Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na msanii wa muziki Ney Wamitengo kuhusu namna ya kuboresha na kufuata maadili ya mtanzania katika kazi ya sanaa anayoifanya leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza.
Afisa Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Rolf Kibaja akizungumza wakati wa kikao cha Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na msanii wa muziki Ney Wamitengo kuhusu namna ya kuboresha na kufuata maadili ya mtanzania katika kazi ya sanaa anayoifanya leo Jijini Dar es Salaam.
Katibu Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza (kulia) akifafanua jambo wakati wa kikao cha Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (kushoto) kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na msanii wa muziki Ney Wamitengo kuhusu namna ya kuboresha na kufuata maadili ya mtanzania katika kazi ya sanaa anayoifanya leo Jijini Dar es Salaam.
Msanii wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki (Ney Wamitego) (kulia) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao cha Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza (kushoto) kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo naye kuhusu namna ya kuboresha na kufuata maadili ya mtanzania katika kazi ya sanaa anayoifanya leo Jijini Dar es Salaam.

Na Genofeva Matemu – WHUSM.

Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza amemfungia msanii wa muziki wa kizazi kipya Ibrahim Musa (Roma Mkatoliki) kutofanya kazi yoyote ya sanaa ikiwemo kutokufanya maonyesho ya sanaa ya majukwaa kwa kipindi cha miezi sita na kumtaka Msanii Emmanueli Elibariki (Ney Wamitego) kuacha kutumia maneno yenye utata yanayolenga kuleta mmomonyoko wa maadili ya mtanzania anapoandaa nyimbo zake.

Mhe. Shonza ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam baada ya msanii Roma Mkatoliki kuitwa na BASATA mwaka jana na kukubaliana kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika wimbo wake wa kibamia lakini hadi sasa msanii huyo kukiuka makubaliano hayo na kukiuka agizo la Naibu Waziri la kumtaka kufika ofisini kwake leo kwa ajili ya kufanya mazungumzo yanayolenga kuwekana sawa katika uandaaji wa kazi za sanaa.

“Kwa upande wa msanii Roma Mkatoriki aliyeimba wimbo wa kibamia ambaye ameshaitwa na BASATA kufanyia marekebisho ya wimbo huo na kukubali kufanyia marekebisho kasoro zilizopo lakini hadi sasa hakuna marekebisho yoyote yaliyofanyika na kibaya zaidi wimbo huo unaendelea kupingwa kwenye vyombo vya habari; natangaza kuwa namfungia msanii Roma Mkatoliki kwa kipindi cha miezi sita haruhusiwi kufanya kazi yoyote ya sanaa lakini pia hakuna kufanya maonyesho yoyote ya sanaa kwenye majukwaa kwa kipindi hicho cha miezi sita” amesema Mhe. Shonza

Aidha Mhe. Shonza amesema kuwa japo serikali inatambua kuwa sanaa ni ajira, lakini ajira hii imekua ikitumika vibaya kwa kuharibu maadili ya mtanzania kulingana na maneno yanayotumika sambamba na kuwa na mavazi ya uchi katika picha jongevu hivyo kudhalilisha utu hasa kwa mwanawake.

“Msanii Ney wa Mitego tumemuonya kutokana na nyimbo anazozitoa kutumia maneno yenye utata na wakati mwingine kuwa na picha jongevu zinazodhalilisha utu wa mtu na kukubaliana nasi kuwa atabadilika na kuzingatia maadili ya mtanzania kwa kazi zake za mbeleni” amesema Mhe. Shonza

Hali kadharika Mhe. Shonza ameitaka BASATA kuanzia sasa inapotokea kuwa wimbo unatolewa na msanii yeyote na unakiua maadili ya mtanzania wimbo huo uchukuliwe hatua kwa haraka bila kupoteza muda katika kuhakikisha kwamba sanaa kama msingi muhimu wa kuburudisha na kuelimisha inazingatia miiko na maadili yaliyowekwa na vyombo vinavyosimamia sekta ya sanaa

Kwa upande wake Afisa Utangazani kutoka Mamlaka ya Mawasiliano ya Tanzania (TCRA) Bw. Rolf Kibaja ametoa rai kwa vituo vyote vya utangazaji nchini kuzingatia kanuni za utangazaji kwasababu vituo hivyo vinapopewa leseni hupewa na sheria na kanuni za uendeshaji wa vituo hivyo; hivo kuwataka waandaaji na wasimamizi wa vipindi kuzingatia kanuni hizo kwani Mamlaka ya mawasiliano imejipanga kuhakikisha kuwa nyimbo zote zitakazokua zinaenda kinyume na maadili zitachukulia hatua kwa mujibu wa sheria kanunu na taratibu zilizopo.

Naye Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza amesema kuwa Baraza halina budi kutumia kanuni na sheria zilizopo kuwajibisha kazi za sanaa ambazo zinaathiri jamii ya kitanzania kimaadili na kuwataka wasanii kufuata misingi imara ya kuelimisha na kuburudisha kuliko kuleta athari katika jamii hasa kwa kizazi cha leo na cha kesho.

Sanjari Msanii Ney Wamitego ameishukuru wizara inayosimamia sekta ya sanaa kwa kumweka sawa na kumpa nafasi nyingine yakuweza kujirekebisha katika kazi zake za sanaa na kuahidi kufanya mazuri mengi ambayo yatakuwa tofauti na aliyowahi kufanya awali.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: