneza marafiki, usizalishe maadui. Hii ndiyo njia ya kwenda mbele.

Ezekiel Kamwaga
Dar es Salaam
07/03/2018
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: