Kikosi cha Timu ya Yanga
Kikosi cha Timu ya Simba
Simba wameibuka washindi kwenye mechi dhidi ya mahasimu wao Yanga sasa unawafanya Wekundu Wa Msimbazi kuhitaji pointi 5 kutawazwa mabingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Shabiki wa Yanga akiwa ahamini kilichotokea
VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wamezidi kuukaribia ubingwa baada ya leo kuibuka na pointi zote tatu kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Bao hilo pekee lililoifanya Simba kuzidi kuukaribia ubingwa ambao kwa mara ya mwisho waliutwaa katika msimu wa mwaka 2011-12, lilifungwa na Erasto Nyoni katika dakika ya 37 kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Shiza Kichuya na kuparazwa na Rafael Daud na kumkuta mfungaji.

Yanga walijikuta wakicheza pungufu baada ya mchezaji wake Hassan Kessy kutolewa baada ya kupewa kadi ya pili ya njano kutokana na kumchezea vibaya Asante Kwasi katika dakika ya 48.
Pamoja na kucheza pungufu, lakini Simba walishindwa kutumia nafasi hiyo kupata bao jingine na badala yake kila dakika zilipotokomea, waliendelea kucheza kwa kujihami zaidi na kurudi nyuma.
Hata hivyo, Simba ndio walitawala zaidi mchezo huo, ambapo walipata jumla ya kona nane wakati watani zao Yanga hawakupata kona yoyote huku Yanga wakiwa nakadi mbili za njano wakati Simba moja na washindi walipiga mashuti matano yaliyolenga bao wakati Yanga mawili tu.

Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 62 na sasa kuhitaji pointi sita tu ili kujihakikishia ubingwa kwani Yanga akishinda mechi zake zote sita zilizobaki atafikisha pointi 66 tu, ambazo zitakuwa zimepitwa na Wekundu wa Msimbazi.

Baada ya kipigo hicho, Yanga wanaendelea kuwa katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi zao 48 wakiwa pointi moja nyuma ya Azam FC, ambayo iko katika nafasi ya pili licha ya kucheza mechi 26 wakati Yanga wamecheza jumla ya mechi 24.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Nyoni ambaye alifunga bao hilo pekee alisema kuwa wao wamepania kila mechi kupata pointi tatu na alifanikiwa kufunga bao hilo baada ya mabeki wa Yanga kuwabana wafungaji wa Simba, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na John Bocco.

Endapo Simba itatwaa ubingwa wa Tanzania Bara, itapata nafasi ya kuliwakilisha Taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika msimu ujao.
Mashabiki wa timu ya Simba wakishangilia kwa furaha mara baada ya ya timu yao kufunga goli.

Kikosi Simba kilikuwa: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Nicholas Gyan/ Paul Bukaba, Yusufu Mlipili, James Kotei, Jonasi Mkude, Asante Kwasi, Shomari Kapombe, John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.

Yanga:Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Said Makapu, Yusuph Mhilu, Papy Tshishimbi/Emmanuel Martin, Obrey Chirwa, Raphael Daud/ Juma Mahadhi na Ibrahim Ajibu/ Pius Buswita
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: