Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TaESA Boniface Chandaruba akiongea na wanahabari (waliopo picha ya chini).
Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano aliyouandaa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TaESA Boniface Chandaruba katika kufafanua  mambo mbali mbali kuhusu ajira.

*Ni kwa ajili ya kupata kazi kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta Tanzania-Uganda

Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

WAKALA wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) umetangaza kuanza kwa mchakato wa utambuzi wa Watanzania wenye taaluma na ujuzi katika sekta ya mafuta na gesi ambapo mwisho wa usajili ni Machi 30 mwaka huu.

Mchakato wa utambuzi huo ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga nchini.

Akizungumza Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Boniface Chandaruba amesema kuwa ili kuhakikisha Watanzania wengi wananuifaka na fursa za ajira zitokanazo na mradi wa bomba la mafuta TaESA imepewa jukumu la kuhamasisha wote wenye taaluma na ujuzi nchini katika sekta ya mafuta na gesi wajitokeze.

“Hivyo tunaomba Watanzania wenye sifa kuja kujisajili TaESA ili waweze kuingizwa kwenye kanzidata ya Wakala kwa lengo la kuiwezesha Serikali kubaini idadi halisi ya walio na sifa zinazohitajika na walio tayari kuajiriwa kwenye mradi wa ujenzi wa bomba hilo.

“Usajili huu unafanyika bure, hivyo tunasisitiza hakuna gharama yoyote itakayotozwa kwa Mtanzania yeyote atakayehitaji kusajiliwa. Maelezo ya kina kuhusu aina ya fursa za ajira zinazotegemewa kutolewa yanapatikana katika tovuti ya Wakala ya www.taesa.go.tz,” amesema .

Chandaruba amesema mchakato wa usajili unafanyika kwa kujaza fomu maalum ambazo zinapatikana kupitia tovuti ya Wakala au kwa kufika kwenye ofisi zao za kanda zilizopo Dar es Salaam,Arusha, Dodoma na Mwanza.Pia amesema fumu hizo zinapatikana kwa barua pepe eacop@taesa.go.tz na kwamba mchakato wa usajili unatarajia kumalizika Machi 30 mwaka huu.

Ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia Watanzania wote kuwa watumishi wa TaESA ni wanazingatia maadili ,hivyo hakuna rushwa ya aina yoyote kwa mtanzania ambaye anataka kujisajili.Kuhusu idadi ya ajira ambazo zitapatikana kwenye mradi huo, Chandaruba amesema unategemewa kuzalisha ajira 10,000 wakati wa ujenzi na ajira zaidi ya 1000 wakati wa uendeshaji wake.

Amesema kuwa mradi wa ujenzi wa bomba hilo la kusafirisha mafuta ni moja ya mradi mkubwa kutekelezwa hapa nchini na unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 3.5 sawa na Sh.trilioni 8.“Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,445 ambapo ujenzi wa kilometa 1,115 za bomba utafanyika nhini Tanzania.Jumla ya Wilaya 24 na vijiji 184 hapa nchini vinategemewa kupitiwa na bomba hilo katika mikoa nane,” amesema.

Ametaja mikoa hiyo ni Kagera, Geita, Shinyanga,Tabora,Singida,Dodoma,Manyara na Tanga.Amefafanua licha ya bomba kupita kwenye maeneo hayo lakini ajira zitatolewa kwa Watanzania kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Alipoulizwa kama ndio wanatangaza sasa au walishatangaza siku za nyuma kuhusu watanzania kujisajili , amejibu kuwa ujenzi wa bomba hilo umekuwa ukizungumzwa kwa nyakati tofauti na hivyo kila eneo limekuwa likitangaza, lakini wao ambao ndio wakala wa ajira nao wanayo nafasi ya kuufahamisha umma.

Hivyo siku 16 ambazo zimebaki zinatosha watu kujisajili hasa kwa kuzingatia teknolokia ya habari na mawasiliano imerahisisha na kufafanua tayari wananchi walishaanza kujaza fomu na kuzipeleka kwenye wilaya na mikoa na sasa wanaotuma maombi hayo watajua wenye jukumu hilo ni TaESA.

Kuhusu TaESA amesema walianza kutoa huduma mwaka 2008 ambapo moja ya majukumu yake ni kukusanya,kuchambua na kusambaza taarifa za soko la ajira, pia kuendesha mafunzo kwa watafuta kazi ili kuwajengea uwezo na mbinu za kutafuta kazi na kuajirika.

Amezungumzia changamoto ya soko la ajira duniani, na kutumia nafasi hiyo kuwashauri wasomi nchini kuwa kutumia elimu ambayo wameipata kujiajiri na hatimaye nao kutoa ajira kwa wengine na kuongeza jukumu la Serikali ni kuandaa mazingira mazuri ya kuwawezesha Watanzania kujiajiri.

Amesema kwa mwaka idadi ya wasomi wanaohitimi vyuo vikuu ni 600,000, hivyo kwa idadi hiyo unaweza kuona soko la ajira serikali halitoshi, hivyo ni vema jamii ikaanza kubadili fikra kwa kutambua badala ya kusubiri ajira serikalini wakatumia elimu wanayoipata kujiajiri.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: