Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Bw. Makwaia Makani akizungumza kwenye tafrija ya kuwaaga wachezaji wa Timu ya Michezo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), timu ya Wizara ya Afya Zanzibar, Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) baada ya timu hizo kushiriki tamasha la Michezo ya Pasaka 2018.
Baadhi ya wachezaji na wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakimsikiliza Mkurugezi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Bw. Makani wakati akizungumza nao.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Utafiti- Zanzibar, Hamisi Rashidi Mohamed akizungumza kwenye tafrija ya kuwaaga wachezaji wa timu ya Wizara ya Afya Zanzibar na Timu ya Michezo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Bw. Makwaia Makani na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Utafiti- Zanzibar, Hamisi Rashidi Mohamed akiwa kwenye picha ya pamoja na wachezaji wa timu hizo baada ya kumalizika kwa tafrija hiyo.

Na Mwandishi Wetu.

Serikali imesema itaendelea kuboresha michezo sehemu za kazi ili kuifanya iwe endelevu na kuwawezesha watumishi wengi kushiriki.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu-Kitengo cha Utafiti Zanzibar, Hamisi Rashid Mohamed wakati alipokua akizungumza katika hafla ya kufunga tamasha la michezo ya Pasaka 2018, iliyoshirikisha timu za michezo kutoka Wizara ya afya Zanzibar, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) , Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Amesema michezo hiyo ni ya muda mrefu ilianzishwa mwaka 1972 na kwamba hakuna budi kuindeleza na kuiboresha zaidi ili kuleta hamasa kwa wanamichezo wa taasisi hizo kushiriki kwa wingi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Bw. Makwaia Makani ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru amesema ushiriki wa michezo ni jambo zuri kwani inawaepusha vijana kujiingiza kwenye mambo yasiyofaa.

Amesisitiza mipango iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni kuhakikisha michezo hiyo inaboreshwa na kutoa fursa kwa watumishi wengi kushiriki.

‘’Hospitali ya Taifa Muhimbili inaipa kipaumbele michezo na nina ahidi kwamba mapungufu yote yaliyopo tutayafanyia kazi kikamilifu na michezo hii tutaendelea kuiboresha,’’ amesema Mkurugenzi Makani.

Tamasha la michezo ya Pasaka lilianza Machi 30, 2018 na kumalizika Aprili 2 , 2018 likihusisha mchezo wa mpira wa miguu ,pete pamoja na kuvuta kamba .

Tamasha hilo mwakani litafanyika Visiwani Zanzibar.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: