Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dk. Inmi Patterson alikabidhi rasmi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) magari matatu aina ya Toyota Land Cruiser kama sehemu ya programu ya Serikali ya Marekani ya Mafunzo na Kujenga Uwezo wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Usafirishaji Wanyamapori.

Kukabidhiwa kwa magari haya TAWA kunaongeza uwezo wa askari wake wa wanyamapori kufanya doria za kuzuia ujangili katika mapori ya akiba ya Rungwa/Kizigo/Muhesi na kuthibitisha ushirikiano endelevu na imara kati ya Marekani na Tanzania. Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Kaimu Balozi Patterson alisema kuwa, “kwa ushirikiano wa dhati kati ya serikali, raia wake, wabia wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi, tunaweza kulikabili na kulitokomeza janga hili la ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori.”

Serikali ya Marekani ni mbia mwenye fahari katika jitihada za Tanzania za kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori, ambapo imekuwa ikitoa mafunzo, vifaa na kufadhili shughuli za kujenga uwezo (capacity building) ili kuongeza uwezo wa askari wanyamapori kudhibiti ujangili katika mapori ya akiba ya Rungwa, Kizigo naMuhesi.

 Miradi inayofadhiliwa hivi sasa na serikali ya Marekani ni pamoja na ule wa kuweka mfumo wa Mawasiliano ya simu, ukarabati wa vituo viwili vya askari wanyamapori na kuweka daraja maalumu la kamba kuwezesha kuvuka mto katika kipindi chote cha mwaka kuelekea mashariki mwa hifadhi. “Mafanikio yaliyopatikana hivi karibuni yanatupa matumaini,” alisema Kaimu Balozi Patterson, “hata hivyo bado vita dhidi ya ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori haijamalizika. Serikali ya Marekani ina fahari kusimama pamoja nanyi katika vita hii.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: